Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Alex Raphael Gashaza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba Wizara hii ni Wizara Mtambuka, ni Wizara nyeti, ni Wizara inayolitangaza Taifa, ni Wizara inayotangaza fahari za Taifa, ni Wizara ambayo ina umuhimu wake. Najua wachangiaji waliotangulia wamechangia mambo mengi na nitasisitiza katika mambo kadha wa kadha. Nianze tu kwa kujikita kwenye bajeti yenyewe, nikimpongeza Waziri Mwenye dhamana kwa hotuba nzuri aliyoitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii kulingana na umuhimu wa Wizara hii naweza nikasema kwamba upo upungufu hususan katika bajeti ile ya maendeleo kulinganisha na changamoto ambazo zinakabili Wizara hii. Ningeomba na ningeshauri kwamba kiasi kilichotengwa kwa ajili ya maendeleo kiongezwe ili kuweza kukabiliana na changamoto ambazo Wizara hii inakabiliana nazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwanza kwenye upande wa utalii. Waliotangulia pia wamesema juu ya promotion katika sehemu hii ya utalii. Naweza nikasema kwamba promotion bado haijafanyika kwa kiasi cha kutosha, hasa promotion kwa utalii wa ndani. Ukijaribu kuangalia Watanzania walio wengi leo ambao angalau wana ufahamu, zaidi ya milioni 30 hawajui fahari, hawajui rasilimali za utalii ambazo tunazo sisi Watanzania. Kwa maana ya kwamba ni wengi ambao hawapati access kuingia kwenye vile vivutio vya utalii. kwa hiyo tunayo kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba tuna-promote utalii wa ndani ili kuweza kuongeza pato katika sekta hii ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado pia tunavyo vyanzo vingi ambavyo hatujavitumia vizuri ili kuweza kuongeza utalii. Vyanzo hivyo ni pamoja na fukwe ambazo tunazo katika bahari kuu, ukianzia Tanga, Dar es Salaam ukashuka mpaka Mtwara zipo fukwe nzuri ambazo tungezitumia vizuri zingeweza kuongeza utalii na kuongeza pato la Taifa. Kwa mfano, ukienda Maputo Msumbiji unaweza kuona jinsi ambavyo wamejaribu kutumia fukwe zao na zinaingiza pato kubwa la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia bado yapo maeneo ya asili ambayo hatujayatumia vizuri. Ukienda kwa mfano, Iringa kwenye zile palace za Ki-chief kwa Chief Mkwawa, leo inatumika kama kituo cha utalii. Kuna aliye-raise hoja ya mjusi mrefu duniani ambaye alitoka Tanzania na akapelekwa Ujerumani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba niwakumbushe Watanzania pia kwamba katika harakati kama mnakumbuka wakati ule wa Vita vya Maji Maji hata Chief Mwenyewe Mkwawa mnakumbuka kwamba baada ya kuuawa kichwa chake kilichukuliwa kikapelekwa Ujerumani. Lakini tarehe 9 Julai, 1954, Kichwa chake kilirudishwa Tanzania na kikawekwa mahali maalum kama makumbusho kwenye palace ya Chief Mkwawa pale Iringa Kalenga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali kupitia Wizara hii, kichwa cha Chief Songea ambacho nacho pia kilipelekwa Ujerumani ni wakati sasa wa kupaza sauti na kukirudisha, ili kusudi kiwekwe kwenye museum na hatimaye kiweze kuwa kituo cha utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna miundombinu pia ambayo haitoshelezi, haikidhi hususani katika maeneo ya utalii kwenye Wizara hii. Kwenye kitabu cha bajeti wameeleza juu ya kuongeza vifaa kwa ajili ya (patrol) ya doria kupambana na majangili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kutokana na miundombinu kutokuwa rafiki wakati mwingine kufika kwenye maeneo ya utalii ni ngumu; niombe pia waweze kuongeza ndege kwa ajili ya shughuli yenyewe ya utalii, kwa sababu mahali pengine barabara hazipitiki, huwezi kwenda kwa magari. Kwa hiyo, wajaribu kuongeza pia ndege kwa ajili ya shughuli hizo za kitalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi Jimboni kwangu, kwa sababu muda siyo rafiki. Jimbo la Ngara ni Jimbo ambalo lina takribani game reserve mbili. Kuna Game Reserve ya Burigi yenye hekta 13500 na kuna Game Reserve ya Kimisi ambayo ina takribani hekta 35,000. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Waziri kwamba katika hifadhi hizi Jimbo langu la Ngara na Halmashauri yangu ya Ngara hainufaiki na chochote. Burigi Game reserve iliingizwa kwenye gazeti la Serikali tangu mwaka 1959, lakini mpaka leo ile tozo ambayo inatakiwa kurudishwa Halmashauri ya asilimia 25 kutokana na shughuli za uwindaji zinazofanyika haijawahi kutumwa hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Game Reserve ya Kimisi vivyo hivyo imekuwa gazetted tangu mwaka 2005, mpaka leo haijawahi kutolewa hata senti tano. Mbaya zaidi Kimisi Game Reserve sasa imekuwa ni kama kichaka cha majangili, wanaonufaika katika Kimisi Game Reserve ni wageni kabisa tofauti na Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wa hii Kimisi Game Reserve unaanzia Rusumo boda unashuka kwenda Karagwe jirani kwa ndugu yangu Innocent Bashungwa. Kuna Kijiji cha Kashasha kule ni mpakani na Rwanda, upande wa Rwanda ni wananchi wanaishi pale. Game reserve yao ya Kagera iko ndani na ndiyo game ambayo wanaitegemea sana kwa upande wa Rwanda kwa ajili ya kuingiza kipato kama utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wa Tanzania unapovuka mto tu unaanza na pori na kule kuna wanyama, kule kuna ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo, kuna maziwa kama Ziwa Ngoma ambalo ziwa lile nafikiri halijawahi kufanyiwa utaratibu wa uvuvi au wa uwindaji mzuri. Kuna viboko wanaibiwa mle, tena wanaibiwa na watu kutoka Rwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kambi moja ya Wanyamapori iko Rusumo pale lakini nashindwa kuelewa wanafanya nini? Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri pamoja na changamoto iliyoko ya mifugo iliyoko mle ndani, lakini niseme kwamba changamoto ni usalama wa maeneo yale na mipaka yetu ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba kama ambavyo upande wa Rwanda wamefanya kutengeneza kama Buffer Zone ambayo wananchi wanakaa wanaendesha shughuli za kilimo, basi na upande huu mwingine kwa ajili ya kuimarisha usalama, tuweze kuangalia namna gani tunaweza kuitumia ardhi ile kwa ufasaha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Ngara ni Jimbo ambalo lina vivutio vingi vya kitalii. Tuna maporomoko ya Mto Rusumo, mto unaotenganisha Rwanda na Tanzania. Maporomoko yale ni maporomoko ambayo tukiyatumia vizuri ni kivutio kizuri sana cha kitalii. Bahati nzuri eneo lile ni eneo ambalo sasa lina miradi mikubwa. Kuna mradi wa umeme unaozalishwa pale, kuna daraja kubwa la Kimataifa ambalo limefunguliwa juzi na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, kuna maeneo ambayo tukiyatumia tunaweza tukainua pato hususani katika sekta hii ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna vilima vinaitwa vilima vitatu. Hivi vilima vitatu vinaunganisha nchi tatu ambazo ni washirika wa Afrika Mashariki, Tanzania, Rwanda na Burundi. Vilima vile ni kituo kizuri kinachoweza kuwa kituo cha kitalii kama Wizara hii inaweza ikawekeza katika eneo lile. Pia bado tuna pango ambalo lilikuwa linatumika kama root ya kupitishia watumwa wakati wa utumwa. Pango ambalo ni underground, unatembea kilomita tano uko ndani ya pango. Lile limegeuka kuwa ni pango kwa ajili ya maficho ya majambazi. Hili likiandaliwa vizuri, likatunzwa vizuri ni eneo ambalo linaweza likawa ni zuri sana kwa ajili ya kivutio cha utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo kadha wa kadha ambayo ningeweza kushauri. Kama nilivyotangulia kusema kwamba, Wizara hii ina changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na changamoto ya ujangili, naomba Serikali sasa ifanye mipango mikakati ya dhati kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inadhibiti hali hii ya ujangili, pia migogoro inayojitokeza ya wakulima na wafugaji. Pamoja na kwamba tumeshauri kuwa Wizara zote ambazo zinaingiliana ziweze kukaa pamoja na kuweka mipango ya pamoja, naomba ufanyike utafiti wa kuona ni namna gani ambavyo ardhi hizi, misitu hii, reserve hiziā€¦
Mheshimiwa Mwenyekiti naunga mkono hoja.