Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Lucy Fidelis Owenya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia. Serikali imekuwa ikija na Mipango mipya tofauti kila miaka mitano. Je, ni kwa kiasi gani kwa kipindi kilichopita Serikali iliweza kutekeleza Mipango yake? Je, katika Mpango huu vyanzo vya mapato vitapatikana wapi ukizingatia baadhi ya wahisani wamejitoa kusaidia nchi yetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge lako Tukufu kila mwaka Serikali imekuwa ikitueleza inataka kuongeza watalii wafike zaidi ya milioni moja wanaoitembelea Tanzania. Nchi yetu ina vivutio vingi sana kupita nchi nyingine Afrika Mashariki, lakini kuja Tanzania ni gharama sana kuliko Kenya, Uganda au Rwanda. Hii inatokana na kutokuwa na usafiri wetu wa anga kutoka nchi za Ulaya na Marekani. Je, Serikali ina mikakati gani ya kufufua Shirika letu la ATCL ili kuweza kuimarisha na kukuza utalii kwa lengo la kupata watalii wengi kuja moja kwa moja mpaka Tanzania badala ya kupitia Kenya inayofanya Utalii wa Tanzania uwe ghali sana?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa jinsi gani Mpango huu utatekelezwa, kutengeneza reli zetu angalau ziweze kuwa na mabehewa ya mizigo badala ya mizigo na makontena yanayosafirishwa kwenda nchi jirani kama Kongo, Zambia, Rwanda kutumia barabara. Hii inachangia sana kuharibu barabara zetu haziwezi kudumu. Mfano, barabara kutoka Chalinze- Dodoma tu, tayari barabara hii imeharibika kabisa na tangu ijengwe haina hata zaidi ya miaka 20? Serikali itueleze ina mpango gani wa kufufua reli kwa uhalisia siyo kwa maandishi ya hotuba.
Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima, lakini hadi sasa hivi bado kilio chetu ni cha kutegemea mvua na wakulima wengi hawana mitaji. Wengi vijijini bado wanatumia ng‟ombe kulimia na wengi hawapati elimu ya kutosha kuhusu mazao ya biashara na Serikali haisaidii ni kwa jinsi gani itawezesha kuhusu kilimo cha umwagiliaji ili waweze kulima kwa kipindi chote mwaka mzima. Je, Serikali ina mikakati ya kuzalisha mbegu za kisasa hapa nchini ili ziwe kwa bei nafuu?
Mheshimiwa Naibu Spika, mbegu nyingi zinatoka nchi za nje na tukumbuke mbegu kutoka nje zinaagizwa kwa fedha za kigeni ukizingatia fedha yetu thamani yake inashuka kila siku na deni la Taifa linakua kila siku. Je, Serikali inachukua mkakati gani, kuendeleza kilimo ili tuondokane na kilimo cha kutegemea mawingu, kilimo cha jembe la mkono badala ya kuleta kauli mpya kila wakati?