Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na niunge mkono hoja mapema.
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza na kumpongeza Waziri pamoja na Naibu Waziri na watalaam wake wote kwa kutuandalia Bajeti nzuri. Inaonyesha wazi kwamba, Mheshimiwa Rais anaanza kutembea kwenye kauli zake wakati wa kampeni za kuleta maendeleo kwa haraka. Kitendo cha kutenga asilimia 40 ya Bajeti yetu na kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, kinataka Tanzania iruke, kwa maana ya kuleta maendeleo ya haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pesa nyingi zimeelekezwa huku, nishauri kabla sijatiririka kwenye miradi. Nidhamu ndiyo muhimu, tunaweza tukajidanganya tukatenga pesa nyingi, lakini kama nidhamu itakuwa kama nilivyozoea kuona katika miaka miwili, mitatu iliyopita haitotusaidia na Wizara ya Fedha hii ndiyo imekuwa ikichelewesha kupeleka fedha za miradi katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, naomba nidhamu iwe ndio kitu cha kwanza kabisa cha kuangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la Kilimo, Serikali au Bajeti yetu imetenga zaidi ya Shilingi trilioni 1.56 sawa na asilimia 4.9. Pesa hii, kwangu naona ni ndogo hasa ukiangalia Matamko mbalimbali ya Kimataifa ambayo tumeridhia ikiwa mojawapo ni Tamko la Maputo kwamba, nchi zetu zinatakiwa zitenge angalau asilimia 10. Kwa hiyo, asilimia nne, bado tuna safari ndefu na naangalia asilimia nne imepungua hata kwa kulinganisha na mwaka jana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichopo hapa ni kwamba, kilimo hakijapewa mkazo na huku hiki kilimo ndicho tunachotegemea kukomboa nchi yetu. Kupitia kilimo, tumeajiri zaidi ya watu asilimia 70 ya Watanzania wetu, kupitia kilimo ndiyo sasa tunaingiza pesa nyingi za kigeni, lakini ndio Pato la Taifa zaidi ya asilimia 25 tunapata kupitia kwenye bidhaa za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba juhudi ifanyike kama hatutaweza mwaka huu, basi mwaka ujao tuongeze pesa zaidi katika kilimo. Kilimo hiki kina-support watu wa vijijini, ndiyo wapiga kura wetu hao waaminifu na ambao wamekuwa wakitekeleza sera zetu kwa utaratibu mzuri zaidi kuliko sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu hawa wamekosa maji, watu hawa wamekosa zana bora za kilimo, wamekosa kupata pembejeo kwa wakati. Nategemea Bajeti hii itajikita katika maeneo hayo na kuhakikisha kwamba, tunapata huduma bora katika wakati muafaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la Afya; katika maeneo yote nchini tumeshakubaliana kwamba tujenge Vituo vya Afya, tujenge Zahanati na huduma zitolewe. Katika eneo langu la Mkoa wa Rukwa na kupitia Taasisi mbalimbali za Kitaifa, imebainika akinamama na watoto, vifo vyao viko juu. Plan International, Africare pamoja na Taasisi zingine kama Benjamin Mkapa, wamebaini kwamba, vifo vya akinamama na watoto viko juu sana. Taasisi hizo wameweza kujenga Zahanati, Vituo vya Afya kadhaa, tumebaki sisi Serikali kuweka vifaa katika vituo vya afya na mojawapo ni Kituo cha Afya cha Kala ili huduma ziweze kupatikana za kuokoa akinamama ambao wanapoteza maisha bila sababu za msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba bajeti hii iende kujibu matatizo haya, tuitafisiri bajeti katika kuona kwamba, Zahanati zinaongezeka, Vituo vya Afya vinaongezeka, Watalaam wanaongezeka; hawa ni pamoja na Waganga, Nurses na Watalaam wa Maabara tuwaone wameongezeka katika vituo vyetu vya afya, watoe huduma bora ili wananchi waweze kupata afya nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni eneo la elimu, eneo la elimu limetengewa pesa nzuri. Naipongeza Serikali zaidi ya asilimia 22.1 ya bajeti, juhudi hii ni kubwa. Tafsiri yake ningependa kuona, tuione kuanzia Shule za Msingi kwamba Walimu hawa wanaokaa katika mazingira magumu, sasa miundombinu yao inaanza kuboreshwa kuliko ilivyo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu, Mwambao wa Ziwa Tanganyika, Walimu ni wachache, hawana nyumba, ofisi zao hazipendezi, kwa hiyo, kwa uhakika huduma inayotolewa inakuwa haitoshelezi, naomba juhudi hizo zifanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni umeme, mwaka jana tulitenga pesa nzuri sana kwenye umeme lakini matokeo yake hatukuweza kufanikiwa kwa sababu pesa hazikutolewa kwa haraka. Naomba kupitia bajeti hii, ambayo kwa hakika tumetenga hela nyingi kwenye umeme basi ielekeze katika maeneo ambao yako remote zaidi. Mwambao mwa Ziwa Tanganyika kuna umaskini mkubwa, lakini kuna Ziwa Tanganyika ambalo limesheheni samaki wengi na wananchi wa eneo hilo wote wanapeleka samaki Zambia.
Nimelisema hili mara kwa mara, naomba mikakati iliyopo ya Wizara ya Nishati na Madini waanzie katika eneo la Ziwa Tanganyika katika Jimbo la Nkasi Kusini kuhakikisha kwamba umeme unafika huko ili wananchi hawa waachane na hali ya sasa ya upagazi ya kupeleka samaki Zambia badala ya kupeleka katika nchi yao. Tuweze ku-attract wawekezaji katika eneo letu, itatusaidia zaidi katika kuboresha uchumi wa nchi yetu lakini pia uchumi wa Taifa zima kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wenzangu kusema kwamba, ile kodi inayotokana na mafao ya mwisho ya Waheshimiwa Wabunge haikubaliki. Haikubaliki na wenzangu wameieleza kwa ufundi mzuri zaidi, tutafute vyanzo vingine bado tunaweza tukavipata, tunaweza tukapata na itatusaidia. Vilevile pesa iliyotengwa kwa CAG ni ndogo, namna ya kukabiliana na ubadhirifu itakuwa ngumu sana na itakuwa kitendawili. Naiomba Wizara iangalie kwa umakini zaidi ili pesa…

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Mipata, muda wako umekwisha. Mheshimiwa Ignas Malocha, atafuatiwa na Mheshimiwa Prosper Mbena.