Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Martha Jachi Umbulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kupata nafasi hii na mimi nichangie hoja iliyoko mbele yetu. Na mimi nichukue fursa hii kwanza kukupongeza wewe binafsi kwa umahiri wako na ushupavu wako wa kuliongoza vyema Bunge letu, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja iliyoko mbele yetu ni mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti ya 2016/2017 na katika kuliangalia hilo, ni lazima tuangalie utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/2016 ili tuweze kujifunza tulikosea wapi na vipi tujisahihishe ili tuweze kwenda vizuri kwa bajeti yetu ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vipaumbele vilivyowekwa katika bajeti ya 2015/2016 mimi nimevichukua viwili ili niweze kuvichambua tuone ufanikiwaji ulikwenda kwa kiwango gani? La kwanza kabisa, kipaumbele chetu cha kwanza ilikuwa kupunguza umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la kupunguza umaskini, tukiangalia katika jamii zetu, kwa mabilioni na matrilioni ya fedha tulizowasomea wananchi mwaka 2015, ni kwa kiwango gani umaskini umepungua baina ya jamii yetu ya Watanzania. Hali bado ni mbaya sana vijijini, wananchi wetu bado hawana milo mitatu, wananchi hawana nyumba bora za kuishi, wananchi wetu bado hawana vyanzo vya uhakika vya fedha na kwa hiyo, ni vizuri kutafakari, ni kwa namna gani umaskini utapungua katika nchi yetu hasa kwa bajeti hii ya mwaka 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujipima hivyo, ni vizuri pia tukaangalia changamoto zilizojitokeza, changamoto kubwa ambayo imejitokeza katika kupunguza umaskini baina ya jamii zetu, kubwa ambalo limeonekana ni upatikanaji wa rasilimali fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Serikali imeweka mfumo thabiti wa ukusanyaji wa fedha katika bajeti ya mwaka huu na zaidi sana ni hili la kutumia electronic machines. Mfumo huu bado una changamoto kubwa sana. Pamoja na kuweka mikakati na adhabu zitakazotolewa kwa ajili ya watakaokiuka kutoza kutumia mashine hizo, bado mimi nina wasiwasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vituo vya petroli, kwa mfano, wakikwambia mashine hii ni mbovu ama iko out of order na ni kweli utakavyodhihirika hivyo, bado utakapomchukulia hatua mfanyabiashara ambaye mashine yake hiyo ni mbovu, utakuwa hujamtendea haki. Kwa sababu utakuta ni ukweli na umempa adhabu na kutakuwa na msururu wa watu kutaka huduma na watakapokosa huduma ya kupata petroli na dizeli wataleta lawama tena kwa Serikali. Kwa hiyo, nadhani tuangalie ni namna gani tutaboresha mfumo mzuri wa ukusanyaji kodi ili tuweze kutekeleza miradi yetu ya maendeleo katika Vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nililotaka kuishauri Serikali ni kwamba bajeti iendane na tathmini halisi ambayo tumeiona katika utekelezaji wa kipindi kilichopita. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona kwamba pamoja na jitihada za kupunguza umasikini ametenga shilingi milioni 50 kila kijiji. Dhamira yake ni njema na itakapotekelezwa itakwenda vizuri. Utekelezaji watatengeneza wataalam, lakini bado ametenga fedha hizo ili kuona ni namna gani umasikini utapungua katika jamii zetu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kipaumbele cha pili, kilikuwa upatikanaji wa huduma za jamii. Kilio kikubwa cha Waheshimiwa Wabunge tangu waanze michango humu tumeona ni kilio cha maji. Maji bado ni tatizo kubwa katika jamii zetu na kwa hiyo, kwa bajeti ya mwaka 2016/2017 ni vizuri kuendelea kubuni mikakati bora ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji. Sasa utaratibu uliopo, naipongeza pia Serikali kwa kutenga hiyo asilimia ndogo ya kuongeza kwenye tozo ya mafuta ya shilingi 100. Nina uhakika shilingi bilioni 250 zitakapopatikana, shilingi bilioni 220 zikienda kwenye usambazaji wa maji vijjijini itasaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ni mkatakati mzuri na mimi nauamini kwa sababu tozo ya kwenye mafuta na petroli ni tozo yenye uhakika, kwa sababu huduma hiyo ipo kila siku na tumeona kwenye miradi ya REA pia. Tozo zilizowekwa kwenye REA imetusaidia kusambaza umeme vijijini na kwa hiyo, hiki ni chanzo ambacho kinaweza kikatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huduma nyingine ya jamii ni suala la elimu. Nampongeza tena Mheshimiwa Rais kwa kuleta mfumo wa elimu bure, nina hakika tathmini mwisho wa siku itakwenda vizuri katika kuboresha elimu katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala zima la huduma za afya. Huduma za afya ni kipaumbele kingine cha pili baada ya maji. Suala la afya hasa kwa kabrasha hili ambalo limetolewa na TAMISEMI kwa Mkoa wangu wa Manyara, ni masikitiko makubwa sana. Nimeona katika taarifa hii iliyotolewa na TAMISEMI na hasa ikishirikiana na Wizara ya Afya; Mkoa wa Manyara katika mlolongo wa kuodhoresha zahanati na uboreshaji na ukarabati wa vituo vya afya, nimesikitika kuona Wilaya ya Simanjiro imewekewa zahanati moja tu, wakati Mikoa mingine na Wilaya nyingine zina zahanati mpaka 10 hadi 15. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, Wilaya ya Kiteto kubwa kama hiyo, imewekewa zahanati tatu tu. Tena cha kusikitisha fedha ambazo zitakwenda kukarabati majengo hayo ni Capital Development Grants ambazo mara nyingi wala hazipatikani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inasikitisha kwa Mkoa wa Manyara, sijui mikoa mingine imetumia mbinu gani kuhakikisha kwamba wamewekewa fedha za kutosha, lakini naiomba Wizara na Serikali na hasa maeneo husika kwamba waangalie hili. Wilaya ya Mbulu ina Majimbo mawili, lakini zahanati na vituo vya afya vilivyoorodheshwa hapa na vya Jimbo la Mbulu Mjini; tunaishukuru Serikali kwa hilo kwa sababu na mimi natokea huko, lakini ni vizuri kuiona Mbulu Vijijini kwani hakuna hata zahanati moja iliyoorodheshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeliona kabrasha hili nikadhani kwamba ni makosa yamefanyika, naamini kwamba wahusika watakwenda kuiangalia vyema na kuhakikisha kwamba kila Wilaya inanufaika na usambazaji ama upatikanaji wa huduma za afya ikiwepo kujenga zahanati na vituo vya afya katika kila kijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo…

NAIBU SPIKA: Kengele ni ya pili hiyo Mheshimiwa.