Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kipekee kabisa namshukuru Mungu kwamba, ametuweka tena hapa kuzungumzia maendeleo ya nchi yetu, hii ni fursa ya pekee kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeze sana Waziri wetu wa Fedha na Mipango. Bajeti hii ni nzuri na imeweka mazingira ambayo yataweza kuwavutia wawekezaji wa nje na ndani, lakini kuna maeneo ambayo yanatakiwa tuyaangalie kwa undani zaidi, nitaongelea kwa hawa wawekezaji wetu wa ndani ambao ni wakulima, wavuvi, wafugaji na wachimbaji wadogo wadogo, kwa sababu hao ndiyo walio karibu zaidi na wale wananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu lazima iweke mazingira rafiki kwa watu hawa kuweza kufanya shughuli zao, hawa wakifanya biashara zao vizuri au wakifanya mafanikio katika biashara zao watawezesha wale wananchi wa kawaida ambao wanatumia bidhaa zao wapate chochote ili waweze kukitumia na hivyo basi kwa kutumia vile ambavyo hawa wanazalisha kodi itapatikana na itachangia katika bajeti yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ina maeneo mawili, kuna ukusanyaji wa mapato na matumizi ya mapato. Ni muhimu kabisa wote tulio hapa na walio nje waone jinsi gani makusanyo yanafanyika na yanafanikiwa. Mara nyingi makusanyo yakishakuwa kidogo hata matumizi hayapatikani kabisa. Bajeti ya mwaka uliopita, mwaka 2015/2016 tuliona jinsi gani makusanyo yalisuasua na haya yalipelekea matumizi kutokufanyika kwa wakati. Suala hili la wakati ni suala ambalo linafanya mambo yote yanakuwa hayatekelezeki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kabisa ambavyo watu wamekuja kupewa hela miezi miwili kabla au wanapewa hela kipindi ambacho hawawezi kuzitumia tena. Hii inawapelekea wale watu kutumia vibaya kwa ubadhirifu au inaleta mambo mengine ambayo siyo mazuri. Naomba kuanzia sasa tusimamie makusanyo na hapa nipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano, tumeona makusanyo ambavyo ni mazuri, tunaambiwa kwa mwezi ni trilioni moja na zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuyasimamie makusanyo hayo na yaende sasa na jinsi bajeti ilivyopangiliwa, makusanyo yaende kama yalivyopangiliwa kwenye matumizi. Wale ambao wanapewa kutumia wasimamiwe, kwa sababu kama hujampa huna cha kumsimamia na wewe sasa huwezi kumuuliza chochote, unamuulizaje na hukumpatia? Naomba hilo liwe angalizo na wote tushirikiane kuona inaendaje.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia hapa ni kuhusu vijana na wanawake, nikisema vijana ile dhana kwamba kijana ni mtoto wa kiume tu hapana hata mabinti zetu ni vijana, vijana ni ‗ke‘ na ‗me‘ sasa inapokuja kwamba wanafanya shughuli zao mathalani wengi wa vijana wetu wanafanya mambo ya saluni za kike na kiume, lakini pia wana ujasiriamali wa lishe, kuna hawa ambao wanapika na kuna wengine ambao wanatengeneza vitu ambavyo vimekaushwa, kama ndizi za kukausha, popcorn na vitu vingine, yote hiyo ni vitu vya ujasiriamali mdogomdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wanatakiwa wawezeshwe kwenye vifungashio ili wafanye vitu vyao kwa usafi. Nani atakayewawezesha? Ni Serikali iweke mazingira rafiki ya wale ambao wanawapatia vifungashio hivyo vipatikane kwa wingi na kwa urahisi. SIDO ndiyo mahali ambapo vifungashio hivyo vingetoka kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona maeneo ambayo SIDO imetamkwa kwamba itasaidika au itafunguliwa zaidi. Nimeona Mkoa wa Mbeya, nimeona Mkoa wa Pwani lakini sikusikia Kilimanjaro ikitajwa, naomba kwa vile ile SIDO ya Kilimanjaro iko vizuri na vitu hivi vinafanyika, Mheshimiwa Waziri wetu wa Viwanda na Biashara aweke jicho lake kule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mengi ya kutaka tushirikiane lakini sasa muda siyo rafiki kwangu; naomba nirudi kwenye jambo moja ambalo naona nisipolisema leo nitaweza nikakosa usingizi, kuhusu Serikali kulipa madeni yake ya ndani. Tulizungumza hapa na wakatueleza ambavyo taasisi zake zinadaiwa na mojawapo ikiwa ni taasisi ya maji inayoitwa MUWSA kule katika Mkoa wa Kilimanjaro. Mamlaka ya maji ile imefinywa sana, wametoa maji katika Chuo cha Polisi (CCP) na maeneo mengine ya Serikali kama Magereza lakini maji yale hayalipiwi. Itamkwe wazi kama Serikali inaona taasisi hizo zitumie maji bure ijulikane!
Mheshimiwa Naibu Spika, napata uchungu, inabidi sasa maji yapandishwe bei na anayeumia kwenye maji zaidi ni mwanamke, mwanamke yule atasaidiwaje! Inawezekanaje taasisi za Serikali zitumie maji bure na zile mamlaka zinajilipa mishahara zenyewe hazitegemei Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena naomba Serikali ilipe madeni yake mapema iwezekenavyo, taasisi zile zifufuke ziweze kununua vitendea kazi kama magari. Tumeambiwa kwamba, kuanzia sasa madeni ya taasisi yatalipwa centrally, naomba Hazina ilipe haya madeni mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu hizi milioni 50 za kila Kijiji. Nauliza, inapozungumziwa hapa kama ndiyo kwanza imeanza inakuwaje? Tulikuwa na hela za uwezeshaji kwa wanawake kuanzia enzi za Mwalimu Nyerere, zikaja mabilioni ya Kikwete, lakini zikishatolewa hivyo hakuna ufatiliaji, nendeni kule kwenye zile benki, achene kuziachia benki zinateseka na pesa ambazo zinawekwa kwenye suspense. Naomba Serikali ikadai kupitia Wizara ya Fedha, hatuanzi kwenye clean plate.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo najua kwamba zile zikipatikana na hizi milioni 50 zitakuwa zimekuwa nyingi tutakuwa tumefungua wigo wa kuwawezesha wanawake na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru nisingependa kengele ya pili inigongee. Naunga mkono hoja.