Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi. Niungane na wenzangu kuipongeza Wizara kwa hotuba nzuri na naiunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kadhaa ya kuchangia, kwanza ni migogoro ya vijiji vinavyozunguka kando kando ya hifadhi. Nkasi tuna Hifadhi ya Rwamfi Game Reserve, hifadhi hii ilikuwa mali ya Halmashauri, Halmashauri waliamua baada ya kuzidiwa kwamba hawawezi kuitunza wakaipa Serikali, lakini kulikuwa na vijiji kadhaa ambavyo vina migogoro na mipaka ambavyo ni Kasapa, King‟ombe, Mlambo, Mundwe, Namasi, Kata, China na Mlalambo. Vijiji hivi vinaambiwa kwamba viko ndani ya hifadhi, lakini vimekuwepo kabla hata ya hifadhi. Tunaomba sheria ziangaliwe upya ili waweze kurekebishiwa mipaka wapate maeneo mazuri ya kulima kwa sababu watu wameongezeka na kwa uhakika wanahitaji namna ya kuendeleza maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka kuzungumza ni suala la uhifadhi, namna ya kuendeleza maeneo ya utalii. Ninyi wenzetu mnaangalia huku tu, jaribuni kuangalia katika mikoa ya pembezoni na Rukwa ni mojawapo. Ukienda kwenye Ziwa Tanganyika kuna ufukwe mzuri sana, ufukwe ambao ni wa ajabu, una kingo za aina aina, mawe yaliyojipanga vizuri, visiwa vizuri lakini hakuna watu wanaowekeza. Nimeona tu kampuni moja kule Kipili kwa Mheshimiwa Keissy ndiyo amewekeza kutoka Arusha, lakini ni maeneo mazuri sana na hayatangaziki kwa sababu Wizara hamfanyi hivyo, barabara zenyewe zinazoteremka katika maeneo haya hazitoi hata motisha kwa mtu kwenda kufika. Kwa hiyo, mtusaidie kuangalia maeneo haya yakitumiwa vizuri yanaweza kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, karibu Namanyere kuna eneo linatoa maji moto linaweza likatumika vizuri kwa utalii. Ukienda njia ya Wampembe kuna mahali kuna maporomoko mazuri sana, Halmashauri wameweza kutembelea pale. Ukienda Jimbo la Kalambo kwa Mheshimiwa Kandege kuna eneo linaitwa Kalambo falls, yale maporomoko ni mazuri sana. Wenzetu wa Zambia wamekuwa aggressive wamejenga barabara nzuri wamefika pale wanafikia kirahisi, mwisho watu wanaamini labda Kalambo falls iko Zambia lakini sisi tumeshindwa kujenga barabara tu kusongeza pale na kuweza kuitangaza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo ngome ya Bismark pale Kasanga bado haijatangazwa vizuri na mambo mengine mengi tunaweza tukayaangalia kwa upya, vilevile lugha yetu ya Kiswahili, humu Bungeni tunaiharibu lugha, tungeizungumza vizuri lugha ya Kiswahili ingekuwa kivutio duniani hapa na Bunge lingetoa nafasi ya kuitangaza vizuri zaidi. Tukija humu sasa tunavuruga vuruga tunazungumza Kiswahili siyo Kiswahili tunachanganya na Kingereza basi tunakuwa tunaharibu, bado tungekuwa na utalii mzuri tu katika hili jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Utalii lazima iwe dhana pana iangaliwe katika mitazamo mbalimbali, wakati Halmashauri tunajenga miradi mbalimbali tuangalie maeneo ambayo tunayapa vipaumbele. Tuwe na timu ambayo inashauri hata uwekezaji binafsi kwa mfano, kule Nkasi, Kipili, kuna watu wenyewe wanaamua kujenga nyumba za wageni. Je, mnachukua initiative zozote kuwashauri ili wajenge waje na kitu kinachofanana na jengo ambalo mtalii anaweza kufikia?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wantumia mitaji sawasawa tu inalingana na mataji wowote ambao mtu anaweza akajenga lakini wanakosa utaalam na ushauri wa kitaalam ambao uwekezaji ule ungeweza kufanywa na mtu binafsi lakini ukaleta vivutio au mahali pa kulaza kwa watu ambao wanatutembelea katika maeneo hayo. Kadhalika katika miradi mingine yOyote tungekuwa na dhana pana katika suala zima la utalii, tusiangalie katika eneo moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la tatu na la mwisho ni huu mogogoro ambao ninauita mgogoro lazima tusiukwepe, mgogoro baina ya wahifadhi, wafugaji na wakulima. Mgogoro huu watu wengi wanauzungumza na tunazungumza hapa katika mitazamo miwili, mitazamo yote iko sahihi. Kuna wanaosema wafugaji wanafanya makosa, wanatuharibia sijui ardhi, wengine wanasema maliasili wanafanya makosa. Serikali lazima myapokee haya, sisi tumechaguliwa na wakulima, wapo waliochaguliwa na wafugaji, lakini haya yote matatizo tumeona athari zake kutokana na Operesheni Tokomeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata ripoti hapa, tumeangalia madhara ambayo huwezi kuyavumilia. Sasa kama Serikali na jambo hili lazima lije hapa Bungeni lipatiwe muafaka, hiki chombo hakiwezi kukwepa kulizungumza hili jambo, lazima liishe na tuzungumze hapa na msikwepe wajibu, watu wetu wana kufa, watu wetu wanaumia. Vilevile mazingira yanaharibika, mito sasa haitiririshi maji kwa sababu ya ufugaji wa hovyo, kwa nini msije na suluhisho mbona mambo mengine mnasuluhisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii naiamini kwa kujenga mikakati ambayo imeshindikana, kwa mfano nimeona katika Serikali hii tumeanza kukusanya mapato mengi kitu ambacho kilikuwa ni tatizo kubwa sana, katika Serikali hii nimeona ufisadi unaanza kupungua, nidhamu kazini imeanza kurejea hili litawashinda. Kaeni muone namna mtakavyoweza kuja na mawazo ambayo yatatusaidia kuondoa tatizo hili. Haiwezekani tatizo likawa linaumiza watu wetu, linaumiza wafugaji, linaumiza wakulima na Serikali isije na suluhisho, mimi siamini katika hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kushindwa kutoa suluhisho katika hili ni kushindwa kutekeleza wajibu wako Mheshimiwa Waziri, ninasema wazi kwamba ni lazima ukae na Wizara zilizo na mahusiano na Wizara yako ili jambo hili ambalo limekuwa kero kwa watu wote liweze kupatia suluhu, hatuwezi kuendelea katika mazingira hayo. Lazima mje na utaratibu, ndugu zangu ni kweli kule Rukwa tulianzisha Azimio la Mto Wisa, tunamkumbuka Mkuu wetu wa Mkoa alikuwa anaitwa Jaka Mwambi, namkumbuka mpaka leo. Mkuu wa Mkoa aliweza ku-manage kuweka wakulima na wafugaji wakakaa pamoja bila ugomvi wowote na wakahitajiana wote, kilichotakiwa kufanyika ni wale wafugaji waliokuwa wanafuga bila kuelewa wafanye nini mifugo yao, wakapata elimu wakaanza kuwekeza, kusomesha watoto, kujenga nyumba nzuri, kuwekeza katika maeneo mbalimbali na hivyo kuvuna mifugo ile ambayo ilikuwa inazidi.
Kwa hiyo, bado hilo linaweza likafanyika, baada ya kuondoka yule Mkuu wa Mkoa, mifugo imefurika kule Rukwa, Mheshimiwa Keissy hapa alizungumza vizuri sana, imezidi uwezo wa ardhi yetu kubeba, lakini kama Serikali wala hatujaona tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili tumeliona tangu wakati wa enzi ya Serikali ya Awamu ya Kwanza, Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu, Awamu ya Nne tulilizungumza sana na kwa wakati fulani nilisikia Rais anasema lazima litafutiwe ufumbuzi. Awamu hii ya Tano kama tutakosa kupata ufumbuzi tutashindwa kuelewa na wananchi watakimbilia wapi? Wataendelea kuuawa? Mtaendelea kuridhika tu watu wanauawa? Kama kweli utakuwa unaendesha Wizara na watu wanazidi kuuawa na hatua zozote hazijachukuliwa sioni kama ni vizuri. Ni vizuri hata kusema nimeshindwa ukaondoka kwenye nafasi, kwa sababu haiwezekani kabisa watu wanauawa tukatoa, lazima tutoe suluhisho na nafasi hiyo lazima ukae ujenge hoja ya msingi, wewe ndiyo sasa tumekupa dawati la mbele la kusuluhisha hili. Wizara yako na wengine wote Serikalini lazima mliangalie hili hatuna namna ya kufanya, hatuwezi kumwambia mkulima ndiye aje hapa aseme, hapana ni lazima tuseme na chombo cha kusemea ni sisi hapa. Hatuwezi kukaa katika makundi mawili tunashindana hapana ni kukaa mezani na kutafuta suluhu ya jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, naomba suala hili liwe na mwisho wake inawezekana mkiamua, kama hamjaamua haiwezekani. Ahsante.