Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mahali popote panapohitaji kupongeza isomeke kwamba nimepongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kulisema hilo, naomba nianze na suala zima la vyanzo vipya vya mapato. Nimeipitia hii taarifa ya Kamati ukurasa wa kwanza, nanukuu, imesema hivi, bado Kamati imebaini kuwa Serikali haijaonyesha utayari wa kupokea ushauri hususani eneo la ukusanyaji wa mapato kwa kutumia vyanzo vipya, ni taarifa ya Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, habari ya bia na soda kabla sijazaliwa, nimezaliwa, nimekua, nimesoma ukisikiliza vyanzo vya mapato ni hivyo hivyo hatuwezi tukaja na vyanzo vipya, hatuwezi tukabuni vyanzo vipya! Nchi yetu nzuri ya Tanzania uwepo wake tu wa kijiografia ambao ametujaalia Mwenyezi Mungu hicho ni chanzo namba moja cha mapato. Uwepo wa hapo Tanzania ilipo nasema ni chanzo kikubwa cha mapato. Niwaombe wataalamu wetu katika eneo hilo waangalie suala hili tuna bandari, utalii, ukiniuliza nashangaa kwa nini soda na bia mpaka leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna nchi nyingine utaambiwa chanzo chake cha mapato labda ni suala la maua tu, kuna nchi nyingine chanzo chake cha mapato ni fukwe na kuna nchi nyingine chanzo chake cha mapato ni madini. Sasa turudi kwa Tanzania yetu mbuga tunazo, wanyama tunao, maua tunayo, fukwe tunazo, bandari nzuri tunazo tumekosea wapi, tunashindwa wapi? Niseme tutakuwa tunamsingizia Mwenyezi Mungu kwamba labda Mungu hajatusaidia ametupa fursa zote hizo tunashindwa wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri wasomi wetu tunao, kwa nini tusitumie nafasi hii ya kijiografia? Ndiyo maana watu wengine walikuwa wanasema wangebahatika kuwa hapa Tanzania wangefanya maajabu. Kwa hiyo, niwaombe wataalamu ambao wamepewa dhamana na Watanzania hebu watusaidie kuitoa Tanzania hapo ilipo kwa maana ya kuibua vyanzo vipya vya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo la vyanzo vya mapato amani hii na utulivu ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia, hali nzuri ya hewa ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia kwa nini tusivitumie kama fursa nzuri? Hayo tu tukiyafanyia kazi wala tusingekuwa na sababu hapa ya kuumizana vichwa kuhusu habari ya kiinua mgongo cha Wabunge na mambo mengine ya namna hiyo kwa sababu vyanzo vipo na ni vingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taarifa inatuonyesha kwamba Pato la Taifa limeongezeka kutoka 7.0 mpaka 7.2. Wananchi wetu wa kawaida ukiongelea habari ya ongezeko la pato wao wanatamani waone kwa macho na washike kwa mikono yao hilo ongezeko. Habari ya ongezeko la pato kwa kupitia maandishi kama hali ya mfuko wake ni korofi hawaipati sura hiyo. Tunasema kwamba nchi yetu tumepiga hatua kwa maana ya ongezeko ya Pato la Taifa basi uchumi usomeke kwenye mifuko ya watu, uchumi usomeke kwa yale wanayoweza wakayaona ndiyo tutakuwa na jambo la kuongea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji, napata tabu sana ukirudi hata katika ramani iwe ni ramani ya East Africa ama ya dunia Tanzania yetu imezungukwa na maji nchi nzima kuna Lake Tanganyika, Lake Victoria, Lake Nyasa lakini hata Bahari ya Hindi. Kuna nchi nyingine wanafanya kazi kubwa ya kuyabadilisha maji ya bahari kuwa maji ya kunywa Tanzania hatujafika hapo. Mimi nilikuwa natamani ule mtandao wa buibui jinsi ulivyo Tanzania hii ingeweza kuunganishwa kwa maji kwa sura hiyo. Maji yangeweza kuvutwa kutoka Lake Victoria yakafika upande mwingine, yakavutwa kutoka Lake Tanganyika yakafika upande mwingine na yakatoka Lake Rukwa yakafika upande mwingine. Leo kuendelea kuongelea habari ya maji kwa nchi ambayo imezungukwa na maji sipati picha, vipi hawa watu wengine ambao hawakupata baraka hii ya kuwa na maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitembelea nchi moja wale watu pamoja na kwamba wanapata mvua mara moja ndani ya miaka mitatu wameweza kutengeneza ziwa (man made lake). Huwezi kuamini ni kubwa linawasaidia kupata maji lakini kufanya utalii kwa sababu wanaenda watu pale kufanya utalii wanapata samaki lakini huku chini wanaweza kumwagilia pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa Tanzania hii mimi narudi kwenye maandiko hivi ni nani ameturoga? Ukiangalia jiografia maeneo mengine jinsi milima ilivyokaa wala hauhitaji kufanya kazi kubwa ya kusema sijui utachimba bwawa ni suala la kukinga tu na wataalamu tunao. Ukishakinga hapo unatengeneza mazingira ya kuwa na maji ya kutosha, hatujafika mahali pa kulalamika suala la maji hebu tubadilike tuache kufanya kazi kwa mazoea. Tusiogope kuthubutu kuja na miradi mikubwa ambayo itakuwa ni ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu, tusifanye kazi kwa mazoea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoke hapo nizungumzie kuhusu msamaha wa kodi kwa wanajeshi wetu. Jambo hili linaweza likawa jema lakini naomba niwakumbushe wapo wadau wengine kama askari wastaafu wale nao tunafanyaje ambao walikuwa ni wanufaika wa suala hili? Naomba wakati tukiliangalia hilo nao tusiwasahau. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la CAG halikwepeki, ni vizuri akaongezewa fedha. Nikirudi TAKUKURU kama ilivyo neno lenyewe ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa hiyo, si muda wote wanapambana kuna wakati mwingine wanazuia. Kwa hiyo, katika suala la kuzuia wanahitaji fedha, naomba nao wafikiriwe. Lakini baada ya kutoka hapo, naomba nizungumzie suala moja. Nafahamu nafasi ya Watanzania walioko nchi za nje tunafanyaje kwa maana ya ndugu zetu hawa kurudisha mapato nyumbani? Naomba nalo hilo tuendelee kuliangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati tukiwa tunaongelea mipango mipana niseme jambo moja, ukienda nchi za watu utakuta vijana wengi wa kutoka Kenya wanafanya kazi huko wanatumia hata nafasi ya Kiswahili kufanya mambo makubwa katika nchi nyingine. Sisi kama Watanzania nafasi ya Kiswahili tunaitumiaje? Kuna sehemu tumesema tufanye kwa makusudi kuhakikisha watu wanakwenda nje wakitumia nafasi hii ya Kiswahili na kwa kuwa huko nje wana uwezo wa kuzalisha na kurudisha fedha ndani, hilo tumejaribu kulifanya?
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.