Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba kwa namna ya pekee nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niseme machache. Mengi yameshasemwa, nami nitakuwa na machache kabisa. Naomba pia, Waziri wa Fedha, Ndugu Mpango na Naibu wake na timu yake niwape hongera kwa kazi. Changamoto bado ni kubwa kwa sababu ndiyo tumeanza bajeti. Kwa hiyo, tumeanza vizuri, nina hakika tutakwenda katika muktadha huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kabla sijaanza kusema ninayotaka kusema, nikuombe wewe mwenyewe kitu kimoja. Wewe Naibu Spika sasa hivi ndio mkubwa wa Bunge hili, nawe hakuna mashaka kabisa, uwezo wako tumeuona wote hauna mashaka hata chembe! Uwezo wako ni mkubwa, lakini wewe ni mkubwa wa taasisi hii sasa. Hivi Waheshimiwa Wabunge wa CCM naomba niwaulize swali moja, hivi sisi tukiwasamehe hawa tunakosa nini? Naomba mnisaidie tu, wewe ndio mkubwa wa mhimili huu; hivi Wapinzani hawa ambao wanakuonea wewe bila sababu, tukiwasamehe tunakosa kitu gani? Sisi ni Chama kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba, hatuna mashaka nawe, uwezo wako ni mkubwa, linda mhimili huu. Kamati ya Uongozi mkutane, Mama Naibu Spika una uwezo mkubwa, tuwahurumie hawa; wewe ni Mkristo, unasali; tuwahurumie hawa. Nami nina hakika, maana leo ukiwauliza kwa nini wametoka, sababu hawana, lakini na sisi tuulizane sisi tunapata faida gani wao kutoka hawa? Mnijibu swali, tunapata faida gani? (Kelele)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba unilinde, hoja yangu mimi nasema, sisi ni Chama kikubwa, tuna maslahi mapana ya kufanya, tuna kazi ya kufanya. Nakuomba kama Mkuu wa mhimili huu, mkae tumalize stalemate hii, haitusaidii kama Chama. Hayo yalikuwa ni mawazo yangu mimi. (Kelele)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hata kama halipendezi, lazima lisemwe. (Kelele/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa niliseme, nataka nijielekeze kwenye kitabu hiki cha Kamati ya Mheshimiwa Mama Hawa, Kamati ya Bajeti. Waheshimiwa Wabunge, ukurasa wa 28 na 29 wa Kitabu hiki cha Kamati, Kamati ya wenzetu wa Bajeti wananung‟unika, wanasema Serikali haijasikiliza maoni ya Wabunge. Yameandikwa humu ndani, naomba ninukuu;
“Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa Kamati ya Bajeti katika utekelezaji wa bajeti hii kwa kiasi kikubwa Serikali haikuzingatia maoni na majukumu ya Kamati ya Bunge ya Bajeti. Masuala la kibajeti ambayo ni ya kisheria Kamati hii imeona Serikali inayapuuza. Bunge linataka kufanywa kama rubber stamp kwa kuidhinisha bajeti ya Serikali.”
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba, narudia tena maneno yangu, wewe ni mkuu wa mhimili huu, linda hadhi ya Bunge. Kama liko tatizo limetokea kwenye Kamati ya Bajeti, ni vizuri kabisa Serikali wakae na Kamati ya Bajeti waelewane. Kwa sababu, Kamati ya Bajeti ndiyo inatusemea sisi Waheshimiwa Wabunge. Sisi wote hatuwezi kuwa kwenye Kamati ya Bajeti. Haiwezekani tuwe na Serikali ambayo haipokei ushauri wa Kamati ya Bajeti. Haiwezekani, mhimili huu tutauharibu, tutauvunjia heshima na Bunge ni chombo cha heshima.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba, yako mambo mengi yamezungumzwa na wenzetu wa Kamati ya Bajeti, hayapendezi. Wanalalamika! Haiwezekani Bunge letu sisi wenyewe, Bunge la Chama cha Mapinduzi wasisikie maoni ya Kamati ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, haiwezekani! Nakuomba jambo hili ulichukulie kwa uzito unaofaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 29 wa maoni ya Kamati hii wanasema, utaratibu wa Kikanuni wa kupokea hoja wakati wa kujadili bajeti umekaa vibaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni mwanasheria mzuri, tafadhali tuongoze vizuri. Hii Kanuni kama imekaa vibaya, tuiangalie upya ili Bunge liwe na maana katika upitishaji wa bajeti ya Serikali, vinginevyo tutakuwa rubber stamp tu.

TAARIFA....

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe Taarifa kaka yangu Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko kwa kutumia Kanuni ya 68(7) kwamba humu ndani hakuna Mbunge wa Upinzani aliyefukuzwa na Naibu Spika. Kwa hiyo, kusema Naibu Spika uwasamehe, ni kuondoa ukweli kwamba walioadhibiwa wameadhibiwa na Bunge zima na siyo Naibu Spika. Hawa waliotoka, wameondolewa na Mwenyekiti wao wa Chama, nami wameniomba niwatetee na ndiyo maana nimesema pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ulinde muda wangu. Hiyo hoja anayoizungumza Mheshimiwa Lusinde naikubali, wala sina matatizo nayo. Hoja yangu ni kwamba, sisi ni Chama kikubwa, ndiyo chenye ajenda. Hata hao wakitoka mwaka mzima hawana cha kupoteza hawa. Sisi ndio tuna ajenda yetu, ndiyo hoja yangu tu iko hapo. (Kelele/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tafadhali muda wangu ulindwe. Nilikuwa nazungumzia juu ya Kanuni ambapo wewe ni Mtaalam, jambo hilo mlizingatie.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba pia nizungumzie makato ya pensheni. Nimesikiliza maoni yakitolewa hapa, lakini naomba tu niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge sio Watumishi wa Serikali. Sisi Wabunge hatuna pensheni. Hatuna hata Bima ya Afya, ukimaliza miaka mitano ndiyo imetoka, haupo tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sielewi hata kidogo msingi kabisa wa kukata pensheni ya Wabunge, siuoni hata kidogo. Sababu zitakuwa ni nyingi. Kwa mujibu wa utaratibu, pensheni yenyewe ni kama posho tu. Pensheni siyo malipo ya moja kwa moja, ni kale kapesa unapewa kwamba Mbunge wewe kajikimu baada ya kazi yako ya miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha anakakata panga, kama alivyosema kijana hapa ili iweje? Waheshimiwa Wabunge, jambo hili halikubaliki kwa sababu, kwanza ni la kibaguzi. Kama hoja ni hiyo, ili Wabunge tuwe fair kwa mujibu wa ile Sheria ya Mwaka 1999 ya Political Pensioners Act, basi wale wote waliotajwa kwenye Act ile waorodheshwe tulipe kodi kama tunataka kuwa fair. Kwa nini Serikali wana-single out Waheshimiwa Wabunge tu? Hakuna sababu ya msingi. Labda Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze hoja ya msingi, kwa nini wanafikiri ni Wabunge tu ndio wawe liable kwa kukatwa pesa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vinginevyo jambo hili mrudi kwenye Kamati ya Bajeti. Hata kwenye Kamati ya Bajeti nao wanashangaa, wanalilalamikia vilevile. Hatuwezi kuwa na Bunge ambalo Wabunge hawasikilizwi, haiwezekani; na sauti ya Wabunge iko kwenye Kamati zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili hata Mheshimiwa Mama Hawa Ghasia kasema kwenye kitabu chake; hata Kamati ya Bajeti hawalijui jambo hili, Serikali wanalitoa wapi? Kwa hiyo, bado naamini kabisa, kama walivyosema wenzangu, bado kukata posho ya Wabunge hawa wakimaliza miaka yao mitano siyo sahihi na ni jambo ambalo halikubaliki, wakalitazame upya kwenye Kamati ya Bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa niliseme, limesemwa sana hili la biashara ya utalii. Mheshimiwa Waziri wala huhitaji mtu kwenda shule kuliona. Wapinzani wetu wakubwa wa biashara hii ni Kenya; wapinzani wetu wa biashara hii ni Rwanda; wapinzani wetu wa biashara hii ni Uganda; wote wameondoa VAT, wewe unaitoa wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, biashara hii tukiweka VAT maana yake watalii hawatakuja. Kama hawatakuja maana yake tutapata hasara. Tukipata hasara, hata hayo mapato ya Serikali yatashuka bila shaka. Kwa hiyo, naomba hii VAT kwenye biashara ya utalii ni jambo ambalo halikubaliki wala halina msingi wowote katika mazingira haya ya ushindani.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa niliseme ni hizi milioni 50 kwa kila kijiji. Ushauri wangu kwa Serikali, tujifunze kutokana na mamilioni ya JK. Tujifunze kutokana na experience ya mamilioni ya JK. Bahati nzuri kipindi kile nilikuwa Serikalini, zile fedha hazikuwa na impact yoyote, ni kwa sababu zilitumika vibaya. Sasa na hizi fedha shilingi milioni 50 kwa kila kijiji kwa muktadha huu kwamba tukafungue SACCOS ziende kwenye vijiji hazitakuwa na impact iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mmoja alizungumza jana jambo hili, ni vyema fedha hizi tukaangalia namna nzuri ya kuzitumia, hata kama maana yake ni kwenda ku-push on kwenye mbolea, kwenye viuatilifu na madawa ya mifugo ili wananchi hawa kama ni mkulima apate mbolea kwa bei ya Coca Cola. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi, vijiji viko vingi sana. Jimboni kwangu au Wilaya ya Kasulu kuna vijiji 108, mara milioni 50 ni takriban shilingi bilioni tano. Hizo shilingi bilioni tano ukizishusha kwenye pembejeo za kilimo, watu watakwenda kununua mbolea kama wanavyonunua Coca Cola na shida itakwisha. Tutakwenda kuwaeleza na jambo hili litakuwa na maana zaidi kuliko hivi tunavyofikiria eti kwenda kufungua SACCOS katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho nizungumzie miradi ya kipaumbele. Miradi ya kipaumbele ambayo imezungumzwa ni pamoja na barabara zetu muhimu; Bandari ya Dar es Salaam, Reli ya Kati, Barabara ya Kidahwe – Nyakanazi. Sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuwa ana-wind up ningependa kuelewa vizuri status ya hii miradi ya East Africa; miradi hii ya Afrika Mashariki ambayo katika ile barabara ya Kidahwe – Nyakanazi kuna portion ya kwenda Manyovu na kuna portion ya Kabingo – Kasulu ambayo inakuwa financed na East Africa. Napenda kujua status yake ili tuweze kwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ni dhahiri naunga mkono hoja kwa sababu ndiyo wanaanza, lakini mshirikiane na Kamati ya Bajeti. Serikali msiwe peke yenu. Nawashukuru sana.