Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Mansoor Shanif Jamal

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MANSOOR S. HIRAN: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu. Naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Kwimba kwa kunichagua awamu ya pili na nawaahidi sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango kwa bajeti nzuri ambayo ameileta ya trilioni 29 na nusu; ambapo amepanga asilimia 40 itatumika kwenye miradi ya maendeleo. Nampongeza sana kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia kwenye maeneo matatu. La kwanza, nitachangia kwenye mchango wa Msajili wa Hazina kwa bajeti kuu. Kwenye kitabu cha volume one, kwa bajeti ya mwaka wa kesho amepangiwa atachangia trilioni 1.3. Msajili wa Hazina anasimamia Mashirika ya Umma na Taasisi mbalimbali ambazo zina makusanyo ya zaidi ya trilioni 10 kwa mwaka. Sasa kama mashirika haya umma yanakusanya zaidi ya trilioni kumi kwa mwaka, kutoa mchango wa trilioni 1.3 ni kidogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango aangalie upya hili suala jinsi ya kutoza na kukusanya fedha nyingi zaidi kutoka kwenye taasisi zilizo chini ya Msajili wa Hazina ili Msajili wa Hazina aweze kuchangia trilioni tatu au zaidi, kwenye mfuko wa bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye kitabu hiki cha Volume one tunacho hapa, ni kwamba bajeti ya mwaka huu wa 2015/2016, Airtel walichangia Shilingi bilioni moja lakini mwaka ujao Airtel hawatachangia chochote, sasa sijui ni makosa au kuna suala lingine, tunaomba Waziri aweze kutufafanulia hilo, kuna tatizo gani pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine; Tanzania Breweries mwaka huu wa bajeti wamechangia bilioni 5.7, lakini mwaka ujao hawachangii chochote, sasa sijui TBL hawatachanga, labda kuna makosa hapa, tungeweza kuelewa kuna tatizo gani pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukifika kwenye suala la Mashirika ya Umma; naomba niseme Shirika moja la Umma la Tanzania Ports Authority. Kwenye taarifa ya Msajili wa Hazina anasema mwaka huu, Mamlaka ya Bandari Tanzania haijachangia chochote wakati taarifa ya Mamlaka ya Bandari iliyoko kwa Msajili inasema mwaka huu wamechangia bilioni 150. Huyo huyo Msajili anasema hawajachangia chochote, huku bandari inasema wamechangia bilioni 150. Sasa ni muhimu tupate ufafanuzi, kwamba hizo fedha zimechangiwa zimekwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, mwaka huu huu tena Msajili wa Hazina amesema Mamlaka ya Bandari Tanzania haitachangia chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme masuala machache kuhusu bandari. Bandari hii, Tanzania Port Authority wana bajeti yao ambayo ipo mbele yangu hapa waliyoipeleka kwa Mhazini wa Serikali. Wanaonesha mapato na matumizi, naomba ku-declare interest mimi ni mjumbe kwenye Kamati ya Miundombinu. Mamlaka hii ya Bandari, mwaka jana, 2014 walipeleka shilingi bilioni 105 wakawela kwenye fixed deposit bank, wanasema ni pesa za ziada wanazitunza pale, huku hawachangii chochote. Mwaka wa jana wamepeleka bilioni 99 zimekwenda kwenye fixed deposit zinatunzwa pale wanakula riba, jumla ya Mamlaka ya Bandari Tanzania ina jumla ya bilioni 440, ziko kwenye mabenki hawana kazi nazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huku kwenye bajeti hizo fedha hazionekani, kwenye bajeti waliopeleka hawaoneshi kama kuna fedha ziko benki. Naomba Waziri wa Fedha afuatilie hili suala, kwamba huku hazionekani hizo fedha ziko wapi? Sasa hili ni Shirika moja nimelisema hapa, tuna Mashirika mengi sana, tunaomba CAG afanye kazi ya ziada, azikague tuangalie fedha ngapi ziko kwenye mabenki ambazo hazioneshwi kwenye ripoti. (Mkofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa kulichangia hapa ni Deni la Taifa. Kila mwaka deni la Taifa linakua, lakini taarifa tuliyoipata kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 16 ni paragraph moja tu.
Ningeomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha atupe taarifa ambayo ni pana, ya kina ili tujue kwamba fedha za madeni ambazo tunazitenga kila mwaka kwenye bajeti zinatumika vipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka ujao tumetenga trilioni nane kwa ajili ya madeni, mwaka jana pia tulitenga matrilioni ya fedha. Ni muhimu tupate taarifa ya hizo trilioni za fedha ambazo tunazipanga kwenye bajeti zinatumika vipi kwenye kulipa madeni ya nje na ndani, kwa sababu makandarasi na wazabuni wengi sana wa ndani wanalalamika hawajapata fedha. Ni muhimu tujue fedha zinatumika vipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kazi, ndani ya miezi mitano wamelipa wakandarasi wa barabara bilioni 698. Naomba walipe na wakandarasi wanaojenga miundombinu ya maji. Naomba maji pia yapewe kipaumbele, wapeleke fedha kwenye maji, wakandarasi wanalalamika sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo langu mradi mmoja wa maji umekaa unasubiri milioni 500, mabomba yamenunuliwa ya plastiki yapo juu yanasubiri kutandazwa chini, yanaoza yanapigwa jua lakini mkandarasi hajalipwa ili amalize huo mradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Deni la Taifa naomba Mheshimiwa Waziri atupe taarifa za kina zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa kulisemea hapa ni Kituo cha Biashara na Huduma Kurasini. Mheshimiwa Serukamba asubuhi alilisemea vizuri, naomba niongeze machache tu. La kwanza huu mradi hauelekweki unakwenda kwendaje. Mwaka juzi mwaka 2014 wakati nilipokuwa mjumbe kwenye Kamati ya Bajeti tulienda kwenye ziara pale kwenye mradi tukaenda kuangalia pale Kurasini hatukuelewa. Tuliomba tupate taarifa ya mkataba ambao wamefunga na yule mbia lakini haujapatikana mpaka leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Waziri wa Viwanda na Biashara aliangalie hili suala kwa undani zaidi, kwa sababu sisi Tanzania hatutaki Mchina aje kufanya biashara hapa ya kuuza vitu kwenye maduka. Hiyo kazi tunaweza kuifanya sisi Kariakoo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hii miradi inaonekana kuna tatizo sisi tumeshawekeza bilioni 100 kwenye fidia, sasa huyo atakapokuja kuwekeza pale lazima sisi kama Serikali tuwe na share kwenye kampuni hiyo, hatuwezi kuwekeza halafu tukamwachia yeye akafanya peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kwa taarifa niliyoipata 2014 wakasema wana mpango wa kuleta vifaa kutoka China na kuanza kuuza Afrika Mashariki na kati. Sasa wale watu wanataka kuanzisha shughuli kama ya Dubai. Unapokwenda Dubai unakutana na dragon mart Dubai pale watu wengi wanaifahamu. Wachina wanakaa sehemu moja wanauza vifaa vyao vyote pale, sasa lile suala sisi hapa Tanzania hatulitaki wale wakija hapa Kariakoo itafungwa na wakija hapa watatumaliza kabisa biashara itakuwa hovyo. Kwa hiyo, naomba hili suala liangaliwe upya. Kwanza huyu mwekezaji bado hajaleta chochote hapa kwa hiyo hatujachelewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine walisema wanataka kuwekeza kwenye viwanda. Ushauri wangu kama wanataka kuwekeza kwenye viwanda basi wawekeze kwenye viwanda ambavyo sisi hapa nchini hatuna, wasije wakatuwekea viwanda vya biskuti wakati tunavyo wenyewe viwanda vyetu. Waweke viwanda ambavyo sisi Tanzania tuna shida navyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.