Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Saumu Heri Sakala

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujikita katika mchango wangu moja kwa moja katika suala la mazingira. Mazingira yaliyoimarika ni suala muhimu sana kwa mustakabali wa nchi yetu na dunia kwa ujumla na ndiyo maana leo kila pembe ya dunia kama siyo nchi huunda vikundi ama asasi mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu ya mazingira. Sasa basi nikija katika nchi yetu uharibifu wa mazingira unazidi kuwa mkubwa kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii yote ni kwa sababu, kwanza, elimu ya mazingira kwa wananchi ni duni mno haiwafikii wananchi kwa ukamilifu unaotakiwa. Nitolee mfano Wilaya ya Kondoa na Chemba ambapo kule napo uharibifu ni mkubwa kutokana na ukosefu wa elimu watu
wanakata miti ovyo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kuni, mkaa na hata maandalizi ya mashamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo linasababisha uhaba wa mvua na ukosefu wa maji tena kwa kiasi kikubwa mno, lakini mpaka leo hii watu walio wengi wa Kondoa na Chemba hawaelewi ni kwa nini wanakosa maji. Wenyewe wanasema ni “wenye ardhi ndiyo hawataki na maji yao.” Sasa ukiwauliza hao wenye ardhi ni akina nani na wako wapi wanakujibu, hata wao wanasikia tu kuna wenye ardhi. Unaweza kuona ni kwa kiasi gani elimu inahitajika katika maeneo mengi ili kunusuru mazingira yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine linalochangia uharibifu wa mazingira ni pamoja na kukosa nishati mbalimbali katika kupika hasa ukizingatia familia nyingi katika nchi yetu bado uwezo wao ni wa kutumia kuni na mkaa hivyo mazingira yetu bado yataendelea kuharibiwa sana kama bado elimu na nishati mbadala havitatolewa kwa makini na ukamilifu. Tunasikia kuna mkaa wa mabaki ya vyakula lakini bado elimu hiyo wananchi hawawezi kabisa na hata vifaa vya kutengeneza mkaa huo pia havipatikani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, Wizara hii badala ya kujikita kwenye kutembelea mazingira na kutoa miti ya kupanda ni vyema ingejikita katika kutafuta elimu itakayosambazwa katika shule za msingi na sekondari ambako huko watatoa elimu juu ya nishati mbadala, kupeleka vifaa, kufundisha masuala ya majiko banifu ambayo majiko hayo hupatikana mjini tu. Hivyo wakipatikana walimu hawa wa kufundisha juu ya utunzaji majiko banifu na utumiaji wa mikaa inayopatikana kutokana na mabaki ya vyakula tutapata faida mara mbili; kwanza, itaongeza ajira kwa vijana na tutakuwa tumepiga hatua katika utunzaji wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa mwisho ni juu ya elimu sahihi kuhusu mazingira. Ufike wakati sasa elimu ya mazingira itolewe katika kuanzia ngazi ya Kaya hadi Taifa.