Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi hii adimu ya kuweza kuchangia hoja hii. Suala la maji ni suala ambalo linamgusa kila mtu katika ukumbi huu. Kila mtu katika eneo lake, katika Jimbo lake ana tatizo la maji na tatizo ni kubwa sana. Ningependa kuchukua ushauri ambao umetolewa hapa wa kuanzisha wakala wa maji vijijini. Ni ushauri muhimu na ni ushauri ambao ni lazima tujifunze na mafanikio ambayo yametokea au yamepatikana kwa REA. REA imetusaidia sana, imesaidia sana kwenye mambo ya Kampeni, sasa ni kwa nini tunashindwa kuanzisha huo Wakala wa Maji Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tabu ambazo Jimbo la Muheza linapata katika suala la maji sijui naweza kufananisha na nini, sijui ni sugu au sijui ni nini, lakini wananchi wa Muheza wana matatizo makubwa sana ya maji. Kuanzia pale mjini mpaka vijijini akina mama wanapata tabu sana ya maji wanashinda kwenye visima, na ukiangalia hayo maji ambayo wanayashindia huku visimani huwezi ukaamini. Wakati wa kampeni nilikuwa nakaribishwa na ndoo na nikaoneshwa maji ni udongo mtupu, maji sio salama kabisa. Kwa hiyo, kuna mambo mengi ambayo yanafanyika ambayo unaona wewe mwenyewe kama binadamu kwa kweli unashindwa. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, tunayo Hospitali teule pale, Hospitali teule ya Wilaya inashindwa kufanya operation kwa sababu hakuna maji, kwa hiyo maji ni tatizo kubwa sana Wilayani Muheza. Nimefarijika kuona kwamba kuna mpango ambao upo ndani ya kitabu cha Mheshimiwa Waziri kwamba mpango wa kutoa maji kutoka Mto Zigi ambao ni kilomita ishirini na mbili na nusu kutoka Muheza mjini mpaka mto Zigi Amani kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga wanatumia maji kutoka Mto Zigi na sisi wenyewe hatuna maji tulishakubaliana na watu wa Tanga kwamba na walishayapima kwamba maji hayo yana uwezo wa kutosheleza Muheza na Tanga yote na maji hayo kuna uwezo wa kuweza kukaa kwa miaka 30 ijayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo umefanyika utafiti wa mwanzoni, sijui imekuja Kampuni moja ya Hispania pale, EUROFINSA, Wizara ya Maji hii, Waziri kwenye bajeti iliyopita hapa Hansard nimeangalia ameahidi kabisa kwamba hao EUROFINSA watakuja na wataweka maji. Upembuzi yakinifu ulishafanyika na nimeona hapa kwenye miradi mikubwa 17 ya maji ambayo tunategemea labda, tunamwombea Mheshimiwa Waziri afanikiwe kupata hizo fedha ili huo mradi uweze kuanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mheshimiwa Waziri kwamba, anafahamu matatizo ya Muheza, amefika Muheza na ndiyo maana kwenye mradi huo ameuweka wa kwanza Muheza. Kwa hiyo, nataka wakati atakapokuja ku-wind up awahakikishie wananchi wa Muheza kwamba maji kutoka mto Zigi safari hii yatateremshwa. Awamu ya Tano imedhamiria na itateremsha maji hayo kutoka Mto Zigi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimefarijika kuona kwamba Mheshimiwa Waziri vijijini ametoa fedha ambazo ni karibu bilioni moja point moja na ushehe.
Kwa hiyo, fedha hizo namwomba zije zote, tutahakikisha kwamba maji vijijini Muheza kote wanaweza kupata na tutawachimbia visima na kuhakikisha kwamba maji hayo ni salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri sikuona fungu lolote la kusaidia maji Mjini Muheza. Ningeomba aangalie ataweza kunisaidia namna gani kuweza kuweka at least fedha kidogo katika maji Mjini Muheza, tuangalie uwezekano wa kuvuta maji kwenye visima ambavyo ni vingi na vinatoa maji kwa wingi, kuweza kuyasambaza kwa sababu ardhi ya Muheza ni chumvi kubwa sana ambayo iko pale kiasi kwamba hata ukichimba visima basi yatatoka magadi matupu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kitu ambacho Mheshimiwa Waziri anataka kufanya ni kuangalia vile visima vyenye maji mengi na kuangalia jinsi ya kuweza kuyatoa yale maji na kuyasambaza kwenye visima ambavyo viko karibu karibu. Nashukuru sana isipokuwa nilikuwa nashauri kwamba suala hili la maji hasa katika Jimbo la Muheza Mheshimiwa Waziri alipe kipaumbele kwa sababu 2020..
Mheshimiwa Menyekiti, naomba kuunga mkono hoja .