Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipompongeza dada yangu Mheshimiwa Esther Matiko kwa hotuba yake nzuri ambayo inaonesha wanawake tunaweza, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwambia Mheshimiwa Maghembe kwamba tutakayoyachangia hapa ndiyo atatudhihirishia ule msemo wa Kinana kumwita ni mzigo au lumbesa ni kweli au atudhihirishie hapa yeye ni mwepesi kama tissue.
KUHUSU UTARATIBU....
MHE. ESTER A. BULAYA: Nasema hivi, kama „tissue’ linakwaza namaanisha „wepesi‟ basi „tissue’ litoke „wepesi‟ libaki pale pale. Atuambie kama yeye ni mzigo au mwepesi. (Makofi)
MWENYEKITI: Endelea.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka kujua, nilipomaliza uchaguzi nilienda Ngorongoro, sikwenda South Africa kama wanavyoenda wengine, kuna mbuyu pale una eneo kama sebule, majangili walitengeneza ndani ya hifadhi ya Tarangire. Nataka kujua, tangu Wizara yake imegundua nchi yetu imepoteza tembo wangapi? Yaani majangili wanaenda kwenye mbuga, wanatengeneza mbuyu unakuwa kama sebule na askari wapo halafu tunaambiwa baadaye ndiyo waligundua. Tunataka kujua waliohusika na eneo hilo walichukuliwa hatua gani? Hilo ni jambo la msingi. Akitujibu hayo, nitajua yeye mwepesi au mzigo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine limeongelewa kwenye Kambi ya Upinzani kuhusiana na kampuni iliyopewa kuwinda, Waziri ametoa barua tena wakati Waziri aliyehusika aliinyima. Miongoni mwa waliokuwa Wajumbe kwenye Tume ya Uwindaji jana alipokuwa akichangia Mheshimiwa Nsanzugwanko alisema watu wale walikuwa hawafuati taratibu na inasemekana walishaua mpaka na simba. Sasa ni sababu zipi ambazo Wizara hiyohiyo moja ina maamuzi mawili tofauti kwenye hiyo kampuni inayolalamikiwa haifuati taratibu, huyu ananyima kibali, huyu anakuja kurudisha, kuna kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kimezunguka hapo? Yaani huyo mtu anachezea tu sharubu za Wizara anavyotaka. Tunaposema haya, tunayaongea kwa sababu hatuhitaji Serikali ichezewe na hao mapapa. Haiwezekani Wizara hiyohiyo moja mnakuwa na maamuzi mawili kwenye kampuni moja yaani mnapingana na Tume yenu ya Wanyamapori? Kweli, atujibu mzigo au mwepesi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukichangia humu ndani kuhusiana na mambo ya wakulima na wafugaji. Jimboni kwangu nina hifadhi, wakulima na wafugaji, yote nayahitaji. Kama kiongozi, siwezi nikaja hapa nikasema nahitaji uhifadhi halafu eti najitoa wazimu nasema nawachukia wafugaji, sitakuwa natenda haki. Wala sisemi kwamba napenda wafugaji halafu niseme sihitaji uhifadhi, sitakuwa nalitendea haki Taifa langu. Mheshimiwa Waziri wa Maliasili hili hawezi akalimaliza kwa kauli, hawezi kulimaliza peke yako, lazima Wizara zote tatu zikae na tukubali kwamba tulikosea, hatukuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba wa Taifa alisema kukiri kukosea siyo shida, ni mwanzo wa kujipanga upya. Taifa letu lilikuwa halijajipanga kwa future kwenye matumizi bora ya ardhi. Leo hii ukiwa unatoka Hong Kong ukapanda treni unaenda Guangzhou utaona upande huu ni mashamba ya kilimo na upande huu kuna mashamba ya mifugo, hakuna mwingiliano pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua hatujapanga matumizi bora ya ardhi na hawa wafugaji bado hatujawafatutia soko la kutosha. Tujiulize leo tuna viwanda vingapi? Tunalalamika wengi, tuna mkakati gani wa kuhakikisha wanafuga mifugo ya kisasa na wanapata soko ndani ya nchi yao kuliko kuja hapa kama viongozi tunapasuka humu ndani, hivi tukitoka nje tunaweza kulisaidia Taifa letu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ya msingi lazima Mheshimiwa Waziri wa Maliasili akae na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Waziri wa Ardhi ili kuona ni namna gani tunaweza tukalitatua tatizo hili lakini kwa Wabunge kutupiana mpira humu ndani hatuwezi kufika na tusicheze na vita ya ardhi, ni mbaya sana. Mheshimiwa Waziri, hili ni jambo nyeti, jambo linalohusu Taifa letu, kama tumeshindwa kugombana katika uchaguzi, hatuhitaji ardhi yetu ije itugombanishe. Lazima tutengeneze mazingira mazuri ya vizazi vyetu siyo kuja kugombana humu ndani ya Bunge. Sisi ni viongozi, lazima busara itutawale katika kutatua migogoro hii, siyo kwa kauli tu ondokeni, mnakowapeleka kuna malambo au mazingira yakoje? Hilo ni jambo la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala la tozo kwenye hoteli, nilikuwa Mjumbe wa Kamati, naomba jambo hili Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa muktadha wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Esther amezungumzia hapa kwamba kuna shilingi bilioni tatu zinapotea lakini tangu kesi ilipokuwa mahakamani Serikali imepoteza zaidi ya shilingi bilioni nane. Leo Wizara hii inashindwa kukazia hukumu wakati Jaji amekuwa mzalendo kwa Taifa lake, kuna nini hapa au hawa watu wenye hoteli bado na wenyewe wanaichezea Serikali wanavyotaka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la kusisitiza, duniani kote hakuna utaratibu wa double entry, utaratibu ni single entry. Mheshimiwa Waziri, mtalii anaingia akitoka lazima alipe tena, tunaona katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nije Jimboni. Nilizungumzia suala la wananchi wangu kuhusu tatizo la mamba, Naibu Waziri akajibu amekwenda kupeleka swali langu katika Halmashauri ya Wilaya, mimi niko ya Mji ndiyo maana alipewa yale majibu. Mimi mwenyewe ofisi yangu ya Mbunge nimehudumia zaidi ya wananchi wanne Mheshimiwa Maghembe, kuna tatizo hili na nashukuru Mheshimiwa Waziri alikiri kwamba ataenda kulifuatilia. Peleka tu watu wa kuvua hatujaomba pesa ili wananchi waondokane na tatizo hili la mamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, wananchi wangu hawataki kuomba chakula. Wanalima lakini tembo wanakuja kuharibu mazao ya wananchi. Hawa nao wameingia kwenye hifadhi? Mheshimiwa Maghembe, please wananchi wa Mara wanaona haya kuomba, tunalima! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wangu wa Nyatwali, Tamahu, Serengeti, Kunzugu, Mihale, Bukole, Mihale nilienda na Mheshimiwa Jenista ameona mwenyewe shamba lilivyoharibiwa. Mkasema mtapeleka magari kule hawafanyi patrol, juzi tembo wamekula heka 20, please, tafuteni ufumbuzi wa kudumu. Watu hawafanyi patrol tuone ni namna gani hawa wananchi wataondokana na tatizo la kuliwa mazao yao. Namwomba sana Mheshimiwa Maghembe ashughulikie suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, wananchi wangu wa Kijiji cha Serengeti, Tamahu, Nyatwari wanataka kujua hatma yao maana wanatishiwatishiwa kuhama. Hawajapewa fidia, hawajashirikishwa na kuna maendeleo kule kuna shule, zahanati na kuna kila kitu. Haiwezekani mtu akaamka tu akawambia leo mnahama bila kuwashirikisha wananchi. Kuna wazee pale wa miaka mingi lazima haya mambo yawe wazi. Wanahama mnawapeleka wapi, kwa fidia ipi, mbona hamjawashirikisha? Hayo ni mambo ambayo nataka anipatie majibu ili nimpime yeye ni mzito au mwepesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.