Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa fursa ya kuchangia Wizara yetu hii ya Fedha. Kabla ya kuchangia mimi niseme maneno machache sana, jambo usilolijua ni kama usiku wa giza. Watu ambao wanakukimbia wewe, wanatoka nje wanakuacha wewe hawakujui. Wewe unajua mimi nakujua sana kabla hujawa Naibu Spika, utendaji wako ulikotoka, chuoni, maisha yako yote, mwadilifu, mpole, msikivu, mtoto wa maskini, umesoma shule za kawaida, unajua mila za Kitanzania, wewe ni mzalendo, hawakuwa na sababu ya kutoka, wametoka hawa ni kama usiku wa giza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uwe na moyo, wale wote wanaokufahamu kule nje, wanayokwenda kuyasema watawazomea. Sisi tuliobaki humu ndani tunakufahamu fanya kazi, tuamini, tuko nyuma yako. Mimi nakupongeza sana, nampongeza pia Mheshimiwa Rais aliyekuteua kuwa Mbunge na baadaye ukagombea nafasi ya Naibu Spika. Nafasi ya Naibu Spika hajakupa Mheshimiwa Rais tumekupa sisi Wabunge kwa kukupigia kura. (Makofi)
Mhehimiwa Naibu Spika, kila jambo lina mwanzo wake, mwanzo wa wewe kuwa Naibu Spika ni sisi Wabunge humu ndani, walielewe hilo. Tunataka ufanye kazi na tunakuunga mkono sisi. Wote tuliobakia na walioko nje, raia, wananchi wa Tanzania wanakupenda, wanakuamini, fanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo sasa nichangie hoja iliyopo mezani na nitajikita katika mambo matatu.
La kwanza ningependa kuongelea ushiriki wa sekta binafsi hapa nchini na naomba ni-declare interest kwamba mimi ni mdau wa sekta binafsi. Serikali hii inaongelea kwamba uchumi huu injini yake ni sekta binafsi lakini Serikali hii haioneshi utatu ule unaotakiwa kwamba Serikali isaidie kuikuza kwanza na kuimarisha sekta binafsi ili yenyewe iwe injini kweli ya uchumi. Yapo mambo mengi, Serikali hii inaitoza kodi nyingi sana sekta binafsi, lakini ziko tozo ambazo hazina lazima kabisa. SDL tumeilalamikia kwa muda wa miaka mitano sasa kwamba ni kubwa kuliko kokote duniani. Asilimia 5 ya tozo ya SDL haina tija kwa waajiri ambao ndiyo waanzishaji wa ajira ambazo zitakuza uchumi. SDL wanasema inaenda kwenye VETA, kuna makampuni mengi hayana interest kabisa na VETA, hayatumii mafunzo ya VETA. Sekta ya ulinzi binafsi kwa mfano, hakuna kwata kule kwenye kozi ya VETA, u-nurse wanalipa hakuna kwata kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile yapo mambo mengine ambayo tunaona kwamba yanatubana sisi sekta binafsi. Ukitaka kuanzisha shughuli hapa Tanzania, utaenda nenda rudi, yanayosemwa kwamba BRELA wamepunguza ukiritimba si kweli. Wewe leo andika kwamba unataka kujua status ya kampuni yako, miezi sita na ukawaone watu mikononi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niongelee Sheria ya Kazi. Najua sana watu wengi tukiongelea Sheria ya Kazi wanaona kama ni jambo la Wizara ya Sheria lakini ndani ya Sheria ya Kazi yako mambo ambayo yanaleta chokochoko ya watu kudharau kuajiriwa. Watu wanafanya mpango wa kutokwenda kazini na huwezi kuwafukuza kazi kwa sababu sheria inakubana na ukimfukuza utaanza mambo mengi na Serikali. Tumeomba sisi waajiri tuweze kuruhusiwa kubadilisha sheria ile lakini lazima tupite kwenye ukiritimba wa Wizara ya Kazi na kule kuna Baraza la LESCO halikutani, kwa hiyo sekta binafsi inadumaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la kutokusikilizwa. Serikali inaamua mambo yake bila kufikiria utatu uliopo na ushoroba uliopo. Juzi hapa tumeshuhudia ndani ya Bunge lako sekta binafsi ya elimu imejieleza mpaka watu karibu walie humu ndani, Serikali imekaa na kujaribu kupanga ada elekezi bila kuwahusisha wahusika. Tunashukuru sana Serikali hii sikivu suala hilo limesitishwa na nafikiri watakapoanza kulifikiria tena wadau wote wa sekta ya elimu watakutana.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka niliongelee ni Sheria ya sasa ya Manunuzi. Hapa pia naomba ni-declare interest kwa sababu ni Mkandarasi Daraja la Kwanza. Sheria hii ya Manunuzi imeanzisha vitengo vinaitwa PMU katika kila mnunuzi wa umma. Mashirika haya baada ya kuanzishwa vitengo hivi yamekuwa na mpango wa kutengeneza bei wao wenyewe. Kwa hiyo, badala ya kufanya kazi vizuri na sheria hii imekuwa chanzo cha rushwa katika makampuni ya umma yanayonunua manunuzi ya umma, lakini vilevile yametajirisha watu binafsi badala ya Serikali kupata manufaa ambayo yalikusudiwa na sheria hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii imekuwa chanzo cha watu fulani kuingiza makandarasi kutoka nje kwa sababu wanataka kuhongwa dola. Pia wanataka safari za nje makampuni haya yakipewa tender wanataka kwenda kuangalia, wanasema wanafanya due diligence na huko ndiko wanapewa hela chungu mzima na imekuwa ndiyo kanuni. Kwa bahati mbaya sana nina mfano mzuri sana wa Shirika la Umma kubwa kabisa na naomba nilitaje kwa sababu nina ushahidi nalo. Benki Kuu ya Tanzania ndiyo shirika kubwa sana la umma linalovunja Sheria ya Manunuzi hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki hii au taasisi hii ya umma Mkurungenzi wake amefungwa jela miaka mitatu kuthibitisha kwamba kuna uvunjifu mkubwa wa Sheria ya Manunizi ya Umma. Pia hapa mkononi nina hukumu ya PPRA ambako Benki Kuu wameshindwa kesi miaka kumi iliyopita na bado wanataka kumpa yule yule aliyefutiwa tender na PPRA na wamefanya hivyo na wamempa. Mbaya zaidi wako wafanyakazi wa Benki Kuu wamefungua kampuni zao wenyewe na wanachukua zabuni za mwajiri wao Benki Kuu. Nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aniambie wafanyakazi hawa ambao wamefungua makampuni wanachukua zabuni za Benki Kuu na wao ni waajiriwa wa Benki Kuu amechukua hatua gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo haya kwa watu wasiojua yanaonekana kama ni mzaha mzaha, hela nyingi sana Benki Kuu zinatoka nje ya nchi kwa sababu makandarasi walioletwa pale wanatoka nje ya nchi na ingawa sheria inasema kama hela ya Tanzania zinatumika zote 100%, ifanyike local bidding. Benki Kuu wameweza kutengeneza njama ya kumtafuta mtaalam kutoka nje aka-specify mitambo inayofanya kazi pale kwamba lazima itoke kwenye kampuni moja fulani. Kampuni hii ndiyo ilishtakiwa miaka kumi iliyopita na kufungiwa na tender ikarudiwa lakini sasa huyo ndiye msemaji mkuu wa zabuni tena za usalama wa Benki Kuu. Mimi naomba atakapokuja Mheshimiwa Waziri alieleze suala hili la Benki Kuu na zabuni kupewa wafanyakazi wa Benki Kuu pamoja na watu waliochongwa kwa ajili ya kufanya kazi za siri za Benki Kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie na naunga mkono hoja hii asilimia mia kwa mia.