Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Gimbi Dotto Masaba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kutoa mchango wangu wa maandishi, juu ya mwingiliano kati ya Serikali za Mitaa, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Wizara ya Maliasili na Utalii katika utunzaji wa mazingira.
Mheshimwa Mwenyekiti, kuna mwingiliano unaokinzana kati ya Taasisi za Serikali nilizozitaja, katika utunzaji wa mazingira jambo ambalo limefanya zoezi la utunzaji wa mazingira kuwa gumu. Ugumu huo

unasababishwa na kukosekana kwa Sera moja au Sheria moja inayoweka uturatibu wa kuhifadhi mazingira.


Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Halmashauri za Wilaya zina Sheria ndogo zinazoruhusu, mathalani, kuvuna baadhi ya maliasili kama vile madini na magogo kwa ajili ya mbao ili kuongeza mapato ya Halmashauri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) inakataza shughuli kama hizo kwa kuwa dira na malengo ya Wizara hiyo; shughuli hizo zinaharibu mazingira. Wakati Wizara ya Maliasili na Utalii inatenga maeneo ya Hifadhi na Mapori Tengefu na hivyo kukataza wananchi wasitumie maeneo hayo kwa shughuli zao za kiuchumi. Halmashauri zinakuwa na uwezo wa kutoa vibali vya matumizi ya maeneo hayo au Wizara ya Ardhi nayo inaweza kutoa maelekezo tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mkanganyiko huo, utunzaji wa mazingira unaweza kuwa mgumu kutokana na kuwa na vyombo zaidi ya kimoja, vinavyoshughulika na mazingira kwa namna moja au nyingine. Kwa sababu hiyo, napendekeza na kushauri kwamba, Serikali iwe na Sera moja ya mazingira, Sheria moja ya mazingira na chombo kimoja chenye mamlaka na masuala ya mazingira. Kwa mantiki hiyo, Wizara yoyote au Halmashauri yoyote ambayo itakuwa na shughuli ambayo itaathiri mazingira, basi Wizara au Halmashauri hiyo ilazimike kuomba kibali cha kuendesha shughuli hiyo kutoka katika Wizara au Taasisi itakayokuwa imepewa mamlaka ya kusimamia mazingira.


Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kutumia nafasi hii kuzungumzia utunzaji wa mazingira usio na tija. Katika taaluma ya uhifadhi wa mazingira, uhifadhi wenye tija ni ule ambao unafanyika, lakini wakati huo huo kunafanyika pia uvunaji wa mazao yanayotokana na uhifadhi huo, kwa matumizi ya binadamu. Dhana hii ya uhifadhi na matumizi ya rasilimali zinazotokana na uhifadhi huo, ndiyo inayoitwa utunzaji endelevu wa mazingira (Sustainable Environmental Management).


Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu ipo misitu mingi ambayo imetangazwa na Serikali kuwa ni sehemu ya Hifadhi za Taifa na kwa sababu hiyo, Serikali imepiga marufuku uvunaji wa aina yoyote katika misitu hiyo. Matokeo yake ni kwamba, yapo magogo mengi yanaoza katika misitu hiyo na Taifa halipati faida yoyote kutokana na uhifadhi huo. Kwa mfano, Msitu wa Shengena katika Wilaya ya Same, umetangazwa kuwa ni Hifadhi na kwa sababu hiyo wananchi wa maeneo hayo hawaruhusiwi kufanya lolote katika msitu huo. Matokeo yake, miti mingi katika msitu huo imezeeka, magogo yanaoza, wananchi hawapati faida na wala Serikali haipati faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira kama hayo, halmashauri zenye mazingira yanayofanana na yale ya Wilaya ya Same zipewe mamlaka ya kutoa vibali vya uvunaji wa mazao ya misitu kwa usimamizi wa Maafisa Misitu wa Wilaya husika na watakaopata vibali hivyo vya uvunaji waelekezwe pia namna ya kupanda miti ili misitu hiyo iwe endelevu na hatimaye kuwa na utunzaji wa mazingira ambao una faida kwa wananchi na kwa Serikali pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.