Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kutoa shukrani kwako kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu naomba nijielekeze katika maeneo makubwa matatu. Eneo la kwanza ambalo ningependa kuligusia kwa umuhimu wake ambalo hili linaunganisha maeneo yote ni eneo la elimu. Nimepitia vizuri mpango, naomba nitoe pongezi kwa yale ambayo tayari yameshafanyika ndani ya kipindi hiki lakini bado kuna maeneo ambayo nilifikiri kuna umuhimu wa kuelekeza nguvu na kuona namna gani tunaweza kuweka maboresho zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni uboreshaji wa miundombinu. Tayari tumeona utekelezaji wa upatikanaji wa elimu bure katika shule zetu za msingi pamoja na sekondari, lakini bado kuna tatizo kubwa za vyumba vya madarasa katika shule zetu lakini pia kumekuwa na matatizo makubwa katika upatikanaji wa nyumba za Walimu. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika mpango huu ambao tunaujadili sasa eneo hili ni lazima lioneshwe wazi ni kwa kiasi gani tunakwenda kuboresha miundombinu hii ili kuunga mkono kile ambacho tayari kimeshafanyika katika eneo hili la kutoa elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sera yetu ya kuboresha viwanda wataalam watapatikana kupitia elimu, lakini bado kuna umuhimu wa kuangalia namna gani tutahusianisha maendeleo yetu pamoja na elimu ambayo tunaitoa kwa vijana wetu katika shule zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nilizungumzie upande wa elimu ni suala zima la mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Kumekuwa na mkanganyiko mkubwa ambapo sisi kama Wabunge lazima tuishauri vizuri Serikali yetu ili iweze kuendelea kutoa mikopo kwa vigezo vile ambavyo vilishakuwa vinatumika. Yako marekebisho, upo upungufu tulishazungumza hapa mwaka jana lakini kuna umuhimu sasa wa hiki ambacho kinafanyika sasa hivi kuangaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Serikali kwa ujumla lazima ifanye jitihada za makusudi kuingilia kati ili kuhakikisha watoto wa wakulima ambao leo hii wanafukuzwa vyuoni bila sababu za msingi wanapata mikopo ili waweze kupata elimu, ambapo hawa ndiyo tutakwenda kuwatumia baadaye katika viwanda ambavyo tunasema tunataka kwenda kuviboresha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili naomba pia nimshauri Mheshimiwa Waziri, hebu wachukue jitihada za makusudi kuiangalia Bodi ya Mikopo. Sasa hivi wamekuja na vigezo ambavyo vitakwenda kuwabana watoto wetu kwa kiasi kikubwa sana. Wametengeneza fomu ambazo kimsingi ukiangalia kwa undani vigezo ambavyo wanakwenda kuviweka bado haviendi kumsaidia mtoto wa mkulima ambaye kwa kweli sehemu pekee ya kukimbilia ni katika Serikali ili waweze kupata mikopo ambayo itaenda kusaidia kuzalisha wasomi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nataka nichangie ni la kilimo. Naomba niungane au nitoe salamu kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Nachingwea na Kusini kwa ujumla. Kwa muda mrefu tulikuwa tunajadili kero ambazo tumekuwanazo kwenye zao la korosho sasa hivi korosho imekuwa na uchumi mkubwa sana. Serikali imeondoa tozo tano ambazo sisi tulizijadili hapa katika mpango huu mwaka jana. Katika hili Mheshimiwa Waziri naomba tuwapongeze sana kwa kusikiliza kilio chetu, tumeweza kuondoa kodi. Leo hii tunavyozungumza mkulima anapima korosho yake kilo moja shilingi elfu tatu mpaka elfu tatu na mia nane, hili ni jambo zito, ni jambo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wito wangu naomba tuharakishe katika suala zima la malipo kwa wakulima wetu mara baada ya kuwa minada imeshafanyika. Leo hii nazungumza kwenye Wilaya yangu ni zaidi ya siku nane mnada umeshafanyika bado wakulima wanaendelea kupata shida malipo yao hawajapata. Hii itaenda kusababisha chomachoma kuendelea kuwadhulumu wakulima kitu ambacho Serikali tayari ilishapiga hatua katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nilizungumzie katika eneo hili la korosho au katika eneo la kilimo ni suala zima linalohusiana na utendaji wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Serikali inapoteza mapato mengi sana katika eneo hili. Ukiondoa korosho ambayo leo kwetu imekuwa ni uchumi mkubwa bado tuna mazao kama ya ufuta, mbaazi ambayo mwaka jana na mwaka huu tumeuza kwa bei ya chini sana na hii ni kwa sababu Bodi ya Mazao Mchanganyiko haifanyi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapoteza kodi hapa, Halmashauri zetu zinapoteza kodi, lakini wakulima wetu pia wanapoteza fedha nyingi ambayo tulifikiri ingeweza kuwasaidia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri anapokwenda kujumuisha, anapokwenda kushauriana na wenziwe tunaomba katika eneo hili tusaidiane na watu wa Wizara ya Kilimo ili tuhakikishe Bodi ya Mazao Mchanganyiko inafanya kazi ili tuweze kukusanya kodi zaidi ambayo itasaidia katika eneo hili la kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nilizungumzie ni suala zima la upatikanaji wa pembejeo. Pembejeo bado hazipatikani kwa wakati. Hapa tunavyozungumza sasa hivi msimu wa kilimo umeanza lakini mpaka sasa hivi bado pembejeo kwa wakulima wetu hazina uelekeo mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri, hatuwezi kujadili kuwa na viwanda kama hatuwezi kujadili namna ya kuwa na kilimo bora. Kilimo bora tutakipata kwa kuwapelekea wakulima pembejeo kwa wakati na vitendea kazi vingine ambavyo vitawasaidia. Kwa hiyo, nafikiri ni muhimu tuishauri Serikali ili iweze kuboresha katika eneo hili ambalo kimsingi litakwenda kuwasaidia wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine katika kilimo ni suala zima la kufufua na kuchukua viwanda ambavyo tayari vilishachukuliwa na wawekezaji. Ndani ya Wilaya yangu ya Nachingwea tuna viwanda viwili, kimoja cha korosho lakini tunacho kiwanda kimoja cha kukamua mafuta. Naomba nimshukuru kwa upekee Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya ziara katika haya maeneo, Serikali haina sababu ya kupoteza muda ichukue hivi viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yale majengo sasa hivi yanatumika kwa matumizi ambayo hayakukusudiwa, vipuri vinaendelea kung’olewa katika vile viwanda. Leo hii tunahitaji kuwa na processing industries kwa hizi korosho tunazozalisha. Tungefurahi kuona Serikali yetu kwa hii sera ya kuwa na viwanda inaenda kuchukua hivi viwanda ili tuweze sisi wenyewe kuandaa korosho zetu, ufuta wetu kwa bei nafuu ambayo tunafikiri itakwenda kuleta tija kwa mkulima badala ya sasa hivi kuuza korosho na ufuta kwenda nje ya mipaka yetu kufanyiwa processing.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nilizungumzie ni suala zima linalohusu nishati. Hatuwezi kuwa na viwanda, hatuwezi kufanya lolote kama nishati ya umeme bado ni tatizo. Mikoa yetu mingi bado umeme wa uhakika hatuna. Kwa hiyo, naomba Waziri atakapokwenda kuhitimisha na kupitia mpango wake lazima aseme tatizo la umeme katika Majimbo yetu na Wilaya zetu linakwenda kupatiwa ufumbuzi kwa namna gani? Hili ni lazima lionekane katika mpango badala ya kuwa katika ujumla wake kama ambavyo imeonesha hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi hii, naomba nikushukuru sana na naomba kuunga mkono hoja.