Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mi nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia mjadala huu uliopo mbele yetu. Nami nianze katika maeneo machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza tunazungumza habari ya mipango ya nchi yetu kwa miaka mitano na kama tunazungumza mipango tujue pia madhara ya mipango ambayo iliwahi kujadiliwa hapa Bungeni kwa waliokuwepo na haikufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakumbuka kwamba miaka minne iliyopita nchi yetu ilijadili habari ya Sheria ya Manunuzi hapa katika Bunge na ikaleta mvutano mkubwa sana. Leo tunasema sheria hiyo ni mbovu kuliko sheria zilizowahi kutokea kwenye nchi yetu na kila mtu analalamika. Kwa hiyo, tunapojadili suala hili ni vizuri tukaweka maslahi ya Taifa letu mbele tukajadili na mkapokea ushauri kwa ajili ya kujenga uchumi wa Taifa letu. Sheria mbovu hizi ambazo ziko kwenye Taifa letu ni majanga kwetu sisi wote. Kwa hiyo ni vizuri mkapokea ushauri na mkaufanyia kazi kuliko kutazama tu imetolewa na watu gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nitaanza na elimu. Leo tunazungumza kwamba tunaenda kutoa bei elekezi ya ada za shule katika shule za binafsi na hii ni kwa sababu ya fear, hii ni kwa sababu ya hofu ya miundombinu mibovu na taaluma yetu katika nchi yetu. Kwa hiyo, kwa sababu tumeona shule za Serikali zinafanya vibaya tunawalazimisha wawekezaji wengine nao wa subsidize ada zao ili wafanye vibaya tuweze kujishindanisha nao, ni vizuri Serikali ikaiga na kufanya competition kwa kufanya mambo yafuatayo katika elimu kwa miaka mitano:
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kuboresha miundombinu na maslahi ya Walimu. Bahati nzuri tunaambiwa Rais alikuwa Mwalimu, Waziri Mkuu alikuwa Mwalimu, Mheshimiwa Profesa Ndalichako alikuwa naye ni Mwalimu na asilimia kubwa ya Wabunge hapa ni Walimu. Leo unazungumza habari ya Mwalimu anayetembea kilomita mbili, tatu kwenda na kurudi kila siku shuleni, hana nyumba anategemea mshahara wake alipe nauli, anategemea mshahara wake alipe nyumba ya kupanga kule shuleni, halafu akafanye vizuri, hawezi kufanya vizuri! Kama tumeshindwa kujenga nyumba za Walimu tuwape Walimu fedha kwa ajili ya kupanga maeneo ya kuishi, tunawalipa shilingi ngapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni madarasa na nyumba za watumishi hakuna katika shule nyingi za vijijini, mnategemea huyo mwanafunzi atafaulu kwa namna gani? Kwa hiyo, ni vizuri tukawa na mipango inayolenga kuboresha elimu yetu tukajishindanisha na shule za private kuliko kuwaambia shule za private washushe ada ili nao wafanye vibaya tuweze kujiona kwamba wote ni kundi la wajinga, haiwezekani! Ni wajibu wa Serikali kutoa elimu kwa wananchi wake, wahisani hawa wanatusaidia tusiwa-discourage kwa kuwalazimisha kufanya jambo ambalo hawawezi kufanya kwa ajili ya kuendeleza elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine ni suala la mifugo, simwoni Mheshimiwa Waziri lakini nilitamani awepo, kwa sababu sisi ni wafugaji na sehemu kubwa ya Watanzania ukiwaacha wakulima ni wafugaji. Ukienda Mji wa Kajiado, Kenya asilimia 80 ya mapato yao yanatokana na mifugo na mifugo hiyo inatoka Tanzania, inatoka Shinyanga inakuja Arusha inasafirishwa inaenda Namanga inaenda Kenya. Kwa nini sisi tunashindwa kujenga viwanda kwa ajili ya ku-accommodate bidhaa zinazotokana na mifugo? Tunategemea kujenga uchumi wa viwanda kwa kutegemea wafadhili, lakini hatutaki kujenga viwanda vinavyo-accommodate bidhaa zinazozalishwa na wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo maziwa, nyama, na ngozi, lakini hatuna viwanda vya namna hiyo. Nawaambia mwaka 2020 tutakuja kuzungumza habari ya utekelezaji wa mipango hii kwa asilimia 10 au asilimia 15 kama hatutakubaliana kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na wananchi wetu zinajengewa mazingira ya kupata soko la uhakika ili waweze kuzalisha zaidi. Kwa hiyo, tutashauri kuwepo na viwanda vya bidhaa zinazotokana na mifugo, ngozi, nyama na maziwa maeneo ya shinyanga, Arusha ili kudhibiti upelekaji wa mifugo yetu nchini Kenya na kwenda kuwanufaisha watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji ule unaishi kwa ushuru tu wa mifugo, lakini sisi hata soko tu la kuuza mifugo hatuna, hata kiwanda cha maziwa hatuna, halafu tunazungumza nchi ya viwanda!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuwe na viwanda vilevile ni lazima tuwe na miundombinu, ardhi tumetengeneza mazingira gani kwa ajili ya kufanya uwekezaji. Kwa hiyo, tunaposema mnapiga kelele hamna mipango mnatu-challenge lakini ukweli ndiyo huo! Huu siyo Mpango wa kwanza kuletwa na Serikali, umeshaletwa miaka mitano, lakini leo tukiwauliza mmetekeleza mipango ile kwa asilimia ngapi hakuna! Sasa tukisema hata huu hamtekelezi mnasema tunawapinga, tunataka mtu-prove kwamba tunawapinga bure kwa kufanya utekelezaji wa mipango hii mliyoleta kwa asilimia angalau themanini, kitu ambacho hakiwezekani, hamuwezi kufanya kwa sababu mnapenda kuandika lakini hamtaki kuweka mipango ya kupata fedha ya kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni muhimu katika suala la viwanda, leo tunazungumza habari ya viwanda, lakini hatusemi kwa nini viwanda vilikufa, hatusemi kwa nini tulikwama na tumeweka mechanism gani ya kuendelea hapa. Sisi wenyewe ni mashahidi, katika watu wanaouwa viwanda nchi hii ni Serikali kwa kuwa-discourage wawekezaji wa ndani na kuwakumbatia wawekezaji wa nje. Maeneo mengi watu wanalalamika, mkulima anazalisha alizeti, unaweka kodi kwenye uzalishaji wa mafuta, lakini mafuta yanayotoka nje yanaingia na zero, halafu mnategemea mtu alime alizeti, mtu atengeneze kiwanda cha alizeti kama anaweza kuagiza mafuta nje bila kodi, halafu tunasema tunazalisha! Hatuwezi kuwa na viwanda vya namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya leo tunazungumza wao wameweka asilimia arobaini ya manunuzi yao yote lazima yafanyike na local contractor ndani ya nchi yao, sisi tunasema bilioni mbili tu international competition. Hatuwezi kujenga nchi kama hatuwa-encourage wawekezaji wa ndani kufaidi uchumi wa nchi yao. Ndiyo maana leo tunawaambia Kiwanda cha Urafiki kinakufa kwa sababu asilimia hamsini na moja ni ya China, asilimia arobaini na tisa ni Serikali na Wachina wanataka kubadilisha kile kiwanda cha Urafiki iwe ni sehemu yao ya kuingiza bidhaa kutoka China na kufanya dumping katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali iangalie kiwanda cha Urafiki. Mheshimiwa Waziri tulikuambia kwenye Kamati na narudia kusema kwa kweli tunaomba Wabunge tuisimamie Serikali kwa sababu kuna hujuma na kuna ufisadi mkubwa katika Kiwanda cha Urafiki, kwa sababu Wachina wamepewa asilimia hamsini na moja, Serikali inashindwa kununua asilimia tatu tu, ili iwe na say katika kiwanda cha Urafiki. Hatuwezi kuendesha nchi yetu kama viwanda tulivyonavyo sisi tunaviua wenyewe kwa sababu tunaogopa kuwashughulikia watu waliotufikisha hapa, haiwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge katika hili tukubaliane katika mambo ya msingi kwa ajili ya Taifa letu, acheni ushabiki wa kivyama, kila mtu ameletwa hapa kwa maslahi ya wananchi wake na tuna wajibu wa kujibu tulichokifanya tukiwa huku Bungeni, hii ni nchi yetu sote yakiwa mazuri ni ya kwetu, yakiwa mabaya ni yetu sisi sote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine katika hilo suala la kiwanda cha Urafiki; tumeenda kiwanda ni kichafu, China wanasema wanataka kukifanya soko walete vitu vyao hapa wamalize wao, sisi tubaki kama watazamaji na bidhaa feki, ndiyo maana leo zimeingizwa simu chafu na simu feki nchini. Badala ya kuzungumza ni Sheria gani inaruhusu kuingiza tunazungumza kwenda kuwanyang‟anya Watanzania zile simu! Tudhibiti kwanza uingizwaji wa bidhaa feki, lakini siyo kuja kumuumiza mwananchi ambaye uliingiza bidhaa halafu yeye amenunua unamhukumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho ambalo nataka kusema katika hili, ni suala la Wanyamapori, kwa sababu tunazungumza habari ya utalii, lakini hatuzungumzi habari ya mwananchi anayekaa na wale wanyama anafaidi nini katika rasilimali ya Taifa lake. Leo wanyama wanavamia mashamba, leo wanyama wanavamia watu, hivyo wananchi hawaoni faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri katika hili na katika Bajeti yake, kwa kweli tuoneshe mazingira ya kwamba, wananchi wale wanaokaa karibu na Hifadhi za Taifa wananufaika zaidi katika mapato yanayopatikana ili wao wenyewe washiriki kulinda rasilimali za wanyama wale waliopo kwa ajili ya maslahi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wananchi wenyewe hawaoni faida ya wale wanyama wanaona kama ni kero, kwa kweli tutaendelea kupata shida na Hifadhi zetu hazitakuwa na tija kwa sababu wananchi wenyewe hawaoni manufaa ya yale maeneo ambayo wao yanawazunguka kwa ajili ya mapato ya maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la mwisho ni viwanda. Tumezungumza habari ya viwanda vyetu nini kiliviua. Mfano, tulikuwa na Kiwanda cha Nyama Simanjiro, lakini siasa iliua kile kiwanda, watu mia sita wakaacha kazi kwa sababu siasa ziliingia, kiwanda kikaonekana mtu ana interest zake za kisiasa ikaua. Kama hatutadhibiti mwingiliano wa siasa na rasilimali za Taifa letu kwa kweli hatuwezi kusonga mbele na siyo mashindano ya kutumbua majipu iwe ni mashindano ya kuwaelekeza wananchi wetu waende katika maslahi na haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mtu anataka kumfukuza mtu kazi, tunatengeneza Taifa la waoga ambao watumishi wetu hawatafanya kazi kwa uhuru na ndiyo tunawategemea kuzalisha katika nchi yetu. Wabadhilifu washughulikiwe lakini tusishindane kufukuza watu kazi, tushindane kuwaelimisha watu wetu, tusiwaoneshe dunia kwamba Watumishi wa Umma na Wataalam wote ni wezi. Tukijenga sura ya Taifa letu hivyo, tutaonekana watu wote ni wendawazimu. Haiwezekani siyo kila Mtumishi wa Umma ni mwizi kwenye nchi yetu, siyo kweli!
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kila mtu anafukuza wengine wanafunga kiwanda huku, mwingine wanafunga geti huku, mwingine anafanya hivi huku, what kind of that nchi? Utawala wa Sheria uko wapi katika hilo? Tunatamani nchi yetu watumishi wapewe nafasi ya kufanya kazi na kuonesha matumizi ya taaluma zao walizosomea ili nchi yetu isonge mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna Mbunge aliyeiandika hii bajeti, wameandika wataalam, sasa kama tunawa-discourage Mawaziri wanasema tunarekodiwa, wanaogopa kusema hii bajeti haitoshi nchi haiwezi kusogea. Kwa mfano ameonesha mtu mmoja, Waziri wa Ardhi ameonesha kuthubutu na nampongeza na nitaendelea kumpongeza kwa kazi nzuri anayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na watu wachache wanaothubutu kuwasaidia Watanzania kwa sura hiyo tutaacha alama ya utumishi kwenye Taifa letu. Kwa nini leo tuzungumze habari ya maadhimisho ya Sokoine, habari ya Nyerere kwa nini sisi tusiache legacy kwenye Taifa letu, tukaacha siasa tukaenda kwenye mipango inayotekelezeka kwa ajili ya kuisaidia nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatutajenga utaratibu huo wa kupokea ushauri wa kitaalam kwa ajili ya maslahi ya Taifa letu tutaendelea kusema haya na nawaambia hamtatekeleza kama hamtaweka priority ya vipaumbele vichache na kutoa vikwazo vilivyoua viwanda vyetu na kuwapa wataalam nafasi ya kutumikia Taifa lao, kuliko kufanya kila jambo siasa. Kama kuna mambo ambayo Rais anasema yanawezekana na hayawezekani tumwambie hayawezekani professionally, hili haliwezekani! Twende kwenye yale mambo ya msingi ambayo hata taaluma inaruhusu kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kusema tunajenga reli, tunasema tunajenga viwanda, tunatoa elimu bure kwa wakati mmoja kwa uchumi wa nchi yetu ambayo tunasema tunakusanya trilioni moja kwa mwezi, mara miezi kumi na mbili, trilioni kumi na mbili, lakini tunataka tujenge reli ya trilioni 300 na kutoa elimu kwa trilioni tano mpaka sita, hiyo hela itatoka wapi? it is impossible tuwe na priority ambazo tunatekeleza, tukasema jamani we have done this, kuliko kuwa na vipaumbele mia mbili halafu Wabunge hapa tunapiga makofi. Tunawaambia Serikali tengeni vipaumbele vichache ambavyo vinatekelezeka kwa ajili ya maslahi ya Taifa letu.