Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

WAZIRI W A MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali yote nakushukuru wewe mwenyewe binafsi, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote wa pande zote mbili kwa michango ambayo wametupa. Nataka nitoe ahadi kwamba michango yote mlioyoitoa kwa kuongea humu ndani na mliyoleta kwa maandishi, tutaijibu na tutawapa bango kitita cha maelezo yote kwa kina.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwape imani kwamba ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, Wizara hii inaongozwa na wahandisi; kuanzia Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, wote ni wahandisi waliosajiliwa. Nina hakika kabisa haya mawazo yote mliyotoa Waheshimiwa Wabunge, tutakwenda kuyafanyia kazi ili kuhakikisha kwamba nchi yetu matatizo ya maji tunakwenda kuyafikisha mahali ambapo ni salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna Serikali yoyote ambayo inapenda kutawala, halafu wananchi wake hawana maji. Kwa hiyo, kwa Serikali ya Awamu ya Tano, maji ni kipaumbele kimojawapo. Mheshimiwa Rais wetu kila mahali alipokwenda kuomba kura, aliahidi kwamba suala la maji nakwenda kulishughulikia kwa nguvu zote. (Makofi)
Ndugu zangu, tuna miezi sita tangu tumeingia madarakani na toka Mheshimiwa Rais, Magufuli ameingia madarakani, sasa fedha zimeanza kupatikana na tumeanza kuzipeleka kwenda kwenye Halmashauri zote. Kwenye Mfuko wa Maji zilikuwa zimetengwa shilingi bilioni 90, lakini mpaka leo tumeshapeleka zaidi ya shilingi bilioni 107 kwenye Halmashauri. Hii inaonesha kabisa kwamba kuna nia ya dhati na ya kweli kwamba tunakwenda kumaliza matatizo ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu tunasema ikifika mwaka 2020 lazima tuhakikishe wananchi wetu wote wanaoishi vijijini, wanapata maji kwa kiwango cha asilimia 85 na wanaokaa mijini wanapata kwa kiwango cha asilimia 90. Kwa hiyo, kazi tumeshaianza. Naomba ndugu zangu mtuamini, tutakwenda kutekeleza jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kambi ya Upinzani na Kamati ya Bunge wote wameshauri kwamba tuongeze uwezo wa Wizara hii kufanya miradi zaidi. Katika kuongeza uwezo, kimojawapo ni lazima tuongeze rasilimali fedha. Kwa hiyo, mapendekezo yaliyotolewa kwa kambi zote mbili kwamba tupanue wigo wa Mfuko wa Maji; kama tunaweza kukubaliana kwamba tu-ring fence Mfuko wa Maji, tuna hakika kabisa tutafanya miradi mingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema Naibu Waziri, Programu ya Awamu ya Kwanza ya WSDP, tulikuwa na miradi 1,800; mpaka sasa tumekamilisha miradi 1,200. Kwa maana kwamba WSDP tumekuwa na mafaniko ya asilimia 62, hiyo ndiyo iliyofikisha kupata asilimia 65 ya wananchi wanaokaa vijijini. Tumepata asilimia 68 kwa maana ya wastani wa programu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la data, mtu unaweza ukasema kwanini unasema 68 wakati eneo lingine wako 40? Ni kweli data hizi tumechukua wastani kinchi; na data ina-base kwa population siyo kwa namba ya vijiji. Maana mmoja anasema mimi nina vijiji kumi vimepata maji, lakini vijiji 90 havina maji, kwa maana havikupata maji kwa programu hii ya WSDP; lakini kuna mipango mingine ambayo ilikuwa inaendelea sambamba na mradi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na miradi ya Water AID, watu wa UNICEF miradi mingi imekuwa inaendelea ambao hawakuwa wameingia kwenye programu. Kwa hiyo, tunaposema mafanikio haya, tuna base na population.
Kwa hiyo, inaweza kuwa ni vijiji vitatu, lakini ndiyo vyenye watu wengi zaidi. Data hizi zimetoka huko kwenye Halmashauri, sisi tumefanya compilation. Huu mradi unatekelezwa na watekelezaji zaidi ya 100 kwa sababu Halmashauri zetu sasa hivi ziko 181, Halmashauri tu peke yake! Bado kuna taasisi nyingine ambazo zinaendelea kutekeleza mradi huu. Kwa hiyo, kila Wilaya katika mwaka huu tumezingatia na kuhakikisha kila Halmashauri ya Wilaya tunaipa fedha za kutekeleza programu.
Mheshimiwa Naibu Spika, waliosema wanataka kutekeleza vijiji gani, imetoka huko kwenye Halmashauri, ndiyo walioleta vipaumbele Wizarani tukachuja. Kulingana na ceiling tukasema basi anza na vijiji hivi; lakini tukipanua wigo, tutaendelea na vijiji vingine. Kwa hiyo, naomba msiwe na shaka kwamba mbona nimepewa hela kidogo? Hapana, tumepewa fedha za kutosha. Hata mimi nasema fedha tulizopewa na tulizotengewa zinatosha. Lazima tuoneshe kwamba katika hizi tulizopata tunaweza kufanya kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niseme kwa kifupi kuhusu hii programu. Sasa hivi kuanzia Januari, tumeanza kutekeleza programu ya awamu ya pili. Washirika wa maendeleo wakiwepo Benki ya Dunia, African Development Bank, KfW na wengine wameahidi kwamba kwenye programu ya pili watatoa dola bilioni 3.3 ambazo ni karibu trilioni saba kwenye programu ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunauhakika kabisa katika miaka mitano ijayo tutafikisha hizi asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini, kwa sababu tayari wapo Washirika wa Maendeleo pamoja na Serikali. Kwa hiyo, duty yetu ni kuwahamasisha wananchi kweli tuweze kupata makusanyo ya kutosha, fedha hizi ziweze kuingia kwenye mfuko wa maji ili tuweze kutekeleza miradi mingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wafadhili pia wameanza kuwa wazito, wanapoona Serikali hatuchangii kwa kiwango kikubwa, basi na wao vilevile wanakuwa wazito kuchangia. Kwa hiyo, kama Serikali tutaonesha kabisa direction kwamba lazima tuweke fedha ambazo zimetengwa ziende kwenye maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea ushauri kambi zote mbili kwamba tuanzishe Wakala wa Maji Vijijini (Rural Water Agency). (Makofi)
Sasa hili kwenye suala la sustainability au uendelevu; tumesema miradi ya maji ili iweze kuwa endelevu, tumekuwa tunawatumia hawa water users, wale watumia maji. Serikali ikishajenga mradi, tumekuwa tunakabidhi kwa watumia maji kuendesha mradi ule ili kusudi mradi uwe endelevu na uweze kutoa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi tumefanikiwa, lakini yapo maeneo ambayo bado kuna matatizo ya hizi Water Users Associations. Tumeendelea kutoa mafunzo, lakini pale tukianzisha Rural Water Agency nina hakika uendelevu wake utakuwa unafanana kutoka Wilaya moja kwenda Wilaya nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jambo hili tunalipokea, ni zuri. Wizara yangu itaanza kuandaa cabinet paper, tutapeleka kwenye Baraza la Mawaziri, tutaangalia namna gani tunaweza kuanzisha hii Rural Water Agency ili itusaidie kufanya miradi yote hii iwe endelevu. Kwa sababu itakuwa haina maana unajenga mradi, baada ya siku mbili mradi ule unakuwa hautoi maji; na inawezekana hautoi maji kwa sababu ya kitu kidogo tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika miradi ya maji, tofauti na kujenga barabara; unaweza kuwa na mradi wa barabara wa kilometa 100 ukajenga kilometa 50, unaweza kuendelea kutumia kilometa 50; lakini mradi wa maji ni lazima umalize mpaka mita ya mwisho. Lazima maji yafike kwenye tanki ndiyo yanaweza kutoka. Kwa hiyo, miradi ya maji ni lazima ikamilike kwa namna inavyotakiwa. Huwezi kusema partial completion. Kwa hiyo, ndiyo tofauti ya miradi ya maji na barabara au ya kujenga nyumba au na vitu vingine. Kwa hiyo, tutazingatia na nina hakika tukiwa na Rural Water Agency, miradi yetu itakuwa endelevu kwa sababu tutakuwa na norms ambazo zinafanana kutoka mradi mmoja mpaka mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la Mfuko wa Maji, bajeti iliyotangulia ya 2015/2016 tulikuwa tumetengewa shilingi bilioni 90. Performance yake imekuwa nzuri kwa sababu hizi fedha ni ring fenced, Wizara ya Fedha imeweza kutupa zaidi ya hizi shilingi bilioni 90 kwa sababu ndivyo walivyokusanya. Kwa hiyo, naamini kabisa tukipanua wigo zikapatikana zaidi ya shilingi bilioni 90 tutafanya miradi mingi zaidi kama nilivyosema toka awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kidogo kuhusu miradi mikubwa ambayo tunayo. Kwanza kuna maombi mengi ya watu kutaka kupata maji ya Ziwa Victoria. Sasa miradi mikubwa ya Ziwa Victoria ambayo tunayo ni kama sita; tuna mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Tabora, Nzega, Uyui, Sikonge, Igunga na vijiji 89 ambavyo vipo kando kando ya zile kilometa 12.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Munde ametaka kujua action plan. Ni kweli mradi huu tumeuzungumza muda mrefu, lakini Serikali imeshapata mafanikio; tumeshapata fedha kiasi cha shilingi bilioni 536 kutoka Exim Bank ya India. Mkataba wa fedha hii umeshasainiwa na tayari pre-qualification tumeshaikamilisha. Ni kwamba sasa kazi haiwezi kuanza mpaka wenzetu kwa utaratibu wa mfadhili aseme, ndiyo endelea (no objection), ndicho kinachosubiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kazi zote tumefanya. Atakaposema no objection endelea, tunaanza kusaini mkataba na makandarasi, wanajaza zile tender, tunaendelea kufanya kazi. Kwa hiyo, ninaamini kabisa Serikali ya India itakwenda kutoa no objection kwa namna tulivyokuwa tumekubaliana. Na mimi nitafuatilia kuhakikisha kwamba kazi hii ambayo tumewaahidi Watanzania kwa muda mrefu hasa wa Kanda ya Tabora, Nzega, Igunga na Uyui kwamba huu mradi sasa unakwenda kuanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi mwingine ambao wameusema kwa maandishi na kwa nguvu sana ni Mradi wa Lake Victoria kwenda Sumve, Malya, Malampaka, Kwimba, unaweza kuipata kwenye ukurasa 126. Mradi huu tumewapa fedha ya kuanza kufanya usanifu maana huwezi ukajenga mradi kama hujafanya usanifu. Kwa hiyo, tumeshaweka fedha, ina maana Serikali imeshakubali kuutekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi mwingine wa Ziwa Victoria ni unaokwenda Busega, Bariadi, Langabilili, Mwanhunzi. Mradi huu tumeutengea shilingi bilioni tano. Kwa hiyo, tayari kuna commitment ya kuanza kutekeleza mradi huu. Kuna mradi mwingine wa kupeleka maji kwenda Isaka, Tinde na Kagongwa, nao tumeshautengea fedha na kwenye randama mtauona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi mwingine kutoka Ziwa Victoria kwenda Mwanza, Bukoba, Misungwi na Magu. Tayari tumepata mkopo kutoka European Investment Bank na sasa hivi tupo kwenye tendering stage ili kuweza kupata makandarasi na tuweze kuanza kujenga mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna miradi mingi kwa ajili ya Mradi wa Makonde, Mheshimiwa Mkuchika amesema kwa uchungu sana. Kama Senior Member of Parliament naomba nikuhakikishie mradi huu tunakwenda kuukarabati. Ni mradi wa siku nyingi, ni mradi muhimu, ninaamini kabisa kwa mpango ambao tumeuweka, ukiangalia kwenye randama tumewaka kwenye miji 17 ambayo tayari tumeahidiwa na Serikali ya India kupata dola milioni 500 ambazo ni karibu trilioni moja. Sasa tumeona huu mradi kwa sababu utahitaji fedha nyingi tumeuwekea katika hii miji 17 pamoja na miradi mitatu ya Kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo mradi huu umewekwa kwenye mpango mzuri, Mheshimiwa Mkuchika, naomba kabisa waambie wapiga kura wako kwamba Serikali inakwenda kutekeleza mradi huu. Angalizo lako kwamba wale waendeshaji wa mradi wanapeleka maji kwa watu wanaofanya biashara, nimeshawaambia kuanzia sasa hiyo biashara waache. Kwa hiyo, hawataendelea kufanya kazi hiyo, vinginevyo nakwenda kuwakamua majipu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza katika Mradi wa WSDP kuna suala la kuchagua tutumie teknolojia gani? Pale mwanzo tulipoanza, sehemu kubwa ya miradi hii walichagua kutumia visima kwa sababu visima ilikuwa ni technolojia rahisi na namna ya kuiendesha imekuwa rahisi. Kwa hiyo, michango ya Waheshimiwa Wabunge wengi, wameacha kutaka kuwa na teknolojia ya visima. Kwa hiyo, kila mahali kama kuna mto, wanataka tuchukue maji Tabora kutoka Mto Malagarasi; Bukoba wanataka tuchukue maji kutoka Mto Kagera, likewise wa Lake Victoria, likewise wa Ziwa Nyasa wote wangetaka tuchukue miradi kutoka kwenye maeneo kama hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua mradi kwa mfano huu wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Kahama na Shinyanga, mradi huu umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 250, huu ni mradi mmoja. Sasa ukichukulia bajeti ambayo inatolewa kwa mwaka ya shilingi bilioni labda 400, sasa ukipeleka mradi mmoja ina maana utakuwa umefanya kazi moja. Ndiyo maana tulifikiria tuanze kwanza na kutatua hili suala la kutumia visima ili tuwe na miradi midogo midogo ambayo tunaweza tukai-spread kwenye nchi. Sasa baada ya kufanya vile na kuona maeneo mengine kwa sababu ya tabia nchi, suala la visima imeonekana havipo sustainable, yaani havina uendelevu. Baada ya miaka miwili, mitatu unakuta kisima kile kilikuwa kinatoa maji, maji yanapungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumeona tutaanza kufanya usanifu, kubadilisha yale maeneo ambayo angalau kuna mabwawa na sasa hivi nahimiza kwamba Serikali itaanza kujenga mabwawa makubwa ili iwe ndiyo source ya kutawanya maji kwa watu wengi kwa muda mfupi na kwa nguvu ya Serikali ya Awamu ya Tano jinsi tunavyokwenda, naamini kabisa jambo hili tunaweza kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana tushirikiane Waheshimiwa Wabunge kwamba sasa tuanze kuangalia uwezekano wa kuvuna maji ya mvua, tuongeze reservers, tuongeze upatikanaji wa maji kwa kuwa na mabwawa mengi zaidi. Haya mabwawa yanaweza yakawa ni kwa watu kutumia maji lakini pia yanaweza kutumika kwa mifugo na pia tunaweza tukatumia kwa kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, ni kitu ambacho ni endelevu. Tukifanya kwa muda wa miaka mitano ijayo tutakuwa kabisa tuna uhakika na chakula cha kutosha na tutakuwa hatuna njaa. Hata yale maeneo ambayo ni kame, wakishakuwa na mabwawa haya, nina hakika tutakuwa hatuna tatizo la chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumeshashauri na kuelekeza Halmashauri watunge sheria ndogo ndogo hasa kwenye shule, kwenye zahanati, lazima tu-design kuvuna maji ya mvua ili tupunguze magonjwa yanayoambukiza kwenye shule zetu zote. Tukiwa na matenki na tukavuna maji, watoto watafundishwa kunawa mikono; nina hakika tutapunguza kwa kiasi kikubwa magonjwa yanayoambikizwa kama kuhara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Zitto kwamba kuna mradi wa umwagiliaji maeneo ya Lwiche na kwamba alikuwa halioni kwenye randama. Naomba nimwambie kwamba jambo hilo lipo na kwenye randama ipo, Serikali inakwenda kufanya kwanza feasibility study na usanifu wa mradi, ndiyo condition ya wafadhili ambao ni Kuwait Fund. Wanazo fedha US Dollar milioni 15, lakini wanasema Serikali ifanye na Serikali tumeweka fedha za kufanya usanifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia alikuwa na hoja kuhusu mradi wa Kigoma kwamba tunachukua hatua gani? Ni kweli mradi wa Kigoma umechelewa kukamilika, lakini mpaka sasa tumechukua hatua ya kumkata tozo kwenye mkataba ule. Mkataba ulikuwa uishe Machi, 2015 kwa hiyo, umeshachelewa; lakini kulingana na mkataba jinsi tulivyokubaliana, mkandarasi akichelewesha mradi, kuna kitu kinaitwa liquidated damages, maana yake ni tozo kwa kuchelewesha. Uzuri wa mradi ule ni kwamba vifaa vyote vinavyohitajika na Mkandarasi vipo Kigoma. Kazi ina progress karibu asilimia 60. Kwa sababu kila kitu kipo, tumeshambana mkandarasi kwamba ikifika mwezi wa kumi atakuwa amekabidhi mradi. Kwa hiyo, mradi utakamilika mwezi wa kumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kusimamisha mkataba utake kutafuta mkandarasi mwingine, kwanza tutapata matatizo mawili. Huu mradi ni wa mfadhili, ukisha-terminate contract, mfadhili anajitoa. Kwa hiyo, itabidi tutafute hela. Sasa kama hatukuweka fedha kwenye bajeti, ina maana mradi utazidi kuchelewa. Kwa hiyo, ni vizuri aendelee kukatwa liquidated damages lakini akamilishe mradi, na sisi tutaendelea kumbana na kuweza kusimamia kuhakikisha anamaliza kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na hoja za baadhi ya Waheshimiwa kuhusu miradi ya maji Dar es Salaam. Kama nilivyosema sasa hivi Dar es Salaam tumeshakuwa na maji yanayozalishwa kutoka kwenye mitambo ya Ruvu Chini na Ruvu Juu yanatosheleza kwa mahitaji ya sasa. Tatizo tulilokuwanalo ni ule mtawanyiko (distribution) na sasa hivi Dar es Salaam watu wamepanua sana kuliko ilivyokuwa mwanzo. Kwa hiyo, watu wapo maeneo mengi ambayo hayana mtandao. Serikali tumeshaanza kushughulikia suala la mtandao wa mabomba ili maji haya ambayo tayari yanazalishwa yaweze kuwafikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi hata katikati ya Jiji la Dar es Salaam hapo nyuma kulikuwa hakuna maji, lakini leo maji yapo na mabomba yanapasuka. Tatizo letu ni kwamba miundombinu ni ya siku nyingi sana, kwa hiyo, tunaikarabati na tunajenga miundombinu mipya ili maeneo yote ambayo hayana maji tuweze kuhakiksha kwamba yanapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, wengine wameongelea suala la maji machafu, ni kweli. Tulisema ngoja kwanza tuweke nguvu kwenye upatikanaji wa maji safi na salama. Haya maji ninavyozungumza yanawekewa dawa, yanachujwa. Ndiyo tumeweka nguvu na yamepatikana. Ukizalisha maji mengi zaidi lazima utazalisha pia maji machafu. Tunao mpango wa kuboresha huduma ya maji machafu kutoka asilimia 10 mpaka asilimia 30.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Korea Kusini wameshatuahidi kutupatia dola milioni 89 kwa ajili ya kuanza kutengeneza mitambo ya kuchuja maji machafu. Kwa sasa tumekuwa tunapeeleka maji baharini lakini hii siyo sawasawa. Inatakiwa maji machafu yaingizwe kwenye mtambo yaweze kusafishwa. Maji haya pia tutayatumia kwa baadhi ya kilimo na baadhi ya viwanda kwenye cooling, kwa mfano, Kinyerezi tunatumia maji ambayo yameshapitiwa au wanaita recycling; umeshayazungusha kutoka uchafu na kuja kwenye maji safi; lakini yatatumika kwa ajili ya viwanda. Yale maji yanayotoka Ruvu yatatumia watu kwa ajili ya kunywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maeneo ambayo hayana mtandao, kwa mfano, wengi wamezungumza habari ya maji kutoka Mto Rufiji, Mheshimiwa Naibu Waziri ameelezea vizuri. Jambo hili ni kweli, tungeweza kupata maji yale yangeweza kufika kwa watu wengi zaidi. Kilichotukwamisha mwanzoni ilikuwa ni makubaliano ya teknolojia ya kutumia na vilevile fedha ambazo zingehitajika kwa miradi kama hii, inakuwa ni nyingi. Kwa hiyo, tutaendelea kulishughulikia, kama nilivyosema tutafanya usanifu na kuweza kuongeza. Tukichukua maji ya Rufiji na maji ya Kimbiji na maji ya Ruvu, tunahakikisha kabisa hata hili suala la kuwa na viwanda, kwa sababu kweli huwezi kuwa na viwanda endelevu kama huna maji. Kwa hiyo, lazima tutahakikisha kwamba maji yanapatikana kwa ajili ya kuhakikisha nchi yetu inakuwa na viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, watafiti wanasema ukiwekaza dola moja kwenye maji ina maana inazalisha dola tano kwenye uchumi. Kwa hiyo, ni jambo la msingi sana, tutahakikisha kwamba tunawekeza kwa nguvu zote kwenye suala hili la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mradi mwingine wameulizia kuhusu mradi wa Manispaa ya Lindi. Ni kweli tumekuwa na mradi ambao pia umecheleweshwa, ni katika miji ile saba ambayo imefadhiliwa na Benki ya Ulaya. Huu mradi utakamilika ikifika mwezi wa nane mwaka huu. Naye mkandarasi pia tumeanza kumkata tozo kwa kuchelewesha. Kwa hiyo, inakuwa kwa mkandarasi ni hasara kama ataendelea kuchelewa zaidi, kwa sababu ataendelea kukatwa. Mpaka sasa tumeshamkata zaidi ya shilingi bilioni 3.6 kwa kuchelewesha mradi ule.
Mheshimiwa Naibu Spika, imezungumzwa pia kuhusu mradi wa Sumbawanga na mradi huu pia nao umecheleweshwa, lakini tumembana Mkandarasi na mradi utakamilika utakapofika mwezi wa sita. Naye pia tumemkata karibu shilingi bilioni 4.2 kwa kuchelewesha mradi ule.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri 181 kila mmoja hapa angesimama angesema tu vijiji ambavyo havina maji; hiyo ni obvious wala mimi sitaki kupingana naye; yeyote atakayesimama. Hata Mheshimiwa Lukuvi angesimama angesema vijiji vyake ambavyo havina maji. Ndiyo maana tumeweka mpango huu kabambe wa WSDP kuhakikisha vijiji vyote vinapata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwamoto amezungumza kwa nguvu sana kuhusu maji Ilula. Tumepata watu wa kutusaidia Serikali ya Australia, ule mradi unakwenda kujengwa; na tupo kwenye hatua nzuri ya kuweza kufika muafaka. Kwa hiyo, zipo hoja nyingi sana na niseme tu, hoja zote ambazo Waheshimiwa Wabunge mmetupa kwa kuongea humu ndani kwa maandishi tutawapatia majibu. Labda nipitie baadhi ya hoja ambazo ninazo hapa.(Makofi)
Mheshimiwa Kiula alizungumza habari kwamba katika Halmashauri yake maeneo mengi ni kame na alikuwa anasema hawana mito; na alikuwa anafikiria, je, kwa nini maji yale ya Igunga yasifike mpaka Singida?
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi namwambia tu jambo hili itabidi tulifanyie usanifu kwanza (feasibility study) tuone possibility kama maji yale bado yatakwenda kwa njia ya mtiritiko. Ukisema utaweka pampu maana yake unaongeza gharama za uendeshaji mradi. Halafu tunasema maji ni lazima yalipiwe kwa sababu ili Serikali iweze kufanya miradi mingi na kuiendesha miradi hii ni lazima walipie. Kwa hiyo, unaweza kukuta gharama ya wananchi kulipa maji yale ambayo yametengenezwa kwa fedha nyingi inaweza ikawa siyo sustainable au endelevu. Kwa hiyo, mambo yote hayo tunayaangalia kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha tumeweka fedha kwa ajili ya kufanya usanifu kwenye mabwawa mapya ya Nduguti pamoja na bwawa la Mlanchi. Kwa hiyo, tutayafanyia usanifu.
Mheshimiwa Mboni Mhita amezungumza habari ya mabwawa yake ya Manga, Mkata na Kwa Ndungwa. Mwaka huu wa fedha Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuanza kujenga miradi zaidi ya shilingi bilioni 1.129 imetengwa kwa ajili ya kuanza kujenga miradi ya vijiji kumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Mheshimiwa Victor Mwambalaswa amezungumzia habari ya Bwawa la Matwiga; bwawa hili lilishakamilika, limefikia asilimia 85; tumewakabidhi Wakala wa Visima na Mabwawa kukamilisha hiyo sehemu iliyobaki. Kwa hiyo, bwawa hilo Mheshimiwa linakwenda kukamilishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Bwanausi, umetoa ushauri kwamba Serikali ijipange upya ili kusimamia fedha za miradi zinazopelekwa kwenye Halmashauri; ungetaka kiundwe Kitengo cha Ufuatiliaji. Mimi nafikiri solution ya usimamizi wa miradi ni hiyo kuwa na Wakala wa Maji Vijijini. Tutakuwa na mfumo endelevu wa kusimamia miradi ya maji. Kwa hiyo, ushauri wako ni mzuri na tunaupokea.
Mheshimiwa Savelina Mwijage alisema Mkoa wa Kagera una vyanzo vingi vya maji lakini havitumiki ipasavyo, ni pamoja na kutaka kuchukua maji kutoka Ziwa Victoria. Mkoa wa Kagera tunayo miradi ambayo inachukua maji kutoka Ziwa Victoria ikiwepo na Manispaa ya pale Bukoba maana ipo ndani ya Mkoa na pia Karagwe kuna ziwa ambalo lipo. Tunaanza na usanifu, kuchukua maji kwenye ziwa ambalo lipo jirani na Karagwe kupeleka mji wa Karagwe. Kwa hiyo, ushauri wako ni mzuri, tutaendelea kuangalia na vyanzo vingine ambavyo vipo karibu na wananchi.
Mheshimiwa Mgimwa alikuwa anashauri Rural Water Agency pamoja na kuongeza tozo ya shilingi 100. Ushauri wako unapokelewa na nimeshaelezea. Mheshimiwa Mary Nagu pia amezungumzia suala la kuimarisha Mfuko wa Maji pamoja na uanzishwaji wa Rural Water Agency. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Profesa Anna Tibaijuka amezungumza kwa kirefu kuhusu ushirikishaji wa sekta binafsi. Ni kweli tukisema miradi yote hii itafanywa na Serikali na kwa kulingana na uhitaji jinsi ulivyokuwa mkubwa, tutakuwa na safari ndefu. Sasa wazo lako ni zuri na ndiyo maana tumeanza utaratibu wa PPP, lakini kwa mfumo kwamba unatafuta mfadhili anayejenga ana-finance lakini Serikali inafanya operation.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, anajenga, anamaliza kujenga, anakabidhi Serikali inaendesha. Kwa hiyo, sisi ndiyo tutakuwa na wajibu kuhakikisha ule mradi unaendelea kuwa endelevu. Kwa namna nyingine unakuwa umeshirikisha Serikali pamoja na sekta binafsi kwa utaratibu wa PPP, kwa maana ya building and finance. Kwa hiyo, ushauri wako ni mzuri, tutaendelea kuhamasisha wananchi ambao wanaweza kujitoa katika eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu unaweza ukaja tukazungumza kwamba wewe unazalisha maji, sasa namna gani tutakubaliana fedha yako itarudi, namna ya kuendesha mradi ule, basi tunakaa na Serikali imesharuhusu kwenye Sheria ya Manunuzi kwamba tunaweza tukatumia sekta binafsi kwenye miradi ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Lolesia Bukwimba amezungumza habari ya Jimbo la Busanda kwamba lina kero kubwa ya maji na hasa katika Kata ya Nyakagomba na Nyamigota. Katika mwaka wa fedha tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 3.280 kwa ajili ya Halmashauri yako ya Busanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa fedha hizi zitakwenda kujenga miradi ambayo Halmashauri yako imeweka ndiyo kipaumbele. Kama bado kutakuwa na miradi ambayo fedha hizo hazijatosha, basi ni mpango, mwaka utakaofata tutaendelea na kuweza kujenga miradi ambayo itakuwa bado haijashughulikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa William Ngeleja alisema mradi wa maji wa Katungulu ulianza kutekelezwa miaka minne, hadi sasa haujakamilika. Tulikuwa na matatizo kwa miaka mitatu mfululizo, fedha ambazo zilikuwa zinatengwa kwa ajili ya maji hatujawahi kupata zaidi ya asilimia 40 ya allocation.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unaweza kuona kwamba kwa miaka mitatu yote mtiririko wake wa fedha haukuwa unaoridhisha na ndiyo maana unakuta miradi mingi tumeibua kama alivyosema Naibu Waziri, sasa tuna miradi zaidi ya 374 ambayo tayari mikataba imesainiwa na inaendelea. Kwa hiyo, jukumu letu sasa ni kuhakikisha kwanza tunakamilisha hiyo miradi ambayo tayari tulishaiibua kwa muda mrefu. Tunamaliza hiyo kwanza halafu tunaibua miradi mipya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ameongelea suala la kwamba, miradi mingi huko nyuma inachukua maji kutoka Ihelela unapeleka Kahama, lakini wananchi wa Ihelela hawana maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya miradi yote ambayo tunaiibua sasa, lazima watu wanaokaa kwenye chanzo wafikirie kwanza kupewa maji ili wawe ni sehemu ya kulinda miradi hii. Kwa hiyo, tunabadilisha mfumo na ndiyo maana unasema miradi yote na kwenye bomba kubwa, wote wanaokaa kilometa 12, ni lazima wapewe maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, miradi iliyokuwa imeshajengwa tunaanza kwanza kuanzia kutoka mwanzo mpaka mwisho, kwa sababu kwanza, hawa watatunza chanzo ili chanzo chetu kiwe endelevu, kiweze kutumika kwa miaka mingi ijayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda wangu ni mdogo na kwa kuwa Waheshimiwa Wabunge naamini kabisa wamenielewa nilivyosema kwamba tusiwe na shaka na timu hii tuliyokuwa nayo, tutakwenda kufuatilia miradi na kuhakikisha inatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna wengine wamezungumza habari ya miradi inajengwa chini ya kiwango. Sasa kwa kweli nitakuwa mkali katika wahandisi wote kwenye sekta hii ambao watafanya miradi chini ya kiwango. Tutahakikisha tunafuatilia ili miradi yetu iwe endelevu. Kwa sababu kuanzia usanifu, ujenzi, matengenezo, yote lazima tufuate specification za kihandisi ili miradi yetu iwe endelevu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakushukuru kwa nafasi hii. Naomba kwa heshima kubwa Waheshimiwa Wabunge mniunge mkono. Naomba kutoa hoja.