Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. George Mcheche Masaju

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi ninashukuru kwa kunipatia fursa hii niweze kuchangia. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuchangia hoja hii na nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hoja hii ina- cut across kwenye Wizara nyingi ndani ya Serikali naomba kuwashauri Wabunge wote wakubali kuliko kumbana Waziri tu, kwa sababu hapo yapo ya Wizara ya Katiba na Sheria, yapo ya Ardhi, yapo ya Nishati na Madini, yako ya Kilimo na Mifugo. Leo Waziri anaonekana hapa anaongelea haya lakini peke yake hayawezi akayatatua. Kwa hiyo, kwa sababu Waheshimiwa Wabunge wamezungumza kwa uchungu na wametoa ushauri mzuri sana kwa Serikali naomba tumuunge mkono Mheshimiwa Waziri ili aweze kuyatekeleza haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kushauri juu ya mambo matatu hivi ambayo yamezungumzwa hapa ya kisheria. Kwanza baadhi ya Wabunge wamezungumza mambo ambayo yanagusa utendaji wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa maamuzi yanayofanywa na Mawakili wa Serikali walioko kwenye Mikoa. Naomba kushauri mambo mengine muwe mnanishirikisha tu kule tunayamaliza, nawaomba Wabunge hawa waniletee hizo taarifa ili tuchukue hatua, inarahisisha zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni hili ambalo limezungumzwa juu ya huu mkataba mbovu wa Kiwanda cha Mgololo (Mgololo Paper Mills), hili naomba kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba nimeagiza waniletee ule mkataba kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili tushirikiane ndani ya Serikali kuangalia kama kweli kuna maeneo ambayo ni mabovu yanaweza kuboreshwa tuyafanyie kazi. Kwa sababu mikataba hii yote kwa kawaida huwa ina vipengele vya marekebisho ya mikataba ile kila wakati inapotokea. Ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kuleta taarifa hiyo humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninaomba kulitolea ufafanuzi ni jambo ambalo limezungumzwa kwa hisia nzuri na kwa ushauri kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge. Hili suala ni la taarifa ya Tume ya Uchunguzi na asili ya taarifa hii ni kwamba kulikuwa na Kamati Teule ya Bunge, Kamati Teule ya Bunge iliundwa kuchunguza juu ya Operesheni Tokomeza na moja wapo ya maazimio ya Bunge ilikuwa ni kwamba Serikali iunde Tume ya Uchunguzi ili kulichunguza hili suala. Kwa mujibu wa sheria ya Tume za Uchunguzi Sura ya 32 ya Sheria za Tanzania, anaeunda Tume hii kwa mujibu wa kifungu cha tatu ni Rais wa Jamhuri ya Muungano na ndiyo anaipatia Tume hii hadidu za rejea. Rais wa Jamhuri ya Muungano aliunda Tume hii kupitia Government Notice Na. 132 ya tarehe 2 Mei, 2014 akaipa hadidu za rejea na ika-report kwake mwezi wa nane, pia akatoa maamuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi kwa mujibu wa Kifungu cha 21 cha Sheria hii kinaeleza hivi;
“Baada ya kupokea ripoti ya Kamishna wa Uchunguzi Rais anaweza;
(a) Endapo Rais atajiridhisha kuwa upelelezi zaidi unaweza kufanyika au mashtaka kufunguliwa atamuelekeza Mkurugenzi wa Mashtaka kulishauri Jeshi la Polisi kuhusu utaratibu unaopaswa kufanyika au kuelekeza yafunguliwe mashitaka yanayostahili;
(b) Endapo Rais atakuwa na maoni kwamba hatua nyingine stahili zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu au watu ataamuru kwamba hatua hizo zichukuliwe.
(2) Pale ambapo itagundulika kuwa kulikuwa na hasara baada ya uchunguzi uliotokana na mwenendo wa mtu yeyote Rais anaweza kuamuru mtu anayehusika kulipa fidia kwa kiasi ambacho Waziri atathibitisha kuwa ni kiasi hicho kinachostahili.
(3) Rais anaweza kuelekeza kwamba taarifa yoyote ya Kamishna izuiliwe kutangazwa au izuiliwe kwa muda ambao Rais ataelekeza.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hili Rais ameelekeza kwa taasisi zote ambazo watendaji wake wamethibitika kutenda makosa au kukiuka sheria au utaratibu zote za utelekezaji wa Operesheni Tokomeza kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria. Aidha, kuzifanyia marekebisho sheria na kanuni zilizopendekezwa kufanyiwa marekebisho. Sasa kwa kuwa hatua ambazo zimechukuliwa na Rais kwa kuelekeza taasisi mbalimbali za Serikali zinahusisha uchunguzi, siyo vyema suala hili likatolewa taarifa hadharani katika kipindi hiki na sheria inamruhusu Rais nimewasomea hiki kifungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo siyo vyema na kwanza hii sio Taarifa ya Bunge ni Taarifa ya Rais, tuipe Serikali fursa aifanyie kazi haya mambo haya la sivyo tutaharibu hata uchunguzi na kile ambacho Waheshimiwa Wabunge wanataka kukifikia hawatakifikia. Huo ndiyo ushauri wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo naomba kulitolea ushauri ni hili ambalo limezungumzwa juu ya kesi ya Kamran. Kamran na wenzake watumishi wa Serikali walishitakiwa kwenye Kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 4 ya mwaka 2011 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi. Tarehe 5 Disemba, 2014 Kamran alitiwa hatiani akiwa hayupo kwa sababu yeye alipopewa dhamana alitoroka, lakini wale wenzake watatu waliachiwa hawakuonekana na hatia. Serikali imekata rufaa katika shauri la rufaa namba moja la 2016 Mahakama Kuu Moshi, kesi hiyo ya rufaa inasikilizwa kesho Moshi.
Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge naomba kuwaambia kwamba Serikali imechukua hatua lakini cha pili suala hili lipo Mahakamani nawapa hizo taarifa kesi hii ya rufaa ya Serikali dhidi ya hawa watu inasikilizwa kesho Moshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine sambamba na hili ni kwamba hatukukaa tu hivi pale, kulikuwa pia na watumishi wengine halafu pamoja na huyu Kamran Ahmed. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imechukua hatua, imeomba Serikali ya Pakstan katika utaratibu unaoitwa mutual legal assistance watuasaidie mambo fulani kuhusiana na tukio husika ili tuchukue hatua zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii pia Serikali inachukua hatua naomba kuwatoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali hii iko makini inajali maslahi ya wananchi kama ambavyo mnaishauri hapa, mtupe fursa tutekeleze yale ambayo tunaweza kuyatekeleza mambo mengine hayana shortcut, hatuwezi kuchukua bunduki tukailazimisha Serikali ya Pakstani itupatie vitu fulani ambavyo walikusudia kutupatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa ushauri huo naomba kuunga mkono hoja.