Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru ingawa muda ni mchache niseme mawili tu ya haraka haraka.
Kwanza, Waheshimiwa Wabunge leo tuna taarifa hizi kumi na zote hizi zinazungumzia mapendekezo ya Bunge hili. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri ni vyema ungetuongoza kwamba kama walivyosema wenzetu kwenye Kamati ya Uwekezaji ukurasa wa 49 kwamba ni vyema maazimio haya, mengine ni mazito sana, kwa mfano mambo yaliyozungumzwa kuhusu Bandari ya Dar es Salaam kama ni ya kweli basi yataisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio hiyo tu wewe mwenyewe kwa sababu ni mahiri kuongoza Bunge hili ningeomba sana haya yote maazimio Waheshimiwa Wabunge tukubaliane yasiachiwe kwa Katibu wa Bunge; sisi wenyewe Wabunge tuunde Kamati yetu ndogo ya kuratibu mambo haya ni mambo mazito sana, vinginevyo yatakuwa hayana maana haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukumbushane kidogo, Mabunge mengine yanafanya hivyo kwamba kazi hii tunayoifanya ni kazi muhimu ya Kikatiba; ni kazi yetu kabisa ya msingi ya kuishauri Serikali na kuisimamia, lazima mambo ya msingi yalimo humu pengine si yote, lakini yale ya msingi lazima yadadavuliwe, yaandikwe vizuri na Serikali tuitake ije na majibu na kalenda yake ya utekelezaji, vinginevyo itakuwa ni hadithi tu, mambo ni mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yamezungumzwa humo ndani, ushauri wangu nakubaliana na wenzetu wa Kamati ya Uwekezaji kama walivyoainisha kwamba tuunde Kamati Ndogo na wewe Mheshimiwa Chenge utuongoze tuunde Kamati Ndogo itakayosimamia mambo haya kwa kuwa ni mambo makubwa na mazito sana ambayo haiwezi kuachiwa Ofisi ya Katibu peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa niliseme kwa muda uliobaki kidogo huu nizungumzie suala la PPP. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda anahangaika sana, hongera. Kaza buti, lazima ufanye promotion na lazima uendelee kufanya promotion.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ushauri wangu ni kwamba, ili upate pesa lazima utumie pesa; waswahili wanasema ili ule lazima uliwe, ndiyo maana yake. (Kicheko)
Kwa hiyo, nilikuwa naomba hii private sekta tuisaidie, yenyewe haiwezi kunyanyuka; private sector duniani kote inasaidiwa kukua ili hatimaye iweze kuzalisha wafanyabiashara na walipe kodi na hatimaye kodi hiyo ndio inakuja kusaidia Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa mambo mengine yanatisha ukiyasoma humu ndani, kwa mfano kama kesi imeamuliwa ni kwa nini wenzetu wa Maliasili hawatekelezi haya yaliyoamuliwa na Mahakama? Kwa nini Serikali hamfanyi? Tunapotaze shilingi bilioni 10 wakati kesi imeamuliwa na Serikali imeshinda? Hakafu wakati huo tunaambiwa fedha hazipo, fedha si ndizo hizi? Ten billion mnai-surrender namna gani wakati kuna court ruling? Wale matajiri kama hawataki kakamateni mali zao tupate ten billion yetu. Sasa mengine humu ndani yanazungumzwa kwa kweli yanatia uchungu sana. Tunatafuta fedha tuna shida ya fedha ya miradi ya maendeleo fedha zingine zimeachiwa kwa matajiri na sababu iliyotolewa humu kwamba eti hakuna Bodi ya Tanzania National Parks, alah! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi bodi hiyo iundwe haraka sana na ndio mambo ambayo sisi kama Bunge lazima tusimame kidete na tuitake Serikali iunde hiyo bodi tuokoe ten billion yetu na hilo linakuwa halina mjadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala mwisho ni la kilimo. Mimi tafsiri yangu ya viwanda ni viwanda vya kilimo, vya mifugo na vya sekta ya uvuvi. Hivi viwanda vya Wachina Waturuki, Waingereza na wengine wanakuja kutusaidia tu lakini the basic industry ni lazima itokane na kilimo chetu, kilimo, wafugaji na wavuvi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako nizungumzie habari ya wawekezaji; ndugu Mwijage tembea na wawekezaji mfukoni kama wapo walete kwetu tutawapa maeneo ya kufanya shughuli zao.