Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu na nakushukuru wewe kunipa nafasi. Naomba nichukue nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa Ofisi ya Spika, Waziri Mkuu, Wabunge wenzangu, kwa salamu za faraja mlizotupatia tulipompoteza Mama yetu mwezi wa Pili. Tulipokea msaada mkubwa sana tunashukuru sana, hasa ule mfuko wa faraja Mungu awabariki na
tunamwombea mama yetu apate mapumziko ya milele. Amina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kabisa kuunga mkono hoja na nina sababu; kwanza natambua kazi nzuri zinazofanywa na Serikali hii ambazo ni kushughulika na mambo mengi ambayo yalisuasua zamani. Tumeona wahenga wanasema kila zama na kitabu chake, ni hakika
kitabu cha Awamu ya Tano kitakuwa cha pekee kidogo na upekee wake ni namna Serikali ilivyojipanga kushughulikia matatizo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona suala la madawati lilikuwa sugu mashuleni limepata ufumbuzi wa haraka kabisa. Tumeona ubadhirifu Serikalini umepata ufumbuzi wa haraka kabisa ingawaje unaendelea, Utumishi wa Serikali umekuwa na nidhamu, uamuzi wa kuhamia Dodoma wa haraka kabisa, umesuasua miaka mingi. Tumeona dawa za kulevya zikishughulikiwa kwa haraka. Kwa hakika wananchi wa
Jimbo la Nkasi Kusini wameniambia niunge mkono juhudi zote zinazofanywa na Serikali hii kama mabosi wangu walionileta hapa kuwawakilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ajenda yetu sasa ni viwanda na katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukurasa wa 19, Ibara ya 28, imezungumza suala la uchumi wa viwanda. Katika uchumi huu wa viwanda, historia inatuambia mahali ambapo viwanda vilianzia kulikuwa na maandalizi muhimu sana kwanza na mojawapo ni elimu. Elimu lazima iwe na msisitizo wa sayansi na teknolojia, masomo ya kisayansi lazima yawekewe msisitizo mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninavyozungumza hapa Wilaya yangu ya Nkasi, Walimu wa Sayansi wako 14 tu katika shule 22, kati ya hizo nyingine zina kidato cha kwanza mpaka cha sita. Kwa hiyo, hatuwezi kufanikiwa kama walimu wa sayansi hatuwapati, walimu wa ufundi hatuwapati, hatuwezi. Kwa hiyo, naomba tuleteeni walimu ili tushiriki katika uchumi ambayo ni ajenda yetu ya sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hatutaweza kufanya vizuri katika kilimo. Kilimo kinahitaji elimu, kilimo kinahitaji sayansi na jinsi kilimo kinavyosukumwa katika nchi hii, niko miaka sita sasa Bungeni, sijaridhika. Naona kilimo kama kinasuasua kila siku, kinaenda ili mradi kiende, wakati kilimo mchango wake kwa pato la Taifa ni mkubwa, mchango wake kwa ajira ya Watanzania ni mkubwa na kilimo ndicho kitakachoendeleza ajenda hii ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uanzishwaji wa viwanda Ulaya, kitu cha kwanza ilikuwa mapinduzi katika kilimo ili kutengeneza ready market. Maana watu wakilima vizuri watakula chakula, watazaliana, watakuwa sasa wananunua chakula hicho, bidhaa mtakazozalisha kwenye viwanda, watakuwa na afya na nguvukazi itakuwepo. Sasa kwa nini kilimo kinasuasua miaka yote na kinabeba watu wote wanyonge? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri watu wanaopelekwa kwenye kilimo kusimamia wawe wakakamavu na hatua zichukuliwe. Kwa nini mkulima apate mbolea kwa kuchelewa? Sababu zinakuwa zinatolewa lakini zote hazitoshi zote. Naomba ufike wakati tuchukue hatua kakamavu, hasa katika suala la ucheleweshaji wa pembejeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mchezo pia katika utoaji wa pembejeo zinakuwa fake, wenzangu wamesema. Mwaka huu mimi ni mmojawapo wa watu walioathirika, nilinunua madawa fake ya kupalilia, ya magugu, jambo hili si jema sana na wasimamizi mpo, vitu hivi vinarudisha wakulima nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo ya utafiti wa mambo ya kilimo, ukurasa wa 21; Wilaya ya Nkasi tuna Kituo cha Utafiti Mirundikwa, hakijasaidiwa vya kutosha, hakina pesa ya kutosha. Naomba tusaidiwe ili tuweze kujitahidi kupata mbegu kwa karibu, sasa hivi mbegu tunaagiza nje bila sababu za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni nilikuja hapa nikatoa kilio changu juu ya kunyang’anywa Shule ya Mirundikwa! Leo hii nipende kuishukuru Serikali, nimepata pesa zaidi ya milioni 259 kwa ajili ya kujenga bweni na kuendeleza madarasa. Niikumbushe Serikali, nilisema wakati ule kwamba, miundombinu iliyokuwepo wakati ule ilikuwa na zaidi ya thamani ya milioni 871 kwa mujibu wa Mthamini wa Serikali kwa hiyo, bado kuna safari ya kutosha ingawa si haba, lazima tushukuru. Ninaposema Serikali hii ikiambiwa jambo inatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nililia hapa kila mtu aliniona, sauti yangu niliipaza, nikapata nafasi ya kumwona Mheshimiwa Rais na kumweleza kwa nafasi mbalimbali, lakini sasa napata matokeo chanya. Sasa kwa nini niseme hafanyi kazi? Kwa nini niseme hashughulikii matatizo ya wananchi? Nitakuwa mtu wa ajabu sana. Kwa hiyo, anafanya kazi vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa katika maeneo niliyoyasema waangalie, Mawaziri watusaidie. Waziri wa Elimu upungufu wa walimu kwangu ni 647, hatuna walimu 647. Upungufu wa nyumba na vyumba vya madarasa ni 1,100. Upungufu wa nyumba za walimu 900, ni mkoa na wilaya iliyo pembezoni kabisa! Mtutupie macho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho Mji wa Namanyere umeshakua vya kutosha, tunaomba uwe ni Halmashauri ya Mji. Mheshimiwa Malocha amekuwa akizungumza upande wake na wenyewe huko. Hiyo inatakiwa iwe wilaya ni sehemu kubwa. Mwisho zaidi tunaidai NFRA zaidi ya milioni 200 kwenye Halmashauri yetu. Halmashauri yetu sasa haiwezi kufanya kazi kwa sababu, mapato hayatoshelezi. Kwa hiyo, kama mtatusaidia mtusukumie hili jambo liwezekane ili Halmashauri ipate nguvu na uwezo wa kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu wote waliozungumzia juu ya asilimia 10 kwamba, hazitoki. Kama kuna mtu aliziona basi labda ni kwa sababu kwetu hazitoki. Tunaiomba Serikali ihakikishe kwamba asilimia 10 zinatoka ili ziende kwa vijana na akinamama kwa mwaka huu. Kwenye bajeti ya mwaka huu zimeingizwa, lakini sasa tulikuwa hatuzipati na hatuzipati kwa sababu ya mapato machache ya Halmashauri, wanaona vipaumbele wanavyokuwanavyo vinawafanya wasizitumie pesa hizi kupeleka kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia wanamsifu sana Mheshimiwa Mavunde. Hiyo habari yako ya mikopo kwa vijana kuwezesha vikundi mbalimbali kwetu haijafika. Tusaidie au tupe namna ambavyo tutaweza kushiriki twende kwa pamoja na wenzetu ambao wanasifia kwamba
unafanya vizuri katika eneo hili. Binafsi, kwangu mimi bado elimu haijafika na vijana wangu wote ni wachapa kazi wanahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niongelee suala zima la uchapaji kazi, kama ilivyo Serikalini muangalie na kwenye kilimo. Kilimo, kuna watu wanajiita wakulima, lakini ni wazururaji tu na hakuna mtu anayewaangalia! Hili haiwezi kutuletea tija! Wasimamizi, hasa watawala, tujitahidi
kuhakikisha kwamba, kila mtu katika eneo lake awe anafanya kazi inayotambulika na kufanya kazi kwa bidii kwa masaa mengi. Isiwe kama ni ajenda ambayo haina msimamizi; tutakuwa tunazungumza kila wakati kwamba tunaondoka hapa tulipo kiuchumi, kumbe tunafuga watu
ambao… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)