Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Godbless Jonathan Lema

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Taifa hili kujadili masuala yote yanayohusu mipango ya maendeleo bila kujadili stability na demokrasia muhimu katika Taifa hili, kinachojadiliwa hapa kilicholetwa na Dkt. Mpango hata kama kingekuwa ni sawa kwa asilimia 100 lakini kwa Taifa ambalo hakuna utawala bora, kwa Taifa ambalo demokrasia imeminywa, kwa Taifa ambalo vyama vya siasa haviruhusiwi kufanya shughuli zake mpaka mwaka 2020, mipango hii ina-create instability katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za nyuma tumekuwa tukisema kwamba nchi hii haitawaliki na tafsiri ya upande wa pili ikawa ni kwamba tunasema kwamba nchi hii haitawaliki kwa sababu tumepanga kuingia barabarani kufanya maandamano, kuvuruga Taifa. Maana ya nchi kutokutawalika ni viongozi walioko madarakani sasa ambao ndiyo wanaotawala Taifa hili kushindwa kabisa kujua na ku-predict future ya Taifa hili itakuwaje incase kama watashindwa kusimamia utawala bora na demokrasia katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongelea Mpango ambao una lengo la ku-attract investors. Mwekezaji yeyote mwenye akili hawezi kuleta mtaji kwenye Taifa ambalo limeua vyama vya siasa kufanya kazi zake za siasa. Maana yake ni nini? Lengo la kuua vyama vya upinzani likifanikiwa vilevile litakwenda kuuwa chama tawala chenyewe. Litauaje chama tawala? Ikifika mahali vyama vya upinzani haviwezi kuongea chama hicho ambacho kimefanikisha mpango huo kitazuia watu wake wasiongee na ndiyo sababu baada ya kikao cha asubuhi Wabunge wa CCM wengi walikuwa positive juu ya jambo hili kiliitwa kikao cha party caucus kwenda kuwaelekeza Wabunge namna gani ya kuja kuongea ndani ya Bunge hili badala ya kuongea ukweli ni kubeba Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa hili linapoelekea na mambo yote yanayopangwa hapa hayatatekelezaka bila utawala bora. Kwa bahati mbaya sana tunaongea Mpango wa Maendeleo wa Taifa hili katika Taifa ambalo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi Watendaji hawana confidence. Hakuna mfanyakazi wa Serikali nchi hii ana ujasiri wa kwenda asubuhi kazini ikafika jioni akajua bado yupo kazini. Jambo hilo limeleta wasiwasi na kwa sababu imeleta wasiwasi kwa Wakurugenzi, Makatibu Wakuu na kwa Mawaziri wengine hawajui ni wakati gani watatumbuliwa na ni kwa vigezo gani watatumbuliwa, kwa hiyo imekosekana creativity ndani ya ofisi za kazi na hakuna innovation. Ndiyo maana Bunge lenyewe likikosa pesa badala ya kwenda ku-push pesa zipatikane, Bunge ambalo lilisema lina fedha ya ziada likatoa fedha za madawati likapeleka kwa Rais Bunge hilo leo limeshindwa kuchapisha nakala zake. Sasa unajiuliza hili Bunge lililokuwa na ziada ya fedha likachukua fedha ikampelekea Rais ya madawati mbona leo imeshindwa kuwa na mpango wa kununua hata tonner ya kufanya kazi zake ndani ya Bunge hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongelea mpango bila kuongelea stability ya Taifa hili, demokrasia, ustawi wa jamii katika Taifa hili mipango hii hata kama ni bora kwa kiasi gani haitafanikiwa. Leo tulimuona Mheshimiwa Rais alikwenda kufungua kiwanda cha Bakhresa, akasema tena nimefurahi sana na zile sukari zilizokuwa zimekamatwa Waziri nendeni mkampe. Unajiuliza sasa kama sukari zilikuwa zimekamatwa kinyume na utaratibu kwa nini zilizuiwa na kama zilikuwa zimekamatwa ndani ya utaratibu kwa nini zilizuiwa mpaka Rais afurahishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo kwa sababu tukisema Waheshimiwa viongozi ambao ni sisi pamoja na huko nje tumekuwa na hofu kubwa dhidi ya kusema ukweli, dhidi ya kupigania ukweli, leo kila mtu ni muongo na woga ni njia anayotumia shetani kutenda miujiza na imani ni njia anayotumia Mungu kutenda muujiza. Kwa uoga huu ambapo watu hawawezi kuamua, kwa uoga huu hakuna mtu anakwenda kazini akajua jioni atabaki kuwa mfanyakazi, ndiyo maana Rais alisema watu wanaficha pesa, ni kweli kauli yake ilikuwa na uhalali kwa asilimia kadhaa. Mimi kama sina confidence ya kwamba nitakuwa kazini kesho maana yake itakuja ku-minimize gharama zangu za maisha. Mimi niki-minimize gharama zangu za maisha maana yake ni kwamba nakosa spending confidence kwenye jamii ndiyo sababu unaona biashara zinakufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kikao cha kodi cha TRA cha Wilaya nilimuuliza mtu wa kodi Arusha peke yake hizi kampuni za biashara ya kati zaidi ya 48 zimeandika barua ya ku-close business itakapofika Novemba mpaka Disemba mwaka huu. Sasa badala ya kumsaidia Rais na kumwambia ukweli na siyo mambo yote anafanya Rais Magufuli ni mabaya, ana courage ambayo watu wengi hawana, lakini courage hiyo ikikosa hekima, maelekezo na ushauri Rais anakuwa kama Mungu, anakuwa yeye ndiyo kila kitu, ndiyo Pay Master General, ndiyo Waziri wa kila kitu, anakwenda kufumania, kila kitu anafanya. Hii imesababishwa na ninyi kutokumwambia Rais ukweli, Rais amekuwa polisi. Imefika mahali hata mtu mdogo kwenye Kamati akiongea Rais anapiga simu mwenyewe, Rais anatoa maelekezo mwenyewe mpaka kwa ma-RPC, hofu kubwa imejengwa katika Taifa hili.
KUHUSU UTARATIBU...
MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namheshimu sana Mheshimiwa Jenista alikuwa Mwenyekiti wangu wa Kamati siku za nyuma, lakini nashukuru kwamba amekiri kwamba Mpango siyo mzuri na kwamba Mpango kutokuwa mzuri siyo intervention ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kitu tunachokisema ndicho ambacho mkiniambia ninyamaze sitanyamaza. Hili ni Bunge na kazi ya Bunge ni kushauri Serikali, inapofika mahali Bunge linashindwa kushauri Serikali ndiyo hiyo hofu aliyonayo, niliposema Rais ana courage ya kufanya maamuzi mazito na magumu mlipiga makofi, tukisema Rais anakosea hatumuudhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimesema nimeona maono kwenye maombi, leo nimepelekwa polisi na sasa hivi navyoongea nimeambiwa maelezo uliyotoa hayatakiwi, polisi wa Arusha wanakuja kunichukua kwamba nimeona maono makubwa kwa nini sijalala hata ndani nimepata bail kabla sijawekwa lockup, haya mambo katika Taifa hili yanakwaza. Sasa ninyi ambao mnamuogopa, mimi siogopi, najua Rais ana nguvu, najua hii Serikali ina Usalama wa Taifa, Mimi nikitaka kufa leo nakufa asubuhi I have no weapon lakini hatutaacha kusema ukweli for the sake of this country, hii nchi inakufa, imepandikizwa hofu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema hapa Mheshimiwa Mbunge mmoja kwamba Wakuu wa Mikoa na ma-DC na Wakuu wa Mikoa wanaweka watu ndani saa 48. Kuna mambo mengine tena mkiongea huko tutasema na Mawaziri tunaongea nao mambo haya nayoongea mimi tunawakilisha sisi, lakini haya ni mawazo ya kwenu mnayotuambia sisi, hatuwezi kuendelea na Taifa lenye hofu kwa kiwango hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mikoani OC hazijakwenda, hakuna fedha, mambo yanakuwa ni magumu, biashara zinakufa sisi ni wafanyabiashara. Utalii hapa mmempa Profesa ambaye Kinana alimuita mzigo some days ago, leo amekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Novemba peke yake utalii umeanguka kwa asilimia 48. TRA wamekuwa kama polisi, kontena la futi 40 lililokuwa linakadiriwa shilingi milioni 18 hadi 20 wakati wa Awamu ya Nne leo ni shilingi milioni 35 mpaka shilingi milioni 40. Wananchi wakiona TRA wanaona kama wameona wanajeshi kutoka Sudan. Hakuna friendliness kati ya walipa kodi na wanaotoza kodi. TRA wamejisifu wanakusanya kodi kwa muda mrefu, Mheshimiwa walikuwa wanakusanya arrears, leo kuna makampuni yameambiwa yalipe kodi ya miezi sita mbele watakuja kurekebisha baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Taifa linayumba, hali inakwenda vibaya, mitaani hakuna fedha, Tanzanite imeanguka kwa asilimia 40, utalii umeanguka kwa asilimia 48 kwa mwezi Novemba. Leo watu wanaopita Serengeti na Ngorongoro hata boda boda akipita mnamuweka kwenye database as if ni mtalii amepita. Mheshimiwa Maghembe akienda aka-print anakuja anasema watalii wameingia milioni moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mliongeza VAT na haya mambo alisema Mbunge hapa, mmekaa na Kenya na Uganda mkakubaliana pamoja, tathmini waliotumia watu wanaoshughulika na mambo ya uchumi ni kwamba Kenya International Airport imekuwa listed kama sehemu hatari ya utalii. Kenya juzi wakamleta mmiliki wa facebook wakamtembeza nchi nzima, ana wafuasi zaidi ya mamilioni ya watu, Kenya utalii unakua, Arusha hoteli zinauzwa, hakuna biashara kampuni zinafungwa, hoteli zinauzwa hata wateja hakuna benki zinafunga. Ukienda leo kwenye DSE, CRDB hali siyo nzuri, Twiga Bancorp imekabidhiwa kwa BOT, uchumi unakwenda hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haya mambo kwenu ni mabaya ni mabaya kwa manufaa ya nchi hii. Ule UKUTA tuliosema tunautangaza kama hamtarekebisha mfumo wa kiuchumi na kiutawala sisi hatutaingia barabarani ila iko siku mtatuomba tuwaambie watu warudi nyumbani hali itakuwa ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Taifa hili Rais hasafiri kwenda kutafuta partners. Leo amekuja hapa Mfalme wa Morocco juzi kaenda Zanzibar kapiga pensi na tisheti yake ina ganja, ina bangi hapa kifuani huyu, ndiye mwekezaji…
Mheshimiwa hujaona wewe.
MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde dakika zangu ambazo Mheshimiwa Jenista alinipotezea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Mfalme na lile jani la mzaituni ambalo linatumiwa na vijana wengi sana wa mjini. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachosema ni nini? Nachotaka Bunge hili lielewe ni kwamba kazi ya Bunge hili ni kuisaidia Serikali maana yake ni kwamba Serikali hii itayumba, kumwambia Rais ukweli siyo kumdharau, kumwambia unakosea siyo kumdharau. Mfalme ambaye haambiwi ukweli siku akishtuka mlikuwa mnamdanganya na hamumuambii ukweli atafukuza wote kazi. Kwa sababu huko tunakoenda atashtuka na atauliza kwa nini sikuambiwa ukweli kuna jambo kama hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema Taifa kama hili ambalo limejaa hofu na wasiwasi ambapo hakuna mtu anayejua kazini atakuwepo mpaka kesho ama kesho kutwa ni Taifa ambalo limekosa creativity na innovation.