Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Saul Henry Amon

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rungwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SAUL H. AMON: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwenye Bunge lako Tukufu. Vilevile niwashukuru wapiga kura wa Jimbo langu la Rungwe kwa kunichagua kuwa mwakilishi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, sina mengi lakini vilevile siko mbali na Profesa Norman alichokizungumza, kwamba, utalii na hata mzungumzaji aliyepita ameongea hicho hicho, utalii umeangaliwa sehemu moja, hilo ndilo langu la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu misitu. Pamoja na kwamba kuna historia na jiografia ya misitu iliyopo na inayovunwa lakini naona ni Mufindi, Mufindi, Mufindi wakati wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msitu pale Mbeya ulikuwepo siku zote, siku hizi naona ni jangwa. Msitu wa Kawetele, toka ulivyovunwa sijui mwaka gani lakini mpaka leo hii Kawetele hakuna miti, Kawetele ni jangwa, hatujui kwa nini wanafanya hivi na kwa nini Maliasili na Utalii wameamua kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina sababu ya kujiuliza, tunashangaa hata Mbeya, Iringa tuna matatizo ya madawati, lakini hiyo miti ingeweza kusaidia madawati kwa ajili ya thamani ya ofisi zetu na shule zetu. Mimi kwa Mheshimiwa Waziri nina ombi kwamba, ningependa kuona mapema iwezekanavyo Kawetele inarudishwa kama ilivyokuwa zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna watu wanaoshambulia misitu ambayo imewekwa kama hifadhi. Rungwe na misitu mingine ya asili bado haihifadhiwi inavyotakiwa, sijajua ni wapi ambako mnaangalia, ni nchi nzima au kuna kipande ambacho mmeamua kukiangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia utalii, tunapozungumza maliasili, ni lazima tuzungumzie nchi yote kwa ujumla; kwa sababu pamoja na kwamba, ina faida kwa ajili ya kupata fedha, lakini vilevile kuna faida kwa ajili ya mazingira yanayoharibika na kupotea bure kwa sababu tu wahusika hawafuatilii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali haiwezi itupe wananchi wa Mbeya tupande ile miti tuweze kuitumia ile ardhi; kwa sababu Mbeya kuna watu wengi. Ukiangalia Mbeya misitu mingi imepandwa na wananchi na bado inavunwa vizuri na wananarudishia iweje Serikali ambayo inapata faida, kwa sababu ile ni kama biashara ya Serikali. Chukueni faida yenu lakini rudisheni mtaji pale pale, kwamba wakati wa kuvuna vilevile irudishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye Sekta ya Utalii. Mchangiaji hoja aliyepita ameongea habari ya kwamba, kuna service mbovu, lakini hiyo yote ni kwa sababu ya kutokuwa na utamaduni. Hatuna chuo ambacho ni thabiti kwa ajili ya kufundisha watu watakaohudumia hoteli zetu ili kuwe na kiwango cha Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tunacho chuo lakini hakitoi na tumebakia kugombana na kusema hawa hawafai. Angalia wenzetu wanaotoka nje standard zao wanavyofanya, ni kwa sababu wamewekeza kwenye vyuo vya utalii. Huko wanapata ma-manager wazuri, wapishi wazuri, wahudumu wazuri. Sisi hivyo vyuo viko wapi? Kweli mtu atoke Mwanza, aje ajifunze Dar es Salaam peke yake ni kweli? Mtu atoke Mbeya aende Dar es Salaam kujifunza habari ya chuo. Vyuo vilivyopo havikidhi haja ambayo inaweza ikatoa international services.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo bado kwenye utalii. Utalii hautangazwi Nyanda za Juu Kusini na kusini mwa Tanzania na maeneo mengine, watu mmejikita maeneo ya kaskazini peke yake. Mheshimiwa Waziri aende Malawi, akaone utalii unavyofanya kazi kwenye Ziwa Nyasa. Sisi hapa tuna Ziwa Nyasa na tuna fukwe ambazo ni nzuri, ambazo hazichafuki, hazina takataka, lakini hatuzitangazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuunga mkono asilimia mia moja mchangiaji aliyepita kwa uchangiaji wake, ametoa mchango wa kizalendo. Naomba Wizara na vitengo vyake, viweze kutangaza utalii uliopo. Kwa mfano, Nyanda za Juu Kusini wameongea habari ya barabara kwenda kwenye mbuga za wanyama, vilevile tunaongea habari ya barabara kwenda Mlima Rungwe, hakuna barabara watu waende wakatembelee Mlima Rungwe. Hatuna barabara kwenda kwenye fukwe nzuri za Nyasa, kuna Ziwa Ngozi ambalo haliingizi maji wala halitoi maji, hamna anayetangaza. Tuna Ziwa Kisiba, kuna ziwa zuri sana ambalo halichafuki, halitoi maji na wala haliingizi maji lakini hatulitangazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mtazamo wangu ninavyojua ni kwamba, hii Wizara inafanya biashara, tunaweza kufikiria kwamba, inafanya biashara kwa kulipa Serikali mapato ya bilioni 10 au15, lakini si biashara ambayo watu tungejiwekeza zaidi kwenye hayo maeneo kama ingekuwa zaidi ya hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu nyingi sana ambazo ningeweza kuchangia, lakini kufikia hapo haya yalikuwa ni mawazo yangu na kwamba, tuchukulie umuhimu wa hali ya juu kutangaza vitega uchumi vyote, vivutio vyote ambavyo vipo maeneo yote ya Tanzania bila kujali ni wapi, watu waende kote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimempa Mheshimiwa Waziri mfano wa kwenda Malawi akaangalie, wanatoka watu sehemu mbalimbali lakini fukwe tulizonazo sisi ni nzuri zaidi kuliko zilizoko Malawi. Haya ni yangu machache kwa leo.