Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia nafasi hii kuchangia Bungeni kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili natoa hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kuhusu misitu. Nashauri uwepo mkakati kabambe wa kutunza misitu yetu. Itungwe sheria ya kuwabana wananchi waache kukata miti hovyo hovyo. Misitu inakatwa kwa matumizi mbalimbali kama nishati (mkaa), ujenzi na pia kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya kata mti panda mti ipo, je, inafuatiliwa? Pia kila Halmashauri kupanda miche ya miti milioni 1.5 kwa mwaka, hivi ni kweli inafuatiliwa sawasawa kuona kuwa miche inayopandwa na ile inayostawi ni asilimia ngapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, karibu asilimia 90 ya Watanzania wanatumia mkaa kama chanzo cha nishati (utafiti umefanyika). Nashauri kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini uangaliwe mkakati kabambe wa kupunguza kutumia mkaa kama chanzo cha nishati badala yake wananchi watumie nishati mbadala na nafuu. Tusipoangalia nchi yetu itakuwa jangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili vyanzo vya maji vitazidi kuharibika na maji yatakauka. Nashauri uwepo mpango kamili wa kunusuru misitu yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majangili wamezidi kuua wanyama na hasa tembo katika hifadhi zetu na hasa Ruaha, Selous na hata Mikumi. Tembo wanauawa, kilio cha tembo, tembo wachanga wanabaki yatima. Nashauri waajiriwe askari wa kutosha kusudi waweze kunusuru tatizo hili la majangili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Waziri aweke mikakati kabambe ya kukomesha ujangili huu na hasa ujangili wa tembo. Serikali iangalie sana chanzo cha kuua tembo na kuchukua meno ya tembo hasa ni nini na ni akina nani wapo nyuma ya ujangili huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya uongozi wa Awamu ya Tano naomba jambo hili lifanyiwe kazi, atakayebainika yuko nyuma ya biashara hizi achukuliwe hatua kali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utalii uzidi kutiliwa maanani ili nchi yetu ipate mapato zaidi. Nchi kama Israel uchumi wake unaendelea kuwa mzuri kwa sababu ya utalii, na baadhi ya nchi nyingine. Nchi yetu ni nzuri, inavyo vivutio vingi vya utalii kila kanda na kila mkoa. Ni kwa nini vivutio vya nchi yetu havitangazwi na hasa Kanda ya Kusini, Kanda ya Mashariki na Kanda ya Ziwa? Vyanzo vizidi kutangazwa kama utalii wa Kaskazini unavyotangazwa. Namna hii tutaweza kupata watalii wengi katika nchi yetu na pato la nchi kupitia utalii litazidi kukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahoteli katika hifadhi zetu za wanyama zingine hazifanyi kazi, zimeachwa tu. Mheshimiwa Waziri kuna hoteli ambayo ilikuwa nzuri sana kwa muonekano na kwa huduma kwa watalii wa ndani na nje katika Hifadhi ya Wanyama Mikumi, lakini imeachwa kama gofu ndani ya hifadhi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri anieleze kuna mkakati gani wa kufufua na kuendeleza hoteli hii ambayo ilikuwa inatoa huduma nzuri kwa watalii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara iangalie migogoro inayotokea kati ya wafugaji na wakulima na hasa mifugo kutoka nchi jirani kuingia kwenye misitu inayozunguka Wilaya ya Karagwe. Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na Wizara husika zingatieni matumizi bora ya ardhi. Migogoro si mizuri katika maisha ya binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.