Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Mattar Ali Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shaurimoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikupongeze wewe binafsi, kwa Waislamu tuna kauli tunasema Wallah umependeza kwenye Kiti hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri ambayo ameitoa mbele ya Bunge hili. Nimpongeze sana kwa hatua hii aliyochukua, bajeti hii imekaa vizuri na wananchi wengi wa Tanzania wamejenga imani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie kuhusu bidhaa zinazotengenezwa Tanzania Bara na kuuzwa Zanzibar kutozwa kodi Zanzibar na bidhaa zinazotengenezwa Zanzibar na kupelekwa Tanzania Bara kutozwa kodi Tanzania Bara. Hatua hii ni nzuri sana, inatia faraja sana kwa wafanyabiashara wetu. Hatua hii ambayo imechukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kigezo chote cha kuondosha migogoro ya wafanyabiashara wetu, kupunguza kelele na mizozo isiyokuwa na maana kwa wafanyabisahara wetu. Niwaombe sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iweze kukusanya kodi hii kwa nguvu zake zote bila ya kuwa na kitatanishi chochote kwa sababu kodi hii kipindi kirefu ilikuwa hailipwi na inaleta usumbufu mkubwa kwa wafanyabishara wetu na kupelekea kuwa na mzozo usiokuwa na maana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hatua hii iliyochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wizara husika kutoza kodi hii upande wa Zanzibar imesaidia kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa kodi kwa upande wa Zanzibar kukua, hata maisha ya upande wa Zanzibar basi yatakua ya hali ya juu kabisa. Kwa sababu kuna wafanyabiashara wachache walikuwa wakitumia mwanya huu vibaya kwa kuhakikisha hawalipi kodi hii kwa kuwa bidhaa hii inatengenezwa upande mmoja wa Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri afanye mazungumzo na Wizara ya Fedha ya Zanzibar ili na wao waweze kutumia mashine za EFD kwa ajili ya kukusanya vizuri kodi zake kwa sababu Zanzibar ukusanyaji wa kodi bado uko chini. Naamini Mheshimiwa Waziri anakaa na Wizara hii basi nimuombe sana kuhakikisha kwamba anawashauri wakusanyaji wa kodi wa Zanzibar, anaishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wafanyabiashara wetu wa kule Zanzibar waweze kutumia mashine hizi za EFD ili kuweza kukusanya kodi vizuri. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo ameifanya kwa kugundua tatizo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie vilevile maduka ya vyombo vya ulinzi kuondolewa msamaha wa kodi, hii ni hatua nzuri sana. Haya maduka kipindi cha nyuma watu wachache walikuwa wanatumia mwanya huu kujifaidisha kwa maslahi yao binafsi. Kwa hatua hii sasa itabana haya maslahi ya wachache. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri afanye jitihada binafsi kuhakikisha askari wetu wanapatiwa maslahi haya moja kwa moja wao wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nigusie mikopo ya elimu ya juu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa kuwa imeongeza idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo hii. Serikali inachukua wanafunzi hawa inawapeleka katika vyuo vya watu binafsi, inawapa mikopo wanafunzi hawa lakini hivi vyuo binafsi gharama yake iko juu tofauti na vyuo vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, naomba Serikali inapotoa mikopo kuwapelekea wanafunzi wa vyuo vya watu binafsi ifanye research mapema kabla ya kuwapeleka wanafunzi hawa katika vyuo hivyo kwani gharama zake ziko juu tofauti na vyuo vingine. Kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri suala hili aliangalie kwa kina. Kiukweli wanafunzi wetu wanaosoma katika vyuo vya watu binafsi wanapata tabu, ada zake ziko juu mno. Inafikia mahali wanafunzi hawa hawafaidiki na mikopo hii ambayo imeandikwa humu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano ni Chuo cha Kampala International University (KIU). Chuo hiki kina wanafunzi wetu kutoka Tanzania ambao wanasoma hapa lakini jambo linalosikitisha zaidi ada ya Serikali wanayopelekewa wanafunzi hawa ni takribani Sh.3,100,000 lakini chuo hiki gharama zake ni takribani Sh.6,000,000. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa kina tatizo hili. Wanafunzi hawa wanaendelea kupata taabu ndani ya vyuo hivi, wanashindwa hata kufanya mitihani yao, hata kuona yale matokeo yao wanashindwa kwa sababu ya kiwango kidogo cha fedha ambacho wanapelekewa katika vyuo hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba sana Mheshimiwa Waziri afanye kazi hii na nataka akija hapa aweze kueleza ni hatua gani Serikali itachukua kuwasaidia wanafunzi hawa kwa sasa ambao wanaendelea kupata shida. Wanafunzi hawa ni wa masomo ya sayansi wanasomea Udaktari na Serikali ina mategemeo makubwa na wanafunzi hawa. Kubwa zaidi wanafunzi hawa wanapewa mikopo ambayo watailipa, sasa ni kwa nini Serikali isiweze kuwapa mikopo ikakidhi mahitaji ya wanafunzi hawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kuhusu kuondoshwa kwa msamaha wa kiinua mgongo cha Mbunge. Kiukweli hili ni tatizo gumu sana. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, Ubunge wetu wa Majimboni ni tatizo sugu sana, ni tatizo kubwa. Mbunge Jimboni ni kila kitu, ni harusi, mchango wa mwenge lazima atoe. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, suala la kiinua mgongo cha Mbunge arudi tena kwenda kuliangalia pamoja na wataalam wake ili alipatie ufumbuzi mzuri. Suala hili kiukweli ndani ya Bunge lako hili Tukufu Wabunge wote akili zao hazifanyi kazi wanafikiria suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.