Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha hatua hii tuliyofika jioni hii ya leo kama Wizara na kama Serikali. Pili naomba nimshukuru na nimpongeze kwa dhati kabisa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya katika kusogeza mbele gurudumu la maendeleo la Taifa letu. Pia naomba nikushukuru wewe mwenyewe Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujasiri wako, kwa kusimamia haki na kuhakikisha kwamba haki inasimama na nidhamu inarejea ndani ya Bunge letu Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia, niwashukuru Wabunge wote waliochangia hoja iliyowasilishwa mezani na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Michango yenu tumeichukua ni mingi, tunawashukuru sana na sina uhakika kama tutaweza kuijibu yote hapa, tutajibu machache, lakini kiuhalisia tumechukua na tutawajibu kimaandishi, tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba kuunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache ya utangulizi, naomba sasa nichangie hoja chache ambazo zimejili katika majadiliano ya Waheshimiwa Wabunge katika kujadili na walioleta kwa maandishi pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza, ambayo ningependa kuichangia ni Ucheleweshaji wa Michango ya Mwajiri na nyongeza ya Pensheni kwa Wastaafu wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kabisa, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango inawajibika sana kuwasilisha mchango wa mwajiri kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wote wa Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2015/2016, Serikali imefanya jitihada kubwa sana katika kuwasilisha michango hiyo. kwa mfano, mchango wa mwajiri uliotarajiwa kuwasilishwa ni Shilingi bilioni 797. 781, hadi kufikia Mei, 2016, Wizara imewasilisha Shilingi bilioni 529.932 kama mchango wa mwajiri kwa Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Wizara na kama Serikali, bakaa ya Shilingi bilioni 267.849 itawasilishwa kabla ya tarehe 1 Julai, 2016. Kwa hiyo, kama Serikali tunatoa Commitment mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba, michango yote hii ya waajiri tutaweza kuiwasilisha katika Mifuko yetu yote ya Hifadhi ya Jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa mujibu wa kifungu namba 30(3) na (4) cha Sheria ya Mfuko wa PSPF namba Mbili ya mwaka 1999, Serikali inatakiwa kuwasilisha pia tofauti ya nyongeza ya pensheni kwenye Mfuko wa PSPF. Kuanzia Julai, 2015 hadi Aprili, 2016 Wizara imewasilisha PSPF kiasi cha Shilingi bilioni 75 kati ya Shilingi bilioni 94 zilizotakiwa kuwasilishwa. Pia tunatoa commitment ya Serikali yetu kwamba, bakaa la bilioni 18 tutaweza kuliwasilisha kabla ya tarehe 1 Julai, 2016 ili kuwezesha Mfuko wetu wa PSPF uweze kufanya kazi zake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu Serikali yetu inafanya kazi kwa Cash Budget. Kwa hiyo, michango ambayo hatujamalizia ni kutokana na mapato, ambayo tumekuwa tukikusanya. Hata hivyo, sote sisi ni mashahidi, kupitia Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, tumeweza kuongeza mapato tangu Serikali yake ilipoingia madarakani na ndiyo maana tunatoa commitment hizi kwamba, tutamalizia bakaa zote zilizobaki katika michango ya hifadhi ya jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongelee hoja namba mbili, ambayo ni tatizo la Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali kutoa takwimu zinazotofautiana juu ya suala moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili ni kweli lipo, lakini kama Serikali hatujakaa kimya, tumeendelea kulifanyia kazi. Ofisi ya Taifa ya Takwimu, tunafahamu ndiyo yenye mamlaka kisheria kuratibu na kusimamia utoaji wa takwimu rasmi zinazotumiwa na Serikali na wadau wengine kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kutoa takwimu zinazotofautiana, Serikali tumeona tatizo hili na hivyo ilitungwa Sheria ya takwimu ya mwaka 2002; kwa sababu ya kukosa nguvu kisheria ilibadilishwa mwaka jana mwaka 2015 na sasa hivi tunajipanga vizuri zaidi ili kuweza kufika na kuja na takwimu ambazo ni sahihi zitakazoweza kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Sheria hii, ambayo imeanza kufanya kazi kuanzia mwezi Novemba 2015, Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, imeanza kutengeneza Kanzidata ijulikanayo kama e-population register, ambayo itaandikisha watu wote katika Kaya na kuunganisha na masuala ya elimu, hali ya ulemavu, afya, kilimo, kazi na masuala mengine katika jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kanzidata hii ni maelekezo ya kifungu cha 56 cha Sheria za Serikali za Mitaa ya Mwaka 1982 pamoja na Kanuni ya Pili na ya Tano ya taratibu za kazi za Mwenyekiti wa Mtaa au Kitongoji ya mwaka 1993 pamoja na Tangazo la Serikali namba Tatu la tarehe 7 Januari, 1994; ambalo linasisitiza kila Mtaa, Kitongoji kuwa na Register ya wakazi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kutambua umuhimu na Mamlaka yake Kisheria, imeanza kutekeleza kazi ya kutengeneza kanzidata ya Taifa, ambayo itasaidia Serikali kuwa One Stop Centre ya Takwimu Rasmi katika sekta zote za katika nchi yetu kwa kutumia takwimu za utawala Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi, mfumo huu unafanyiwa majaribio katika Kata ya Mapinga, Mkoani Pwani na baadaye tutaendelea nchi nzima. Kupitia Ofisi ya Takwimu ya Taifa, kazi ya kuimarisha takwimu za utawala, umetengewa jumla ya Shilingi bilioni 1.6 kwa nchi nzima kwa bajeti ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kuwaomba Wananchi wote kupitia sisi Wabunge wao kutoa ushirikiano wa kutosha kwenye zoezi hili kwa ajili ya Taifa letu. Pia Watendaji wa kata, vijiji, vitongoji na mitaa watoe ushirikiano wa kutosha ili tuweze kuwa sasa na takwimu zilizo sahihi kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya tatu, ambayo ningependa kuitolea ufafanuzi ni hoja iliyoletwa na Kambi Rasmi ya Upinzani, kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi maalum katika Kitengo cha Madeni na Uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali haina pingamizi na mapendekezo haya ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi maalum katika Kitengo cha Madeni na Uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi Jamii ili kujiridhisha na usahihi wa taarifa zilizopo. Ni wajibu wa CAG kufanya kazi hiyo na Serikali itampa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha kazi hiyo kwa wakati na kwa kadri Bunge litakavyoelekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ushauri wa kutenganisha deni halisi la Taifa na Matumizi mengineyo yanayohusu Mfuko Mkuu wa Hazina pia tutaufanyia kazi kwa kadri itakavyowezekana. Ingawa hakuna ubadhirifu wowote ulioripotiwa katika Mfuko huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa ni fedha zilizoidhinishwa na Bunge hazitolewi kama zinavyoidhinishwa. Kama nilivyotangulia kusema, tunafahamu mfumo tunaoutumia kutoa fedha za utekelezaji wa bajeti yetu ni mfumo wa Cash Budget. Kwa mfumo wa Cash Budget, fedha za miradi ya maendeleo pamoja na matumizi ya kawaida hutolewa kulingana na mtiririko wa upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ni vyema ikaeleweka kuwa bajeti ni makadirio ya mapato na matumzi, hivyo ni muhimu lakini si lazima bajeti iliyopangwa au kuidhinishwa na Bunge ilingane na matumizi halisi kwa sababu inaangalia uhalisia wa mapato tutakayokusanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kama nilivyosema mwanzo, Serikali inaendelea na jitihada za kuboresha upatikanaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ili kuweza kutoa fedha kama zinavyoidhinishwa na Bunge. Tunatarajia kabisa kwamba mapendekezo yetu ya bajeti yetu tutaweza kuyafikia kwa kiwango kikubwa kutokana na uboreshwaji wa mapato ambayo Taifa limeyafikia kwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa inasema Serikali iruhusu kutumia fedha za maduhuli badala ya kupelekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Kama Serikali, tungependa kufanya hivyo, lakini utaratibu wa fedha za maduhuli kupelekwa Mfuko Mkuu unasaidia kuwepo kwa mgawanyo mzuri wa fedha kwa taasisi au Wizara ambazo hazikusanyi maduhuli, mfano Ofisi yetu ya Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kuruhusu maduhuli yatumike sehemu yanapokusanywa bila kupelekwa Mfuko Mkuu kuna hatari kubwa ya baadhi ya taasisi zetu kutopata fedha na kusababisha kushindwa kutekeleza majukumu yake. Serikali ina vyanzo mbalimbali vya fedha kwa ajili ya kutekeleza bajeti yake. Fedha za maduhuli ni mojawapo ya chanzo cha mapato ya Serikali yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiruhusu fedha hizi za maduhuli zisipelekwe kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, ipo hatari ya Wizara, taasisi na mikoa isiyokusanya kutopata fedha za kuendesha ofisi, kuendeleza shughuli za maendeleo na kulipa mishahara. Hivyo fedha za maduhuli zinapaswa kupelekwa Mfuko Mkuu ili ziweze kugawanywa katika mafungu mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza bajeti iliyoidhinishwa, ambapo makusanyo ya maduhuli ni asilimia 15 ya mapato yote ya ndani. Tunawaomba Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono katika hili ili tuweze kutekeleza bajeti yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa Serikali iwalipe wastaafu kwa wakati wanapostaafu, ikiwa ni pamoja na kuwalipa pensheni kwa kutumia viwango vyao vya mshahara wa mwisho. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba mishahara ya mwisho kwa watumishi wenye masharti ya ajira ya kudumu na malipo ya uzeeni ndiyo inayotumika kukokotoa kiinua mgongo na pensheni ya watumishi hao mara wanapostaafu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wastaafu ambao nyaraka zao za kustaafu zinawasilishwa kwa wakati, yaani angalau miezi mitatu kabla ya mtumishi husika kustaafu na zikiwa hazina kasoro yoyote, wamekuwa wanalipwa mafao yao kwa wakati. Ili kuhakikisha wastaafu wote wanalipwa kwa wakati, waajiri wanashauriwa kuwasilisha nyaraka zote ili tuweze kuwalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia napenda kuwaomba waajiri wote, upo mchezo ambao unafanyika mwajiriwa anapokaribia kustaafu, amebakiza miezi miwili kustaafu tayari ameshapeleka nyaraka zake mbalimbali katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, unakuta sasa mwajiriwa huyu ana-collude na mwajiri wake, anapandishwa cheo, kwa hiyo hii ndiyo inayoleta utata. Tayari nyaraka zake zilishapelekwa, sasa inakuwa ni vigumu, umepandishwa cheo mwezi mmoja kabla ya kustaafu inakuwa ni changamoto kushughulikia mafao yako pale ambapo mwajiriwa huyu anapostaafu. Hivyo niwashajihishe waajiri kupeleka nyaraka zote pale miezi mitatu inapokaribia mstaafu huyu anatarajia kustaafu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine iliyowasilishwa na ambayo napenda kuitolea maelezo ni kwamba mikopo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo haujasaidia kubadilisha hali ya maisha ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kuna kipindi cha mpito kati ya kukua kwa deni la Taifa linalotokana na mikopo ya miradi ya maendeleo na ustawi wa maisha wa wananchi wetu. Tunafahamu wote ukikopa leo deni linaongezeka leo lakini utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo unachukua muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuna lax period ambayo lazima turuhusu miradi hii inapokuwa imeshatekelezwa, kama miradi mingi ya ujenzi wa barabara, then tutaweza kuona maisha ya wananchi wetu yanaendelea kubadilika. Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba muda si mrefu maisha ya wananchi wetu yataendelea kubadilika na mpaka 2025 tutakuwa ni Taifa la kipato cha kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongelee tatizo moja ambalo limeongelewa ambalo nalo nimeona Wabunge wengi wameliongelea. Nayo ni marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ambayo haijajumuishwa katika Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali uliogawiwa kwa Wabunge; wanaomba Serikali iwasilishe marekebisho ya Sheria hiyo haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410, yatawasilishwa Bungeni kupitia Muswada wa Sheria unaojitegemea kuhusu marekebisho ya sheria hii. Serikali imejipanga kuwasilisha Muswada huu katika Bunge hili la Bajeti linaloendelea sasa hivi. Kwa hiyo, naomba niwape comfort Waheshimiwa Wabunge, marekebisho hayo yatakuja na sheria hii itafanyiwa marekebisho kabla Bunge hili halijafika mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naomba nirudie kusema naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Nakushukuru sana.