Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri wa Fedha na Mipango kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri, amefanya kazi yake na mpango huu ni mpango mzima wa Serikali. Ni matarajio yangu kwamba tunapozungumza mpango huu hatuzungumzii peke yake Waziri wa Fedha, tunazungumza co-ordination yote ya Serikali ndani ya mpango huu. Kwa maana hiyo Waziri Mpango naomba uwe msikivu, lazima uwe msikivu na ujaribu kuyachukua mawazo yote ambayo Waheshimiwa Wabunge tunayatoa hapa kwa mustakabali wa nchi hii.
Mheshimiwa Mpango nikupe tu siri moja, ni mtaalam mzuri, msomi mzuri, lakini una professional arrogance, una kakiburi, na mtu anayekwambia ukweli anakusaidia. Tunasema hivi ili baadae tutoke hapa tulipo tusonge mbele zaidi. Wenzangu wamesema tunaheshimu kila Mbunge aliyepo hapa ndani kwa sababu ameingia kwa nafasi yake, na wewe uko hapa kwa heshima zote, lakini chukua mawazo ya Waheshimiwa Wabunge yafanyie kazi, usipofanya hivi inatupa ugumu sisi na ukakasi wa kusema na wewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi nyuma Mheshimiwa Mpango kwenye bajeti ya Serikali iliyopitishwa mwaka jana, vitu vingi tulipendekeza hapa vilikuwa na mambo mazuri sana, lakini nadhani kwa kufikiria kwako au kwa kuona kwako mambo mengi hayakufanyika kama tulivyokuwa tumependekeza. Hii sisi ilitupa nafasi ngumu sana ya kuelewa sasa tunakwendaje kama Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili mpango huu unapaswa kuwa tenganifu, we should harmonise, mambo yote ambayo yanahusika katika kuwezesha uweze kutekelezeka. Haiwezekani tunapanga mipango, unakuja na kitabu hiki, hutuelezi vizuri kwamba hapa ya mwaka jana tumefanyaje, wapi tumekwama, nini tufanye kwa safari hii! Kwa sababu unapozungumza katika suala la mpango, lazima tu-reflect tumetoka wapi, nini tumefanya, nini tumeshindwa kufanya na nini tukifanye zaidi kipindi kinachokuja. Sasa Mheshimiwa Mpango naomba utusikilize sana, tunapotoa ushauri ni kwa nia njema, lakini vilevile tuki-echo kazi nzuri anayofanya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amekuwa na nia njema sana, lakini naanza kupata wasiwasi kwamba inawezekana mlio karibu nae hamtoi ushauri stahiki kwake, hii inasababisha baadhi ya mambo mengine yasifanyike kama ambavyo watu wanategemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tunaomba ifanye kazi kama timu moja. Haiwezekani Serikali hiyohiyo Waziri huyu anasema hiki, huyu anasema hiki, hakuna co-ordination! Na hili ndiyo tatizo ambalo linafanya hata Bunge hili lishindwe kuwashauri vizuri zaidi. Kwa hiyo, naomba sana kupitia mpango huu Mheshimiwa Mpango ongoza wenzako katika kutekeleza mpango huu, lakini uwe msikivu, usikivu wako utakusaidia ili tuweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sasa hivi tunasema uchumi unakua. Ni kweli, ukienda by figures and facts they never lie, lakini hali halisi lazima iwe translated kwa wananchi wenyewe, waweze kuona kwamba uchumi sasa kweli unakua. Kama hakuna translation, hakuna trickle down effect, hata tungesema namna gani hii itakuwa ni ngonjera ambayo haina mwimbaji.
Nakuomba sana suala zima kwa mfano la kodi, tulisema hivi suala la kuweka VAT on auxiliary services and transit goods italeta matatizo. Tukiweka VAT kwenye tourism sector italeta tatizo! Tumeona yote haya kwa mfano sekta sasa hivi ya utalii imedorora, lakini mnasema eti imekua! Sasa nashangaa inakuaje wakati tunaona kabisa the actual situation hali ni mbaya, wewe unasema inakua!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumneona suala la bandari, ndiyo kulikuwa kuna ukwepaji kodi, suala la kimfumo na utaratibu TRA wangeweza kufanya kudhibiti, lakini tunategemea kwamba tupate floor nyingi ya mizingo inayokuja tuweze kupata mapato makubwa zaidi, Mheshimiwa Mpango naomba haya mambo ujaribu kuyasikiliza vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi tuka-introduce VAT on financial services. Tunaona sasa hivi mabenki yanavyo-suffer. Tunaona jinsi ambavyo hali ya kibenki na hali ya kiuchumi inavyozidi kuyumba. Tunaomba sasa kufanya kosa siyo kosa, kurudia kosa ni makosa. Tujisahihishe, kama kuna mahali tulikosea tujaribu kurekebisha mapema, tusiwe tunajaribu ku-copy mambo fulani na kuja kuya-paste hapa, tuyafanyie kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba suala zima la perception management lifanyiwe kazi. Kuna watu wana perception za kwao kwamba sasa hivi uchumi wa Tanzania unakua, wengine wanasema uchumi wa Tanzania haukui, lakini ninaamini kwamba kwa sababu numbers na figures never lie uchumi unakua, lakini tunachoomba ni translation ya uchumi huo kwa wananchi waweze kuona kwamba uchumi unakua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Halmashauri nyingi hazina fedha, Serikali haina pesa, wananchi hawana hela! Sasa unapozungumza production, kukua kwa uchumi ni pamoja na production, sasa kama production haiongezeki uchumi hauwezi kukua. Wananchi watazidi ku-suffer na ku-suffer, mimi ninaamini kwamba Serikali hii ni sikivu na inajaribu kuyafanyia kazi mambo ambayo yamekuwa yana matatizo yaweze kurekebishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imebana sana spending yake, lakini fedha iko wapi? TRA makusanyo yameongezeka kutoka shilingi bilioni 850 mpaka 1.3 trillion, lakini ukiangalia outflow ya pesa tumekuwa na madeni, Deni la Taifa linazidi kupanda utadhani as if Waziri wa Fedha hutumii nafasi yako kuya-manage haya kwa sababu you need to do a financial management, is just a simple financial management.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani pesa zinazidi kutumika zaidi licha ya makusanyo kuongezeka, lakini bado spending yake inakuwa challengeable! Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri kupitia mpango huu ninaamini kwamba Watanzania tuna imani na wewe na Bunge hili litumie kama ni chachu ya kukusaidia wewe ufanye kazi yako vizuri zaidi, lakini timiza wajibu wako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema hata kwenye maandiko mtu mnyenyekevu hata Mungu anampa baraka, nyenyekea Mheshimiwa Mpango, unapewa ushauri na watu sikiliza. Watu wa Business Community wamekuita mara nyingi ukutane nao unakataa! And then you came to the budget! Kamati ya Bajeti hapa, walikuwa wanasema Waziri tunamuita haji kwenye vikao. Sasa najiuliza kwamba sasa ni Waziri anafanya kazi gani hizi? Ni aibu, ni aibu. Dhamana ambayo unayo ni kubwa, hebu jaribu kuwa msikivu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni sekta ya kilimo, sekta ya uvuvi ambayo inaajiri watu wengi sana inatakiwa sasa iwekewe kipaumbele, ili wananchi sasa na hasa wakulima, wavuvi na uzalishaji wa viwanda, tunasema kwamba ni Serikali ya viwanda, sera yetu ni ya kujenga viwanda, lakini huwezi ukajenga viwanda ukafanikiwa kama unakuta Waziri wa Viwanda tena wanamuita mzee wa sound! Eti mzee wa sound, Waziri wa Viwanda ni mzee wa sound! Haiwezekani! Tunachotaka sisi ni Waziri azungumze vitu ambavyo vinatekelezeka siyo porojo za kila wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tufike mahali tukubali changamoto hizi, tupunguze maneno lakini tuwajibike zaidi na tutekeleze zaidi. Leo hii wananchi wanachotaka ni kuona kwamba matokeo yanapatikana. Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa sana, anafanya kila njia kuona Watanzania wananufaika na uchumi wao, Watanzania wananufaika na rasilimali zao na ninyi msaidieni sasa kwa nafasi zenu acheni maneno. Acheni kusigana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia wenzetu wa Kenya walianzisha kitu kinachoitwa interest rate capping. Riba kwenye mabenki zinazidi kupanda na zinapopanda ina maana wananchi sasa hivi wanashindwa kukopa fedha, wanashindwa kufanya production, kuna haja sasa Mheshimiwa Mpango suala zima la riba kwenye benki liangaliwe upya. Serikali ifanye serious intervention ili kusudi mabenki haya yawasaidie wananchi kama wanakopa fedha basi ziweze kutumika vizuri katika kukuza uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kusema kwamba lazima baadhi ya gharama nyingine za uzalishaji hapa Tanzania zipungue gharama. Huwezi ukasema unaweka viwanda wakati gharama ya umeme ni ghali, maji ni ghali, halafu kuna series kubwa sana ya kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kodi zaidi ya 100 ambazo mtu anapaswa kuzilipa, haiwezekani! Ninaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha kupitia mpango huu hebu jaribu kuja na kitu ambacho kitasaidia ku-harmonise yote haya. Vinginevyo mpango wako ni mzuri na mimi sijawahi kukukosoa, mpango huu ni mzuri, lakini hakikisha kwamba unakuwa msikivu na yale mambo ya msingi yafanyie kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba yawezekana tuna itikadi tofauti, lakini maslahi yetu ni ya Watanzania wote. Hakuna mtu ambaye ana maslahi nje ya Watanzania na lolote unalolifanya ndani ya Bunge hili litusaidie kumsaidia Mtanzania ambaye ndiye ametuweka sisi hapa ndani. Ninaomba sana Waheshimiwa Wabunge kupitia Bunge hili na haki za Wabunge ziweze sasa kuzingatiwa kwa sababu vilevile Mbunge aweze kufanya kazi zake anahitaji kuwa na uwezo wa kufanya kazi zake.
Mheshimiwa Mpango pamoja na yote kapu lote umelikamata wewe na usidhani kwamba watu wanavyokuona namna hii wewe ni Waziri zaidi ya Waziri kwa maana umeshika sekta nyeti, lakini hakikisha kwamba unamshauri Rais vizuri, sikiliza wadau na mtekeleze yale ambayo Watanzania wanahitaji kuyaona. Tungependa kuona kwamba ndoto ya Mheshimiwa Rais Magufuli inatimizwa na Watanzania baada ya miaka mitano tuseme kwamba sasa uongozi wa Awamu ya Tano wa Serikali ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli umeweza kufanya moja, mbili, tatu na tujivunie kwa hilo, lakini naomba katika mpango huu vilevile sekta zote na Wizara zote zinakuwa harmonized hii itatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawaziri wote, Mheshimiwa Chief Whip, mpango huu Mawaziri wanapaswa kuwa humu ndani wasikilize, ni wajibu wao kuona kwamba kila Waziri katika sekta yake anashiriki kikamilifu katika mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana.