Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili ni chombo cha wananchi na nataka niseme Bunge hili lingefanya kazi yake kama chombo cha wananchi na siyo vikao vya vyama, hii bajeti ya Mheshimiwa Maghembe ilikuwa haipiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri alikwenda kwenye tv anasema wafugaji wanatembea nyuma ya mikia ya ng‟ombe. Waziri anasema ng‟ombe hawana faida, kwanza faida yao Pato la Taifa wanachangia asilimia nne tu! Kwamba utalii sijui unachangia asilimia 22. Sasa unajiuliza hivi leo tungekuwa tumeondoa ng‟ombe wote katika nchi hii, kama sukari tu imetushinda kuagiza, nyama ninyi mngeweza kuagiza watu wakala nyama? Sukari peke yake imetushinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila kitu kwenye ng‟ombe ni pesa, maziwa, kwato, kila kitu! unachotupa pale labda ni sauti tu peke yake. Kila kitu kwenye ng‟ombe ni pesa. Tumeshindwa wenyewe kusimamia ng‟ombe hawa, leo watu wanasimama kwenye Bunge la Watanzania wanasema ng‟ombe wanaharibu mazingira, kwamba mifugo inaharibu mazingira. Ni utafiti wa wapi huo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Dar es Salaam watu wanatumia mkaa, nchi nzima ni mikaa. Watu wanakata miti kwa ajili ya mikaa, watu wanatumia nishati, tumeshindwa kupelekea watu nishati tunasema mifugo inaharibu mazingira. Hata mkiua ng‟ombe wote nchi hii halafu mkaacha watu wakaendela kutumia mkaa, nchi hii itakuwa jangwa. Pelekeeni watu nishati Dar es Salaam, pelekeeni watu nishati rahisi Arusha na Mwanza, Majiji matatu peke yake mki-control watu wasitumie mkaa kesho yake nchi hii itakuwa kijani tupu. Leo mnakuja kusema ng‟ombe anaharibu mazingira, ng‟ombe anakata mti? Hiyo haikubaliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Maghembe ukumbuke kwenye Bunge la Katiba aliwaita wafugaji nyumbani kwake akawanunulia chakula anawashawishi wapigie Katiba kura, leo unawaita kwamba wanaharibu, unasema ng‟ombe anaambukiza magonjwa, hauli nyama ya ng‟ombe wewe? Utakula pundamilia kila siku kweli? Hilo ni vyema likaeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijiji vimeingia kwenye migogoro na TANAPA na mbuga kwa sababu watu wa mbuga wana extend mipaka yao. Vijiji vya Nyanungu, Kegonga, vijiji vya Masanga, hivi vijiji mpaka mwaka 1963 vilikuwepo na vina GN! Baada ya mwaka 1963 mipaka ya mbuga imekuwa extended, ni migogoro kila siku watu wanauawa.
Mheshimiwa Waziri ninaomba Kata tatu hizo nilizozitaja, Kata ya Kwihancha, Kata ya Nyanungu, Kata ya Masanga - Gorong, I mean uende pale ukatatue ile mipaka, vile vijiji vilikuwa nje ya mbuga na mipaka ya TANAPA ndiyo imekuwa extended kufuata mwananchi na mnawahamisha hamna sehemu wanayochungia ndiyo maana inaleta migogoro. Kwa hiyo, hilo nilitaka niliseme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo leo tungekuwa tuna Bunge la Wananchi tusingepitisha bajeti hii ni Operesheni Tokomeza. Nina picha hapa, naomba karatasi moja ije mezani kwako na nyingine iende kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013 watu waliuawa, watu walichomewa nyumba zao, mifugo ilipigwa risasi, ng‟ombe anauawa, ng‟ombe anaua tembo. Mbuzi waliuawa, watu wakabaki wanalala nje, Bunge likaja likajadili hapa, mkasema watu walipwe fidia. Kuna watu waliuawa kinyama, panga linachomwa moto mtu anaambiwa akanyage kwenye panga, akikanyaga akitoa mguu nyama inabaki pale, watu walipigwa misumari. Bunge likaja likajadili hapa, hakuna kitu chochote mpaka sasa kilichozungumzwa kwenye bajeti hii ya Serikali kwamba hawa watu wanakwenda kulipwa vipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Serikali wanapokuja ku-wind up hapa watuambie hoja ya operesheni tokomeza, ambayo ilitokomeza watu wetu, watu maskini! Madiwani, Wenyeviti wa vijiji na mpaka leo majangili wakubwa hawajaguswa na operesheni hii. Hawakuguswa na hawajaguswa. Ninyi wote ni mashahidi mnakumbuka hapa, Al Jazeera walitangaza na BBC kwamba Rais wa China alipokuja Tanzania aliondoka na meno ya tembo. Hamkuwahi kukanusha. Wachina kila siku ndiyo wanakamatwa kwa sababu Serikali yetu inakwenda kupiga magoti kwa Wachina kila siku hamtaki kushughulika na Wachina. mnakuja kushughulika na watu wanyonge! watu maskini. Leo mnasema utalii, utalii huu, mimi sikatai kwamba utalii uwepo na unachangia kwenye Pato la Taifa lakini utalii unagusa mwananchi wa kawaida kule chini kweli kwa maisha yake? Mpaka pesa hizi zije kwenu, mje mzishushe ziende kwa wananchi, mzunguko wenu, mnaweza kweli? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu akiwa na matatizo atauza ng‟ombe wake, atatibu mke wake, atasomesha mtoto wake, atafanya maendeleo yake binafsi kwa pesa zake. Lakini pesa ambazo zinaingia Serikalini hatukatai, tunahitaji pesa hizi zije Serikalini, lakini ni lini mtazishusha ziende kwenye maendeleo ya mtu mmoja mmoja kule kijijini? Ng‟ombe ana mfungamano au mifugo ina mfungamano na maisha ya watu moja kwa moja ya kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba anapokuja ku-wind up hapa Waziri atuambie, hatukatai wafugaji watengewe maeneo, wapate maeneo yao ya kulisha, lakini leo tusije hapa tunawapaka rangi kana kwamba wafugaji hawafuati sheria, wafugaji siyo watu wazuri, wafugaji wanahonga Mahakama, yaani kila anayesimama hapa, kuna watu wanafikiri ng‟ombe ni mdudu lakini nyama ya ng‟ombe wanataka kula. Wamesimama huku wanazungumza mpaka wanatetemeka, wanasema tupigwe risasi. Tupigwe risasi kwenye nchi yetu? Tuna kosa gani sisi? Sisi ndiyo tunawaletea nyama mnakula kila siku hapa kantini nawaona pale mnabugia nyama, supu, makongoro sijui nini, yanatoka kwenye ng‟ombe hayo na maziwa, usipoletewa chai ya maziwa unalalamika, unafikiri maziwa ya mbwa hayo? Hayo ni maziwa ya ng‟ombe ni lazima yatoke kwenye ng‟ombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba watu wasizungumze hapa kudhalilisha watu wengine na wakazungumza kana kwamba hii nchi ni ya kwao peke yao. Hatukatai tunahitaji wakulima walime, tunahitaji na wafugaji tupewe nafasi ya kufuga katika nchi yetu.
Ninaomba sana Mheshimiwa Maghembe unapokuja hapa utuambie hawa watu waliouawa kwa mfano kule kwangu waliuawa Peter Maseya alipigwa vibaya sana na akauawa na familia yake mpaka sasa iko traumatized. Aliuawa Nicholas Wegesa Moserega, Mheshimiwa Waziri uje hapa utuambie nyumba zilizochomwa moto, ng‟ombe waliouawa kwenye Kata zile tatu zaidi ya ng‟ombe 184, uje utuambie majibu yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais aliunda Tume ya Majaji kwenda kuchunguza na mnachukua vitu hivi kwasababu mmeshawaona Watanzania ni wasahaulifu, mnachukua mnavitunza, mnaunda Tume, hamtoi majibu mnakalia yale majibu. Tunataka hayo majibu tuambiwe ni nini findings za hayo majibu na ni kwa vipi tunakwenda kuondoa matatizo yaliyojitokeza.