Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nikushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Mpango huu wa Miaka Mitano unaeleweka vizuri iwapo utasomwa katika context yake ya kwamba Mpango huu unatokana na Mpango Elekezi wa Miaka 15. Ukishauweka katika context ya miaka 15 unaelewa kwamba kilicholetwa hapa kwa miaka hii mitano ni hatua ya pili ya utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Miaka 15. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukishaelewa hivyo, unaweza ukapunguza sana kejeli ambazo zinatolewa na baadhi ya Wabunge humu ndani. Hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huu ilikuwa kutanzua vikwazo vya uchumi; ni hatua nzuri ambayo imefikiwa kwa kipindi cha miaka mitano tunachokimaliza msimu huu wa 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, tunapokuja na Mpango wa miaka mitano inayoanzia mwaka 2016/2017, tunazingatia pia uzoefu tulioupata miaka mitano iliyotangulia. Ukiangalia katika Mpango huu, miaka mitano iliyopita ilieleza bayana, pamoja na kutanzua vikwazo vya uchumi, pia kipindi hicho cha miaka mitano iliyotangulia kilienda sambamba na kubaini maeneo ya vipaumbele. Maeneo ya vipaumbele yaliyobainishwa ni pamoja na Miundombinu, Kilimo, Viwanda, Rasilimali Watu, Huduma za Kifedha, Utalii na Biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapotoka kwenye awamu ya kwanza na tunapokwenda kwenye awamu ya pili ambayo itachukua tena miaka mitano, tumechagua eneo la viwanda kama eneo mahususi la kulifanyia kazi. Mpango huu ukiusoma kwa umakini na ukaulewa, utaelewa ni kwa nini sasa tumechukua viwanda na kwa nini Mpango huu umeitwa kama kipaumbele kujenga misingi ya uchumi wa viwanda? Tunapoongelea viwanda, tunaenda sambamba na miundombinu ambayo itafanya viwanda viimarike lakini biashara iimarike. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mpango huu umebainisha vizuri maeneo ya ujenzi wa barabara, reli, bandari, lakini pia umeeleza miradi mahususi ambayo itaifanya Tanzania yetu iwe Tanzania mpya, Tanzania ambayo inakwenda kujibu kero za vijana, akinababa na akinamama wa Taifa hili. Ukiusoma katika context hiyo, unakubaliana nami kwamba Mpango huu wa miaka mitano kama sehemu ya utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Miaka 15, Mpango huu umekaa vizuri kwenda kutatua matatizo ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Serikali nzima ya Awamu ya Tano kwa kujifunza kutokana na uzoefu wa miaka mitano iliyotangulia na kuja na Mpango madhubuti utakaolijenga Taifa letu vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninavyouangalia Mpango huu na namna ulivyokaa, nina maeneo machache ambayo ningependa nishauri. Ukiangalia Mkoa wa Ruvuma ambao lango lake lipo katika Jimbo ninaloliongoza, Jimbo la Madaba unaona kwamba Mkoa wa Ruvuma umejaa fursa nyingi sana ambazo kama zitatumiwa vizuri na Mpango huu, kwa hakika Tanzania itakuwa nchi ya neema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zipo barabara muhimu ambazo zitatakiwa zijengwe na ziimarishwe ili Mpango huu wa viwanda uweze kuwanufaisha wananchi wa Jimbo la Madaba na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla ambao kwa asilimia kubwa wanachangia sana pato la Taifa na wanachangia sana chakula kinacholisha Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Jimbo langu la Madaba linapakana na Wilaya ya Ulanga, lakini kufika Wilaya ya Ulanga nahitaji kufika mpaka Mikumi na baadaye niende Ifakara ndipo niende Ulanga. Wakati wananchi wangu wa Kijiji cha Matumbi wanatumia siku sita kwa mguu au nne kufika katika Wilaya ya ulanga, lakini wanatumia siku mbili kwa mguu kufika mpakani mwa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na upande wa pili wa Malinyi.
Mheshimiwa Spika, hicho tayari ni kikwazo kikubwa sana cha uchumi kwa maendeleo ya maeneo yote mawili. Pamoja na kwamba Mpango huu bado haujabainisha nini kitafanyika, haujafafanua, nafikiri kwa sababu Mpango huu una sifa ya kujifunza kwa Mipango iliyotangulia, basi tuendelee kuangalia lile eneo ambalo linapakana na Jimbo la Madaba kama sehemu moja muhimu ambayo itachangia sana uchumi wa wananchi wa maeneo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia imeelezwa vizuri sana kwamba Mkoa wa Lindi unapakana na Mkoa wa Ruvuma, nalo ni eneo muhimu sana kama tunataka kuimarisha uchumi wa wananchi wale kupitia viwanda kwa sababu tunazalisha malighafi ya kutosha, tunahitaji kusafirisha, lakini tutazalisha bidhaa nyingi za viwandani, tutahitaji ziende Lindi, Ifakara, Mahenge na maeneo mengine ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa miaka mingi sana Mbunge aliyemtangulia Waziri Mheshimiwa Jenista Mhagama, Mbunge Profesa Simon Mbilinyi, aliyestaafu, alianza kuongea sana kuhusu miradi ya NDC, hususan mradi wa Mchuchuma na Liganga. Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Peramiho, ambaye sasa kipande cha Jimbo lile kimekuwa Jimbo la Madaba, ninaloliongoza sasa, kwa miaka kumi amesimamia ajenda hiyo ya mradi wa Mchuchuma na Liganga.
Mheshimiwa Spika, mradi ule kama utafanikiwa kwa kiwango hiki ambacho umeelezwa katika Mpango huu, kwa hakika utatukomboa sana wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, utawakomboa sana wananchi wa Madaba na Jimbo la Peramiho. (Makofi)
Mheshimwa Spika, ni vizuri sasa, kwa vile maandalizi ya kuanza ku-explore ule mradi wa Liganga Mchuchuma, ni vyema sasa barabara inayotoka Wilaya ya Ludewa kufika Madaba iimarishwe ili kwamba wananchi wa pale waweze kunufaika na ule uchumi, lakini pia ndiyo barabara inayokuja kuunganisha na barabara ya Makambako kuja Dar es Salaam, kwa ajili ya kusafirisha mali na bidhaa zitakazozalishwa katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, tuna usemi wa Kiswahili, Waswahili wanasema, “Siku ya kufa nyani, miti inateleza.” Wakati nipo nje ya Bunge hili, kuna wakati nilikuwa naona kuna baadhi ya hoja zenye mashiko kutoka upande wa pili wa upande wangu wa kulia, lakini kadri ninavyozidi kukaa ndani ya Bunge hili, katika hiki kipindi cha miezi kama sita hivi nimekaa hapa, nazidi kuona kwamba hoja zenye mashiko zinazidi kupungua. Naamini sasa kweli miti inateleza. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna wakati ambapo hoja ya ufisadi ndiyo ilikuwa mhimili mkubwa wa kushikilia. Leo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli alipoisimamia hoja ya kutumbua majipu na kuondoa mafisadi, wale wale ambao walikuwa wameshikilia hiyo nguzo, wanamlalamikia na wanamlaumu. Ama kweli Waheshimiwa Wabunge ni lazima tujipime wakati mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inanisikitisha sana ninapoona mtu anaji-contradict mwanzo hadi mwisho wa hotuba yake. Anaanza na kusema Baraza la Mawaziri halifanyi kazi, halifai. Baraza hili ni lile lile la Awamu ya Nne, wanabadilishana nafasi, halafu baadaye anasema Mheshimiwa Waziri fulani umenifaa sana, unafanya sana kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuishi kwa contradiction. Lazima tuwe na consistent katika hoja zetu. Leo nimependa sana…
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, lazima ni-declare interest, approach aliyoitumia Mheshimiwa Ally Saleh, imetujenga sana na imemsaidia sana Waziri wa Fedha kuweza kuboresha Mpango huu wa Miaka mitano wa Maendeleo. Napenda sana tutumie approach hiyo ili kuisaidia nchi yetu na kuwasaidia Mawaziri waweze kutuletea majibu yanayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunalo eneo lingine muhimu sana kwa Jimbo la Madaba…
TAARIFA
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa kanuni ya 68 (8)!
SPIKA: Mheshimiwa Joseph, naona kuna taarifa ambayo haivumiliki...
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika ahsante. Taarifa hiyo siipokei kwa sababu wale ambao walileta ushahidi ndani ya Bunge hili, mimi nikiwa nje ya Bunge hili, kwamba Mheshimiwa Lowassa ni mmoja katika mafisadi wakubwa, ndio hao hao waliomkumbatia na kwenda naye katika kampeni ya Awamu hii ya Tano. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)
MBUNGE FULANI: Wanafiki wakubwa!
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, kwa namna yoyote siwezi kuipokea hiyo taarifa. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha
kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mhagama, muda wako umekwisha. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante.