Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Kwanza nianze kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu mizuri ambapo kila Mbunge aliposimama amezungumzia angalau tatizo alilonalo kwenye eneo lake kuhusu upatikanaji wa maji. Kumekuwa na mabishano kuhusu asilimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba tutaendelea kuyapeleka maji, kwa maana kwamba kutokana na ilani ya Chama cha Mapinduzi, tumesema vjijini tutapeleka kwa 85% ifikapo mwaka 2020 na mijini tutapeleka kwa 95%. Tunafanya hivi kwa kufuata programu ya maji ambayo tulianza nayo mwaka 2007. Kuna miradi ambayo tulianza kuitekeleza, kwanza tutakamilisha miradi ambayo haijakamilika, halafu tutaingia awamu ya pili ambayo tumeanza sasa hivi, kuweza kuainisha ni miradi ipi na maeneo yapi tunakwenda kufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge watakaporudi kwenye Majimbo yao, kwenye Halmashauri zao wakaangalie vipaumbele ambavyo wangetaka tuanze navyo. Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni ameelekeza maeneo 65 nchi nzima ndiyo kipaumbele na sisi katika kufanya kazi tutafuata hilo. Sasa ninyi Waheshimiwa Wabunge mtusaidie ni wapi ungetaka tuanze napo, kwa maana kwamba tuweze kufikisha hizi asilimia tunazosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa, mwaka 2025, lengo la Serikali ni kwamba tutapeleka maji kwa kiwango cha 100% vijijini na mijini. Changamoto tunayoipata katika maeneo ya mijini sasa ukishaongeza upatikanaji wa maji unaongeza pia maji taka. Sasa tunataka katika hii phase ya pili, tuingie katika namna ya kuweza kuongeza jinsi tutakavyoondoa maji taka katika miji yetu ili pia tuweze kuondoa changamoto za maradhi kama kipindupindu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jambo hilo tutaliweka kwenye Mpango ambao Mheshimiwa Waziri wa Fedha ametoa mwelekeo na sasa kila sekta tutakwenda kuangalia ni miradi ipi kulingana na ceiling ya bajeti. Pia nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, tulishaweka Mfuko wa Maji toka mwaka jana na Mfuko wa Maji huu kutokana na tozo ya mafuta ambayo tuna uhakika, zile shilingi 50 kwa kila lita tutapata kama shilingi bilioni 90 mpaka ikifika Juni. Fedha hizi zitasaidia kulipa wakandarasi ambao sehemu kubwa wamesimama na fedha hiyo imeanza kutoka na tayari tumeanza kupeleka kwenye Halmashauri.
Naomba sana Wakurugenzi wetu fedha zile ambazo tunapeleka specifically kwa mradi, walipe miradi ile ambayo tumeamua kuimaliza kwanza. Miradi mingi ipo kwenye 90% na 95%. Tukiweza kuwalipa tuna uhakika wananchi wetu wataanza kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana fedha hizi zisiende kufanya kazi nyingine, tutakuwa wakali na tutachukua hatua kwa Mkurugenzi ambaye ataamua kuzitumia fedha hizi anavyotaka yeye. Fedha hizo ni moto, kwa hiyo, tumepeleka tuhakikishe kabisa wanakwenda kulipa Wakandarasi wamalize miradi ili wananchi wetu waanze kupata maji. (Makofi)
Kwa upande wa Da es Salaam naomba niseme tu kwamba ikifika mwezi Machi, tutakuwa tumepata maji yanayotosha mahitaji, kwa maana ya kiujumla wake ya wananchi. Kazi kubwa ambayo tutakuwa tunakwenda kufanya sasa ni ule usambazaji. Kule Kimbiji na Mpera tumeshachimba visima tayari saba kati ya visima 12 kwa ajili ya maeneo mengine ya Kigamboni, Mkuranga ili tuweze kukamilisha na kuhakikisha wananchi wa maeneo yale wanapata maji. Kwa hiyo, naomba sana ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tutachukua haya mawazo yenu yote na tutayaweka kwenye Mpango ili tuhakikishe kwamba tunakwenda kutekeleza kama tulivyopanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wananchi wengi ambao wanaishi kandokando ya Ziwa Victoria nimetoa ahadi na Rais ameahidi kwamba tutachukua maji ya Ziwa Victoria kuweza kusambaza katika miji yote mikuu ya mikoa inayozunguka Ziwa Victoria pamoja na Makao Makuu ya Wilaya. Hii miradi tumeshaanza, mingine kwa kutumia wafadhili mbalimbali, lakini mengine tutakwenda kufanya kwa kutumia fedha zetu za ndani. Sasa tutakapofika kwenye bajeti, basi Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono ili tuweze kutekeleza miradi kama ilivyokuwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Nashukuru kwa nafasi, ahsante sana.