Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

HE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante angalau kwa dakika tano. Nashukuru kwa kunipa nafasi, naomba kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya. Mwisho, nimpongeze Waziri kufanya ziara kwa kuja kutembelea Mkoa wetu wa Rukwa na hatimaye kuliona Ziwa Rukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ziwa letu linakauka, ziwa ambalo ndiyo jina la Mkoa wetu wa Rukwa, lakini kwa sasa linaelekea kukauka. Nakuomba Waziri, Mheshimiwa January Makamba uendelee na nguvu hiyo na utenge fedha kwa ajili ya kusaidia Ziwa letu la Rukwa lisiweze kukauka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umenipa dakika tano lakini naona zinataka kunichanganya ni chache sana. Niombe tu kwamba katika huu Mfuko wa Mazingira basi ianzishwe sheria kama ambavyo ilivyo sheria kwenye mifuko mingine. Hakuna maendeleo bila uwekezaji katika mazingira, hakuna maendeleo bila utunzaji wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kubwa ambalo nataka kuongelea leo ni suala la Serikali yetu kupiga marufuku viroba. Hili nataka kuliongelea kwa uchungu kidogo kwa sababu, sisi ndiyo Wawakilishi wa wananchi. Wananchi wanatakiwa sisi tuwatetee ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mtu ambaye anapinga uharibifu wa mazingira, lakini suala la kupiga marufuku viroba tungelipa nafasi kidogo. Kuna watu wamenunua viroba hivi, kuna watu wametumia fedha nyingi sana, kuna watu wamekopa fedha nyingi na hatimaye tumezuia biashara hii ambayo naamini kabisa biashara hii ilikuwa halali haikuwa haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimuulize Mheshimiwa Waziri kama biashara hii ilikuwa halali na leo hii tumepiga marufuku, wananchi hususan wafanyabiashara wa Mkoa wa Rukwa na Jimbo la Sumbawanga Mjini walinunua kwa wingi wakitegemea wakienda kuuza watapata faida, lakini tumevizuia. Niombe tu kauli ya Serikali kwa hawa ambao wamezuiliwa je, hatuna haki ya kuwalipa fidia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tuliangalie hili kwa uchungu, kwa hisia kali. Leo hii mtu amekopa fedha benki, kachukua fedha zile kaenda kufanya biashara, amekopa viroba vyake akauze, leo hii tumevizuia, hebu niambie ni hisia gani anapata na uchungu gani mkubwa anaoupata. Kuna mtu amejiua Dodoma hapa, leo hii ukienda kwenye vituo vya Polisi kuna viroba vimejazana, matokeo yake wanachukua kimoja kimoja wananyonya. (Kicheko)
Mheshimiwa Waziri Mkuu nikuombe sana, kwa sababu nahisi, najua uchungu wa mtu anavyofilisika. Kwa hiyo, hili liangalieni upya, litoleeni maelezo, ni bora tukazuia production, bora tukazuia kule ambako vinatengenezwa, tuwape muda wafanyabiashara hao waliovinunua wauze mpaka viishe, naomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu kule kuna wafanyabiashara watano, mpaka leo wamekamatiwa mali zao, wamefilisika na nyumba zao zinauzwa. Nimwombe sasa Mheshimiwa Waziri anapokuja kutujibu hoja yetu hapa, naomba hili alitolee ufafanuzi, ni lini hawa wafanyabiashara wataruhusiwa kuuza viroba vyao au Serikali itoe tamko iwalipe fidia ichukue viroba wakaviteketeze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu kubwa ilikuwa ni hiyo, kwa sababu sioni mantiki yoyote ya kile kitu ambacho ilikuwa ni halali, mtu akachukua fedha zake akaenda akanunua tena amenunua kiwandani, siyo haramu hiyo hapana, amenunua ili akauze apate faida, sisi tunazuia tunawanyang’anya tunakwenda kuvitunza kwenye maeneo mengine watu wanaumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge ndiyo wawakilishi wa wananchi, tunatakiwa tuwatetee wananchi, tusipowatetea humu ndani hakuna kwa kuwatetea kwingine. Naomba sana tuungane katika hili, nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu aje atusaidie hili. Wananchi hawa ni wa kwetu sisi wote, ndiyo kazi yetu kuwawakilisha ndani ya Bunge, siyo kila kitu tunakiunga mkono hapana! Katika hili Mheshimiwa Waziri Mkuu nakuomba sana, binafsi kwa niaba ya wananchi nikuombe sana usaidie jambo hili waweze kuliruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.