Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia muda wa kuchangia eneo hili la TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Waziri wa TAMISEMI kwa kazi kubwa anayoifanya na wasaidizi wake, hongera sana Mheshimiwa Waziri. Kazi unayoifanya Watanzania wanaiona na hotuba yako inaonesha kabisa mwelekeo wa bajeti yetu, lakini pia mwelekeo wa mambo
ambayo yamefanywa katika bajeti iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kuchangia eneo la elimu. Ni kweli kabisa kuna tofauti kubwa kati ya elimu bila malipo na elimu bure. Hii tofauti ipo na Serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa kufafanua majukumu ya Serikali ni yapi, lakini pia majukumu ya jamii au wananchi ni yapi. Ni kweli kwamba tofauti kati ya elimu bila malipo na elimu bure inapaswa ifike kikamilifu kwa wananchi wetu kule chini.
Mheshimiwa Spika, ni jukumu letu sisi kama wanasiasa kuwaeleza wananchi, lakini pia ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wetu wa kawaida wanajua majukumu yao. Uelewa wa wananchi bado haujakaa sawasawa na kwa maana hiyo, ninaishauri Wizara ifikishe
elimu hii kwa kutumia Idara ya Elimu kwa ngazi ya chini kabisa ili wananchi wajue majukumu yao ni yapi kama yalivyofafanuliwa na miongozo ya Serikali.
Kimsingi suala la elimu bila malipo lina changamoto zake na ndiyo maana tuko hapa kwa ajili ya kutatua changamoto hizo. Serikali ilipoamua kupeleka fedha katika shule za msingi na sekondari imekwenda sambamba na kubana matumizi ambayo yanasababisha baadhi ya maeneo kutotekelezwa vizuri katika utoaji wa elimu.
Mheshimiwa Spika, naomba niliongelee eneo moja tu la mitihani. Ni kweli kabisa ili mwanafunzi aweze kujifunza, anahitaji kichocheo cha kuwa na majaribio na mitihani ya mara kwa mara. Kwa maana hiyo basi, pamoja na kwamba tunakwenda vizuri katika kutoa elimu hii bila malipo, lakini tunaiomba Serikali iongeze fedha ambazo zitawasaidia walimu kutoa majaribio ya mara kwa mara ili tuweze kuongeza ufaulu wa wanafunzi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine muhimu ni eneo la miundombinu ya shule zetu. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri inaonesha wazi kwamba tunalo tatizo kubwa la miundombinu katika shule zetu, tuna matatizo ya vyoo, tuna matatizo ya majengo na matatizo ya nyumba za walimu.
Nadhani sasa umefika wakati wa Serikali kutenga fedha ya kutosha na kuzisimamia vizuri Halmashauri zetu ili fedha nyingi itengwe katika maeneo haya kuondoa hizi changamoto ambazo tumekuwa tukizieleza kila siku.
Mheshimiwa Spika, suala la kuboresha miundombinu ya elimu liende sambamba na kuangalia shule zenye mahitaji maalum hasa zile zinazopokea watoto wenye mahitaji maalum yaani watoto wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Masasi kuna shule mbili; shule moja ilipata fedha katika mwaka wa fedha uliopita na kuboresha kwa kiwango kikubwa shule moja kwa ajili ya watoto wenye ulemavu, lakini shule ya msingi Lugongo hali ni mbaya na hakuna vifaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine muhimu tunapozungumzia elimu ni suala zima la idadi ya walimu katika shule zetu. Umefika wakati Serikali iseme, wanapofanya majumuisho Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI atuambie, ni lini hasa wanaajiri walimu wa shule za msingi na ni lini hasa
wanaajiri walimu wa shule za sekondari.
Mheshimiwa Spika, hata tufanye vipi, kwa uelewa wangu na kwa uzoefu wangu wa eneo la elimu, ni afadhali mwanafunzi asomee kwenye mwembe lakini mwalimu awepo. Mwalimu ndiye ambaye ana msaada mkubwa wa kumpa maarifa mwanafunzi. Tuna changamoto kubwa na
tumekuwa tukisema muda mrefu sana kwamba pamoja na kwamba tumetatua changamoto ya madawati, pamoja na kwamba tunaendelea kujenga majengo, lakini kama walimu hawapo wa kutosha, hali haiweze kuwa nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna shule nyingine zina walimu wanne, wanafunzi 600. Hali haiwezi kuwa sawasawa katika kujifunza kwa watoto. Katika Jimbo la Masasi tunapungukiwa na walimu takribani 219 wa shule za msingi, tunapungukiwa na walimu 60 wa masomo ya sayansi; wanatakiwa walimu 84, wapo walimu 24 tu. Hatuwezi kuongeza ufaulu wa watoto katika mazingira ya namna hiyo. Kwa hiyo, lazima Serikali ifike wakati iajiri walimu hawa.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo mambo haya yanatakiwa tuwianishe. Tunajenga mazingira mazuri ya kujifunzia watoto, lakini pia tunatengeneza mazingira ya maslahi kwa walimu wetu. Ni kweli kwamba Serikali inalipa madeni, hasa madeni yaliyo nje ya mshahara kwa walimu wetu. Pia ni kweli kwamba walimu bado wana malalamiko, tuendelee kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto zinazowakabili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2016 Serikali iliwapandisha baadhi ya walimu madaraja. Katika Jimbo langu, walimu 397 wa Masasi walipandishwa wakapokea mshahara mmoja baadaye wakashushwa. Hawa ni walimu wa Jimbo moja tu, eneo moja tu, walimu wana malalamiko, wanakata tamaa. Ulishapewa mshahara, baadaye unashushwa. Tunaomba Serikali iangalie namna gani inaweza kuyaangalia mazingira haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wapo walimu ambao walitakiwa kupanda madaraja kutoka mwaka 2014 mpaka leo hawajapandishwa madaraja. Mwaka 2010 Serikali iliondoa annual increment kwa walimu na ilikuwa pengine ni tofauti na mazingira ya mikataba waliyosaini wakati wanaajiriwa,
lakini mpaka leo walimu hawa hawajaambiwa kwa nini annual increment imeondoka, lakini hata kama wanaambiwa, bado wanabaki kuwa na malalamiko.
Tuangalie mazingira ya walimu ili tuone namna gani walimu hawa wanaweza kuwa na motisha pia ya kufundisha.
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, nizungumze kidogo eneo la uratibu katika shule zetu. Ipo changamoto hasa maeneo yale ambayo yana changamoto ya usafiri. Waratibu wa Elimu wa Kata wanashindwa kufanya kazi yao ya uratibu vizuri kwa sababu wengi hawana usafiri. Tunasikia kuna baadhi ya maeneo, waratibu wana usafiri, lakini tungeomba sasa tuyaangalie na maeneo ya kusini hususan katika Jimbo langu la Masasi, waratibu wetu wapewe usafiri angalau wa pikipiki ili waweze kuyafikia maeneo ya shule zao mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika, nizungumze kidogo katika eneo la afya. Kama kuna eneo lina changamoto kubwa sana ni eneo la afya. Tuna tatizo kubwa. Katika Jimbo langu, tuna tatizo linaloendana na upungufu mkubwa wa watumishi, hili ni tatizo kubwa sana!
Mheshimiwa Spika, tuna zahanati lakini hazina watumishi wa kutosha; tuna upungufu na tumeomba kupatiwa watumishi wa hospitali, takribani watumishi 56 wa huduma ya afya lakini hakuna hata mmoja aliyeajiriwa mpaka sasa. Huu ni wakati ambapo Serikali inatakiwa kusema ni lini inaajiri watumishi wa afya ili tuweze kupata rasilimali watu katika maeneo yetu ya huduma za afya?
Mheshimiwa Spika, katika eneo la afya hususan katika Jimbo langu bado kuna changamoto kubwa. Pamoja na kupungua kwa watumishi, lakini hatuna magari ya wagonjwa. Wilaya nzima kuna magari mawili tu ambayo moja ni bovu na moja ndiyo linalofanya kazi; siyo rahisi kuweza kuwapeleka wagonjwa wanaohitaji msaada wa haraka hospitali.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tungependa katika eneo la huduma za afya kuwe na upatikanaji wa dawa kwa wakati; hili pia limekuwa ni eneo lenye changamoto kubwa sana. Katika Hospitali yetu ya Mkomaindo mwaka 2014 ulifanyika ubadhirifu wa fedha za dawa.
Mheshimiwa Spika, niliwahi kuuliza swali, niliwahi kueleza masuala haya mara nyingi, lakini kila Waziri anapotoa majibu hapa, sijapata majibu ambayo yanaridhisha ni kwa nini hatua hazichukuliwi kwa watu ambao walihusika na ubadhirifu huu wa dawa mwaka 2014?
tunaomba Serikali ichukue hatua katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni ujenzi wa jengo la utawala. Jimbo langu la Masasi halina jengo la utawala lakini kwa bahati mbaya sana, fedha ambazo zilikuwa zimeā€¦
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.