Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Vilevile namshukuru Mungu kwa kuweza kunipa afya bora na kuweza kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu kuchangia hotuba hii ya bajeti kuu ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuzungumzia suala la afya, nasikitika kusema kwamba sijaona mkakati mahsusi wa kujenga zahanati pamoja na vituo vya afya. Tuko katika mkakati wa kuhakikisha kwamba tunapunguza vifo vya akinamama wajawazito. Najiuliza tunawezaje kupambana na vita hii ilhali hatuna facilities za kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivi? Katika bajeti hii nimeona Hospitali za Mikoa ndiyo ziko chini ya Wizara lakini kiuhalisia watu wengi wapo kwenye Kata na kwenye Halmashauri zetu. Watu waliokuwa kwenye Kata, kwenye vijiji vyetu macho yao yanakuwa yanatazama zahanati zao na vituo vyao vya afya ambavyo viko kwenye Kata na kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua Kanuni ya 106 inasema kwamba Mbunge hataruhusiwa kupendekeza mabadiliko yoyote katika makadirio na mapato ya bajeti ya Serikali, lakini naiomba Serikali kwa bajeti inayokuja iweze kuliangalia vizuri suala la zahanati na vituo vya afya viwekwe katika Serikali Kuu ili tuweze kuviboresha na kuvijenga kwa ufanisi mkubwa ili kuweza kutatua tatizo lile la vifo vya akinamama wajawazito ambapo wengi wao wako kwenye Kata huko kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niishauri Serikali, ni vyema kuweka pesa nyingi katika Mfuko wa Maji kwa sababu tatizo la maji ni kubwa sana Tanzania na anayeteseka katika matatizo ya maji ni sisi wanawake. Akinamama wa mkoani kwangu kule, akinamama wa Kata za Saja, Kijombe, Wanging‟ombe, Mkongobaki, Nkomang‟ombe, Ludewa Mjini, Ludewa Vijijini pamoja na Njombe Mjini kuna shida sana ya maji kwa muda wa miaka mingi. Ni vyema Serikali itambue umuhimu mkubwa wa kuweka pesa nyingi katika Mfuko wa Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, naomba nizungumzie suala la utalii. Wenzetu wa Kenya wametoa kodi katika suala la utalii lakini sisi Watanzania tumeamua kuweka kodi katika suala la utalii. Kiuhalisia sisi Tanzania mshindani wetu mkubwa katika suala la utalii ni Mkenya. Wenzetu Wakenya wana ndege ya moja kwa moja kutoka Europe na America kwenda Kenya na mtalii anapotumia ndege hiyo anapata ahueni ya pesa katika tiketi karibu asilimia 45 ya air ticket. Hiyo ni advantage kwa wenzetu wa Kenya kwa sababu watalii wengi watakuwa wanataka kwenda Kenya kwa ajili ya ku-save hizo costs za air ticket na mambo mengine. Kabla hatujaweka asilimia 18 bado utalii wetu wa Tanzania ulikuwa wa gharama kubwa ukilinganisha na wa Kenya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mtalii kabla hajaamua kuja vocation huwa analipa in advance, mwaka mmoja kabla au miaka miwili kabla. Kwa kuweka kodi hii kutatokea usumbufu kwa wale watalii ambao tayari walishalipa hela zao kuja kutalii kwa mwaka huu wa fedha 2015/2016 na ikiwezekana 2017. Kwa mkanganyiko huo, kuna uwezekano mkubwa wa watalii wengi kuahirisha na kutaka pesa zao warudishiwe kwa sababu wanaona kwamba mimi nilishajipanga bajeti yangu ya vocation ni kiasi hiki na sasa hivi naambiwa kwamba niongeze asilimia 18 ya pesa ambayo ilikuwa haiko kwenye bajeti yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara iangalie suala hili la utalii katika masuala mazima ya ushindani wa utalii baina yetu sisi na watu wa Kenya, huenda tukasababisha watalii wengi waache kuja Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ile wanaita msafara wa nyumbu wanaokuwa wanazunguka Kenya na Tanzania, migration ya wanyama. Nina wasiwasi wanaweza watalii hawa wakawa wanasubiri wanyama wakifika Kenya ndio waende badala ya kuja kuangalia kwetu Tanzania wakati sisi tuna advantage kubwa wakati wanyama wanasafiri miezi ya saba ndiyo kipindi ambacho nchi nyingi za Ulaya wanakuwa wako kwenye holiday na wanatumia muda huo kuja kutalii Tanzania. Naomba Serikali iangalie ili tusiweze kupoteza mapato katika suala la utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika bajeti zilizopita imeonesha kabisa kwamba utalii unachangia asilimia 25 ya mapato ya Tanzania. Kwa nini leo tuisumbue sekta hii na twende katika kushusha mapato hayo? Naomba Serikali iangalie kwa umakini kwa sababu asilimia 25 ya kuchangia kwenye mapato ni asilimia kubwa sana, tuiangalie kwa umuhimu wa kipekee ikiwezekana hii kodi tuitoe ili tusiweze kukosa watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nizungumzie suala la kiinua mgongo. Najua Serikali ina dhamira njema ya kuongeza mapato katika bajeti yetu, lakini nashangaa katika category ya watu tisa akiwemo Makamu wa Rais, Prime Minister, Chief Justice, High Court Judges, Maspika, Supreme Court Judges, Regional Commissioners na hawa Wakuu wa Wilaya, kwa nini wame-single out Mbunge tu ndiyo akatwe kodi ya kiinua mgongo ilhali katika hilo group hao watu wote nao wanatakiwa waingizwe kwenye kukatwa makato haya. Kama kweli Serikali ina nia ya dhati na hawa watu wengine wote wakatwe au labda kama kuna kitu kimejificha tunaomba Wabunge tukijue hicho kitu ni kitu gani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge tuna mzigo mkubwa, Wabunge tunahudumia watu wengi huko vijijini kwa hela hiyo hiyo, Wabunge tunapeleka watu hospitalini, tunahudumia misiba, harusi, wagonjwa, kwa kipindi hiki cha Ramadhani Wabunge ndiyo hao hao ambao wanasaidia kule watu wengine ambao hawajiwezi katika masuala mazima ya kuhakikisha kwamba wanafuturu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iwaangalie Wabunge kwa jicho la huruma na hatuna nia mbaya kwamba hatutaki kuchangia mapato kwa sababu katika mishahara yetu tunakatwa kodi. Naomba sasa watuangalie na sisi ili tujue ni jinsi gani ya kurudi humu ndani na tuendelee kuwahudumia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.