Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kuchangia kwanza kwa kuangalia ni nini kimetekelezwa kwa Mpango wa Kwanza. Ukiangalia kiuhalisia Mpango wa Kwanza haujatekelezwa kwa asilimia 60 kama ambavyo mmeandika. Ni kwa nini nasema hivi? Mfano mdogo tu kwenye hotuba ya Waziri anatuambia kwamba maji vijijini yameenda kwa zaidi ya asilimia 72 kwamba wananchi wa vijijini zaidi ya milioni ishirini wamepata maji.
Mheshimiwa Spika, sasa mimi nikawa nauliza ni Tanzania ipi imepata maji safi na salama? Mkoa wa Mara, Wilaya ya Tarime, Mji wa Tarime siyo tu vijijini hata mjini hakuna maji. Ile Sera ya mwaka 2002 kwamba maji unapata ndani ya mita 400 ni ndoto. Kwa hiyo, kama takwimu zenyewe ndiyo hizi ni dhahiri mtakuja mtasema mmetimiza kwa asilimia 60 lakini kiuhalisia hakuna kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo mme-document hapa kwamba fedha za maendeleo sasa hivi zitakuwa zinaenda kwa asilimia 40 ya bajeti. Mkumbuke Mpango wa Kwanza tulisema asilimia 35, lakini mtu asimame aniambie kama Serikali hii na naomba sana msiwe mnasema Serikali ya safari hii ya Awamu ya Tano imedhamiria as if sasa hivi ni chama kingine, ni Chama hicho hicho cha Mapinduzi ndiyo mlikuwepo miaka yote…
MHE. ESTHER N. MATIKO: Msitake kutu-fake Watanzania mnakuja hapa mnasema ooh, sasa hivi tumedhamiria, nikiangalia cabinet iliyopo sasa hivi over sixty percent ni ile iliyokuwepo Awamu ya Nne. Mkumbuke kwamba hata Awamu ya Nne tulikuwa tukiongea hapa tukiwashauri, baba yangu Mheshimiwa Wasira alikuwa anakuja hapa anatubeza kwenye Mpango, nilikuwa Waziri Kivuli wa Mpango na bahati nzuri aliyekuwa kwenye Mpango ndiyo Waziri wa Fedha na Mpango sasa hivi. Halafu mkikaa mnasema sasa hivi hii Serikali ina dhamira ya dhati, come on, are you serious? Watu wale wale, chama kile kile tumekishauri, over sixty percent Mawaziri mliokuja madarakani ndiyo wale wale labda mmebadilishwa tu, ulikuwa Waziri wa Katiba na Sheria sasa hivi ni Waziri wa Afya, ulikuwa sijui wapi sasa hivi umeenda pale. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, sasa leo tukisema kwamba tulidhamiria kuimarisha miundombinu ya barabara ambayo ndiyo inaenda kuchochea uchumi wetu na mtu aka-document tukasema Rais, Mheshimiwa Magufuli ndiye aliyekuwa Waziri kipindi hicho na nakumbuka katika vitu ambavyo vilipewa kipaumbele ni ujenzi wa barabara, lakini ndiyo mmejenga kwa asilimia hamsini na tatu.
Mheshimiwa Spika, hivyo ambazo hatukuvipa kipaumbele sana asilimia 20, asilimia sijui ngapi! Asilimia tatu! Halafu tunaishia kuwa na mipango. Kwanza nilikuwa najiuliza, kuanzia jana na-postpone tu. Maana yake nasema nachangaia nini? Tunatoa ushauri, tunasema but nothing is going to be done. Tunachangia nini?
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, naomba sana, tukisimama tuwe kama Wabunge, acha Mawaziri watakuja watajibu kama Serikali. Nashangaa Mbunge anasimama anatetea kweli! Kaka yangu wa Mkuranga, documents za Kambi ya Upinzani, tulicho-document kimetokana na alichokiandika Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, sasa ukianza kusema, nikasema anajidai aah, sijui zimeongezeka 500. Ongeza hizo 500, zinakuwa ni 3000. Sasa 3000 kwa miaka mitano, leo unazitekeleza vipi?
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, taarifa!
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, naomba nishauri na naomba...
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, taarifa!
SPIKA: Taarifa iko upande gani?
MBUNGE FULANI: CCM.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Kulia kwako.
SPIKA: Ahsante, Mheshimiwa Mabula....
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, kwa heshima zote kabisa mdogo wangu katika hili Bunge, hajitambui. Ikumbukwe CCM ikichukua takwimu za Urais wanapataje, imeanzia 81% imeshuka mpaka Mheshimiwa Magufuli amepata 58%, tena questionable! Questionable! (Kicheko/Makofi)
Kingine, huyo huyo wakati Uenyekiti unabadilishwa badilishwa, wakati Mheshimiwa Mnyika anasema kwamba ule uongozi wa Mheshimiwa wa Kikwete ni dhaifu, ninyi mlisimama na kusema na kufedhehesha kila kitu! Leo yaani mnajikosoa ndani yenu wenyewe. Tunafurahi sana na wananchi wanawaona na wanasikia kwamba hamfai! Niendelee! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kwenye nishati ambacho ni kichochezi kwenye viwanda. Mpango uliopita, yaani mlikuwa mmedhamiria mnaleta Megawatt 2,780, lakini mpaka tunavyoongea miaka mitano ni Megawatt 496 tu. Hivi viwanda tunavyoongea tunaenda kuvipataje, kama nishati yenyewe bado ni goigoi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo kule kwetu Tarime ni wakulima na wafugaji. Tunahitaji hata viwanda, tuwe na umeme. Kwa mwendo huu, tutafikaje? Halafu tukiishauri Serikali hapa kwamba tuwe na vitu ambayo tukiviongea vina tija, watu wanaweka… nyie Wabunge, mmekuja kama Wabunge, wajibikeni kama Wabunge, acha Mawaziri watende. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yaani kiuhalisia nikipitia sekta zote, kwenye elimu ndiyo kabisa! Siku ile Mheshimiwa Rais alisema hapa kwamba viwanda ambavyo anadhamiria na ambavyo vitaajiri Watanzania, vitatumia nguvu kazi zaidi kuliko teknolojia ya kisasa. Kwenye Mpango, matarajio yetu kwenye VETA tu hayajafikiwa kwa kiwango kikubwa sana. Sasa leo tuseme tuna Mpango mkakati upi ili uweze kutuaminisha kwamba hii dhamira ya dhati tuliyonayo tutafikia? Mimi mwenyewe natamani sana Tanzania tuweze kukua kiuchumi, wananchi wengi hawana ajira. Tuna rasilimali nyingi, lakini zilikuwa zinakumbatiwa tu na wachache huko, zinatumika vibaya.
Mheshimiwa Spika, sasa kama kweli hiyo awamu ya tano ina dhamira ya dhati na kwa sababu bajeti hii tunaenda kuongea mambo mengi Wizara mbalimbali, tutaenda kuipima kama ina dhamira ya dhati. Kweli kama ina dhamira ya dhati ya kuwasadia Watanzania, Mheshimiwa Waziri tunaomba hayo uliyoyaandika utuainishie kwamba tunamaanisha. Asilimia 40 zinaenda kwenye maendeleo, tumejizatiti vipi kwenye kodi?
Mheshimiwa Spika, mwaka 2015 wakati nachangia bajeti hapa nilimweleza mfano tu, Mama Sada. Nenda hapa kwenye supermarket moja Dodoma, umenunua vitu, hakupi ile risiti ya TRA, akaenda, akafuatilia akapata.
Mheshimiwa Spika, hawa Usalama wa Taifa, leo ukinunua vitu hawakupi risiti za TRA. Juzi tu nimenunua kitu Kariakoo Sh. 620,000/= nikawaambia wanipe risiti ya TRA, ooh, risiti ya TRA tukikupa inaenda zaidi ya hapo. Sasa si hii ndiyo bei umeweka kwenye duka lako? Ndiyo! Unajua aliniambia basi naomba nikupe sh. 100,000/= halafu sh. 520,000/= nikuandikie ya kawaida.
Mheshimiwa Spika, Usalama wa Taifa, ninyi kama Wizara mnadhibiti vipi hilo? Tunapoteza mapato mengi sana. Hii mnayosema sijui risiti za electronic, hazifanyi kazi, wanaziweka kando. Mtanzania akienda, anamwambia nitakupa hiki, fanya punguza, shell, yaani kote tunapoteza mapato and then mnakuja tu mme-document ma-paper; tupe sign mnakusanya vipi kodi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haitoshi tu Mheshimiwa Rais kusimama kwenye TV, Tanzania lipa kodi. Mmeweka mechanism gani kuendeleza hii ya Mheshimiwa Rais anayosema kila siku kwenye TV kwamba kodi itakusanywa kweli? Wekeni watu waende kwenye maduka! Ajidai kama ananunua kifaa, aone kama atapewa hiyo risiti au atapewa lugha gani? Kamata, fanya vyote nchi nzima, watu walipe kodi, siyo kuwanyanyasa watu wadogo wadogo, wajasiriamali wenye vimbogamboga, wenye miradi midogo midogo ndio wanaoleta fedha kwa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilisema mwaka 2015 kwamba, worthiness ya mtu i-reflect ulipaji wa kodi yake. Sijui hata wamefanya nini? Mnatangaza watu wawe na TIN, sijui kila mtu awe na TIN: Je, kweli kila Mtanzania ana-TIN? Mimi kwa mfano, Esther Matiko, worthiness yangu ina-reflect nalipa kodi vipi? Do you trace that? Kama hamtaweza kukusanya mapato ya ndani na wafadhili wenyewe ndiyo hivyo, hii mipango, miaka mitano tunakuja hapa, patupu! Tena leo bora tunaambiwa zimepikwapikwa ziko asilimia 60. Tukija mwaka 2019 hapa tunaelekea 2020 tutaambiwa story zile zile.
Mheshimiwa Spika, nimalizie. Tuwe na nishati, tuboreshe miundombinu ya barabara kama mnataka hivi viwanda kuanzia kule kwa mkulima, barabara zipitike. Tuboreshe reli.
Mheshimiwa Spika, ukija kwenye Air Tanzania, aibu! National Carrier, aibu! Ukisafiri, ukaenda na hizi ndege, ukifika Nairobi, wanashuka watalii wote mnakuja Tanzania wachache. Wakishafika pale, ina maana zile hoteli za Kenya ndio wanafaidika. Wanaletwa na magari kuja kwenye mbuga zetu za Tanzania. Hata juzi niliona wanasema, hata daraja la Kigamboni ambalo mmelizindua jana, watasema liko Kenya. Mlima Kilimanjaro Kenya, mengine yote Kenya. We are not branding our Nation. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Samatta ni mchezaji sijui wa wapi huko, what are we doing? Tuwe serious! Tutafute vyanzo ambavyo vinatuletea mapato. Sekta ya Utalii, let„s have our National Career. Hatuna National Career! Ni wafanyakazi tu wamebaki na jengo pale city center tena ambalo lipo kwenye prime area, mliendeleze basi! Tunabaki tu na vijistori, tutaleta, tutaleta. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa Jimbo langu la Tarime. Kwanza kabisa, naomba kabisa kipekee nimshukuru Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Najua kama wanavyojinafasi humu ndani, mkijivua kweli, ile ambayo tumekuwa tukiwashauri miaka yote, mnasema kelele za chura hazimnini sijui nini; sasa kweli mkiamua kufanya hivyo, siyo kama maigizo kwa sababu mnaona Mheshimiwa Magufuli anavyofanya, mtafika mbali.
Mheshimiwa Spika, ndugu yangu pale huwa anavaa zile scarf za Kitanzania na nini, kweli yule ni mzalendo sana. Amekuja Tarime, ameongea mambo mengi sana na Wanatarime.
Kama kweli hiyo dhamira itaenda kutendeka kama ni ya Serikali hii, rasilimali tulizonazo zikageuzwa kuwasaidia Watanzania, maana yake tumekuwa tukiongea, pale kuna Soko la Kimataifa, tumekuwa tukipiga kelele humu mimi na Mheshimiwa Nyambari, limechukua miaka mingi kumalizika, liko Lemagu; lile soko lingemalizika, ingekuwa ni kipato kikubwa sana kwa nchi yetu. Liko border pale! Mnachukua muda mwingi sana kumaliza lile soko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wenzetu Kenya wanachukua hiyo opportunity, ukienda upande wa pili wa Kenya ni tofauti kabisa na Tanzania. Lile soko likikamilika, ule mnada ukafunguliwa, kipato ndani ya Mji wa Tarime, kipato ndani ya Wilaya ya Tarime kitaongezeka na Taifa linaenda kupata fedha ambazo leo zitatumika kusaidia hayo madawati na kujenga Maboma. Maana yake mmesema elimu bure, kule kwetu hakuna vipato. Havipo Tarime Mjini! Sasa mnahangaisha watu kujikusanya maskini wale wajenge viboma; watoto wanasoma 200 kwenye darasa moja. tupeni lile soko lifunguliwe, mnada ufunguliwe, kipato kiongezeke.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kipekee kabisa namshukuru ndugu yangu, kaka yangu pale, naomba na Mawaziri wengine, mmepewa ridhaa na Watanzania, mnatumikia nchi. Maana kuna mwingine nilisikia ooh, pale sijui CHADEMA, sijui CUF hatupeleki maendeleo. What?
Mheshimiwa Spika, hizi rasilimali ni za kwetu wote. Wale Watanzania wote wametuweka wote madarakani. Ninyi mmepewa ridhaa ya nchi, kuna wengine wamepewa ridhaa za Majimbo na Halmashauri. Tunatakiwa tuwatumikie wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nafikiri ushauri wangu mkiuzingatia, vichochezi vya kuanzisha viwanda, viwepo; nishati, miundombinu ya barabara na kilimo mkiboreshe, Sekta ya Elimu ili tuweze kupata hao watu ambao tunasema tunaenda kuwatumia, reli na usafiri wa anga. Ndoto ya Waziri wa Fedha na hii Mipango mnayotuletea, itatimia. Kinyume cha hapo, tutakuwa tunacheza vidogoli tu siku zote. Ahsante sana.