Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia kwenye mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri isingekuwa sahihi sana kama Wabunge wengine ambavyo wamezungumza kuanza kuchangia kwenye mpango huu au mipango mingine yoyote ya Serikali kabla ya kufanya tathmini ya mpango uliokuwepo ambao tunaendelea nao sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko kwenye quarter ya pili ya bajeti, Halmashauri hazijapelekewa pesa, hazijapelekewa OC, watu wanalia, mnataka wakusanye mapato lakini hamjawawezesha kuweza kukusanya hayo mapato, kwa sababu bila OC sijui mnataka watu watembee kwa miguu kwenda kwenye minada kukusanya pesa, haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema hivi, mimi sio mtabiri, lakini nataka nikuambie Waziri Mpango baada ya Waziri aliyetumbuliwa hapa unamkumbuka, anayefuata ni wewe, wewe ndio utakuwa wa pili kutumbuliwa na Mheshimiwa Rais Magufuli. Na kwa nini utakuwa wa pili ni kwa sababu mambo yanapokwama, mipango mliyopanga yote inapokwama wewe ndio utabebeshwa zigo hilo ili aonekane yeye yupo sawa wakati mnakosea wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira; mnaleta hapa kuzungumza mipango hii, mlisema hamuajiri kwa sababu mnafanya tathmini ya watumishi sijui kutafuta watumishi hewa, haya mmetafuta hewa mwaka mzima, vijana wamesomeshwa na baba zao watu maskini wako mitaani, dada zetu wanajiuza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo nayo sijui mnatafuta wanafunzi hewa. Kilimo hakuna pembejeo mnatafuta majembe hewa, mnatafuta wakulima hewa? Jambo la msingi ni kwamba mseme Serikali yenu imefilisika na haiweze kutekeleza chochote msaidiwe kuliko mnakuja hapa mnasema watumishi hewa, watumishi hewa mnatafuta mwaka mzima, wakulima hewa mnatafuta mwaka mzima, kilimo kimesimama. Wanafunzi mkawapa mikopo mwaka jana, mambo ya aibu kweli kweli! mwaka jana tumewapa mkopo leo mtu anaingia mwaka wa pili hamtaki kumpa mkopo, wengine wanaingia mwaka wa tatu hamtaki kuwapa mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yenu hii mlitoa matumaini mnasema hapa kazi tu, hapa kazi nini sasa watu hawana mikopo wanafunzi wanalia, mnatoa mtoto kijijini anakwenda chuo anafika pale hana pa kuishi, hakuna mkopo, ni matatizo kwenye familia. Sasa mimi nakutabiria Mpango unakaribia sana kutumbuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye elimu; elimu yetu wakati anazungumza pale Mheshimiwa Mapunda, amesema vitu vinne ambavyo vinahitajika kuwepo kwa viwanda amezungumzia personnel au man power, ni man power ya aina gani ambayo imeelimika ili iweze kuajiriwa kwenye hivyo viwanda?
Leo elimu ni majanga; mama yangu Profesa Ndalichako mimi nilikuwa nakuheshimu sana ukiwa Katibu wa Baraza; umewahi kutoka pale unaonesha watu wamechora ma-zombie kwenye mitihani, wewe umepewa Wizara hii umechora zombie kubwa kuliko wale wanafunzi. Na sijui hata wizi wa mitihani utazuiaje kama wewe Profesa ulitoka hapa kwenda kuiba kura Kinondoni, sijui. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika elimu hivi baada ya wewe kutoka hapo na Uprofesa wako na ni kwa nia njema tu, kwa sababu hili Bunge mmelifanya kama idara fulani ya pale Ikulu labda hata ya umwagiliaji maji pale, kumwagilia maua ndio maana leo Wabunge wanasimama hapa wanasema ukweli hali halisi ya uchumi ni mbaya, wengine wanasimama wanatetea. Jana tu walikuwa wanazungumza hapa wanapiga makofi, sasa hivi wamegeukana na mimi nilijua hamtafika mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya uchumi ni mbaya hata kwenye kununua vocha tu, ukinunua vocha ulikuwa unapewa GB sita leo ni GB 2.5 kwa shilingi 10,000; yaani hata mtu ambaye hajaenda shule anajua. Kwahiyo, hali ya mazingira ya mtaani elimu inazidi kuporomoka.
Tumetengeneza madawati tumepeleka, maeneo mengine madawati yapo nje yananyeshewa hapa kwenye mpango hamjaonesha mkakati wowote wa kujenga vyumba vya madarasa ili yale madawati tuliyopeleka yaingizwe ndani, yataoza kwenye miti, mwakani tena tuanze kukamatana kupambana na watu wanunue madawati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea kwenye elimu hapa Profesa Ndalichako ungekuja na mpango ambao utaondoa elimu yetu hii kwenye mkwamo, ambao tutajua kutakuwepo na maandishi yanayoeleweka kwamba elimu tunayoenda nayo ni ya aina hii, tutoke kwenye elimu ile ya akina Mungai ambayo tulikuwa tunaunganisha hesabu sijui na historia na wewe unaendelea huko huko. Leo mnafanya hivi kesho mnafanya hivi, keshokutwa mnatoa vigezo hivi, siku nyingine mnatoa vigezo hivi. Mimi nawaasa vijana Watanzania wote ambao Serikali hii imewatosa haitaki kuwapa mikopo wajue wana nguvu nyingi sana za kuunganisha kura yao ili mwaka 2020 waondoe Serikali hii kwa sababu hakuna matumaini katika maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda; amezungumza vizuri sana Mheshimiwa Chegeni hilo ndio jina la yule bwana sio sisi tunaosema ni wananchi. Ukikutana naye hapo nje ukamsimamisha Waziri vipi, nikupe kiwanda? Anaingiza mkono mfukoni, anataka kuchomoa kiwanda mfukoni akukabidhi. (Makofi/Kicheko)
Mpango wenu hamjajenga kiwanda hata kimoja mpaka sasa, mmebaki mkisikia Bakhresa anataka kufungua kiwanda mnakimbia pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda Mheshimiwa Waziri Mpango wewe unajua, ni msomi na uwe unasikiliza watu hapo unaelewa. Kiwanda ndiyo kinaajiri kuanzia mama lishe mpaka engineer kiwandani peke yake. Kwa sababu mama lishe atakuwa pale atawauzia wabeba mizigo wa viwandani, atawauzia madereva wanaobeba mizigo kwenye kiwanda. Kiwanda kitaajiri engineer wa kuendesha mitambo, kiwanda kitaajiri mhasibu, kiwanda kitaajiri kila mtu.
Leo umekuja hapa, kwanza ninyi wenyewe Serikali hii ambayo sasa inataka kufuta eti siyo yenyewe, Serikali hii ya CCM ikaua viwanda, ikauza viwanda. Mmerudi mmeimba Serikali ya viwanda, leo tunaelekea mwaka mmoja na siku kadhaa hata kiwanda cha pini hamna mpango nacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkisikia Bakhresa anazindua kiwanda chake mnakimbia pale mnasema sukari tuliyokunyang‟anya tunakurudishia na shamba tunakupa zawadi. Halafu mnatoka pale kwamba tumefungua kiwanda. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taarifa mnakataa hapa kwamba Serikali haijaishiwa kuna taarifa mnatisha wafanyabiashara, mtu amelipa ushuru ana risiti mnamwambia hizo ni risiti fake, Serikali iliyokuwepo ilikuwa inatoa risiti fake. Mnawalipisha watu kodi mara mbili.
Leo Benki zinatangaza hasara, wewe ni msomi utuambie nini implication ya benki kutangaza hasara, CRDB wamesema, nini implication yake kiuchumi? Maana msituambie tu kwamba uchumi unakuwa vizuri, uchumi unakuwa vizuri watu wanalia mtaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mmewaruhusu traffic, Wabunge walikuwa wanalia hapa kila traffic ameambiwa kwamba kwa siku ni lazima apeleke makosa matatu. Leo makosa ya barabarani ni chanzo cha uchumi kwa Serikali ya CCM, aibu. Makosa ambayo yanatakiwa kuzuiwa watu wasifanye makosa ninyi mna-encourage ili mpate uchumi….
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Kuhusu Utaratibu!..
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba unilinde kidogo muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Leo wakuu wa traffic nchi nzima wanatangaza mapato yaliyopatikana kutokana na makosa kwamba mwezi wa tisa tumepata bilioni kadhaa kutokana na makosa, nini maana yake? Kama hamu-cherish yale makosa kwamba ni chanzo cha mapato cha Serikali hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, makosa yale nafikiri yamewekwa ku-discourage watu kuendelea kufanya makosa, lakini unapotangaza unajisifu kwamba ma-traffic wamekamata makosa kadhaa ina maana ni chanzo mmeweka pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema siyo kwa nia mbaya ni kwa ajili ya kuwaambia hawa watu wasikie waelewe kwamba waliambiwa hapa tukikosa mapato yanayotokana na bandari mtaanza kufukuzana na bodaboda, watu walisema humu mkatuzomea. Sasa leo tunaposema haya hamtaki tena, mnataka tukae wapi? Tukisema hili ninyi kwenu baya, tukija hapa ninyi kwenu baya mnataka nini sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliwaambia mkipoteza mizigo nchi hii haitawezekana. Leo eti TRA wanataka wawe TRA ya Congo pia wamesema Wabunge wengine hapa, yaani mnataka kujipa majukumu ya kukusanyia Congo kodi. Kwani kama Congo kule wanakwepa kodi ninyi inawahusu nini? Wamepitisha hapa, wamewalipa mapato yenu, mnachukua mnafanyiakazi, mnataka kuwakusanyia Congo ili wawape nini? Mmekuja hapa mnaongea na Rais wa Congo anawahakikishia mizigo itaongezeka, imeongezeka? Kwa sababu hana mandate ya kuwaambia wafanyabiashara lazima wapitie hapa na wao wamehamia Beira, wamehamia Mombasa sasa wote tunapiga miayo hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunadanganyana tumepandisha bajeti kutoka shilingi trilioni 22 desperately kabisa kwenda shilingi trilioni 29 eti mnataka hadi Mama Lishe alipe kodi, Mheshimiwa Mpango, mama lishe alipe kodi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana mnawaambia hawana ajira eti wajiajiri, wewe mwenyewe umeshindwa kujiajiri umeomba Ubunge hapa unataka kijana wa mtaani ajiajiri. Wabunge wote hawa tumeshindwa kujiajiri tukaenda kuomba ajira kwa wananchi, wengine Profesa sijui na nini. Kijana aliyemaliza mwaka wa kwanza mnamwambia nenda ujiajiri kule! Vijana hawawezi kutengeneza ajira!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jukumu la Serikali yoyote duniani kulinda watu wake na ni aibu kwamba leo nchi hii wakati wa hapa kazi tu hakuna madawa kwenye mahospitali; miradi yote mliyoweka ya kielelezo haiendi, barabara hamtengenezi tena na wengine hapa walikuwa wanaitukana Serikali ya…
MWENYEKITI: Ahsante.