Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara hii muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu kwenye maeneo makuu mawili, yaani nishati na madini. Naomba nianze na Sekta ya Madini ambayo tunajua kuwa, kuna Watanzania wamejiajiri kwenye sekta hii, lakini pia, kuna wawekezaji toka nje wamewekeza kwenye sekta hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Tarime Mjini limebahatika kuwa na migodi midogo kwenye Kata ya Kenyamanyori na Turwa. Wilaya ya Tarime tumebarikiwa kuwa na Mgodi wa North Mara ambao ni mkubwa na muwekezaji wa kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya uwekezaji wananchi walikuwa wakifanya uchimbaji mdogomdogo, lakini baada ya uwekezaji ule wamepata adha kubwa sana, hawana maeneo yaliyotengwa dhahiri kwa ajili ya kuwapa maeneo ya kuchimba bali wameendelea kuuawa pale wanapokuwa wameenda kuona chochote kwenye mabaki (vifusi).
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali na mgodi iliahidi ndani ya Bunge hili Tukufu wakati nilipotaka mkakati wa Serikali kutatua wimbi la mauaji ya Watanzania kwenye huo mgodi 2011, waliahidi kutenga maeneo pamoja na kumwaga vifusi vile kwenye maeneo ya wananchi, pamoja na ku-support vikundi mbalimbali ili vijishughulishe na ujasiriamali kuweza kukukuza uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yalisemwa na kurudiwa na Mheshimiwa Nagu, aliyekuwa Waziri wa Uwekezeaji, Mheshimiwa Wasira aliyekuwa Waziri wa Mahusiano na Uratibu na Mheshimiwa Ngeleja aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini. Ni vyema sasa Serikali ikatimiza haya kwa wananchi na Wilaya ya Tarime na Watanzania waishio Nyamongo na maeneo jirani na North Mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime kuna migodi ambayo wachimbaji wadogo wadogo wanashughulika na uchimbaji wa madini. Maeneo hayo ni Nyabhori na Kebaga, Kata ya Kenyamanyori na Mgodi mwingine ni ule wa Bajeti ambao upo mpakani mwa Turwa na Kenyamanyori. Kwa ajili ya kuboresha au kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji hawa wadogo ni muda muafaka Serikali kuhakikisha hizi ruzuku za zaidi ya bilioni 500 zinawanufaisha walengwa na sio matajiri wachache wanaojivisha joho la uchimbaji mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo wadogo ambazo naomba Serikali kujitahidi ndani ya bajeti ya mwaka huu waweze kupatiwa ruzuku, sambamba na vifaa muhimu vya kurahisisha uchimbaji. Changamoto ya kwanza ni juu ya teknolojia inayotumika kuchimba madini, ni ya kienyeji ambayo ni hatarishi sana kwa maisha yao; mfano kuchoronga miamba inabidi watumie nguvu nyingi badala ya morden equipments.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni changamoto ya maji. Aina ya uchimbaji ni underground ambapo unakuta water table ipo juu sana, hivyo inawawia vigumu kufanya shughuli za uchimbaji sababu ya maji na ikizingatiwa vitendea kazi vyao ni duni sana. Ni rai yangu sasa, Serikali itambue maeneo haya na kutoa ufadhili wake kwenye mashine za kuvutia maji kama vile motor, generator na waweze kutoa kwenye vikundi mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ni miundombinu mibovu ya barabara kuelekea kwenye migodi hii. Nashauri Waziri akae na Wizara husika kuweza kushawishi ujenzi wa barabara angalau kwa ngazi ya changarawe ukizingatia migodi hii inachangia kwenye pato la Serikali kupitia leseni za uchimbaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine lenye changamoto kubwa ni juu ya kuweza kupata mitambo ambayo hupima udongo na miamba, ili kujua upatikanaji wa dhahabu au madini mengine. Maana kwa sasa wachimbaji wadogo wadogo wanajichimbia kienyeji na kwa kubahatisha tu na hivyo kujikuta wanapoteza nguvu kazi nyingi sana na haina ufanisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Wilaya ya Tarime tumekuwa hatupatiwi sehemu ya mrahaba toka ACCACIA, kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa kutoa kiasi cha fedha ambacho hutumika kuleta maendeleo ya kijamii. Baadhi ya maeneo ya huduma za jamii ambazo ACCACIA wanapata ndani ya Mji wa Tarime ni Hospitali ya Mji, soko, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Uhamiaji, Stendi, Mahakama, hivyo kwa kuwa wafanyakazi wa ACCACIA wanapata huduma tajwa hapo juu ni dhahiri kuwa ACCACIA wana wajibu wa kuhakikisha Halmashauri yetu ya Mji wa Tarime inapata huduma muhimu za kijamii pamoja na mrabaha toka mgodi wa North Mara. Mji wa Tarime una ukosefu wa maji na barabara za mitaa ni mbovu mno.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mchana huu nichangie katika Sekta ya Nishati ya Umeme; Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa asilimia zaidi ya 70 hawana nishati ya umeme. Halmashauri ya Mji wa Tarime ina mitaa 88, ambapo kiuhalisia kuna kata nne ambazo zipo na vijiji na hamna nishati ya umeme kabisa. Kata hizi ni Ketare, Kenyamanyori, Nandoto, Nkende na baadhi ya maeneo ya Kata ya Turwa na Kata ya Nyamisangura.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishapeleka barua kuelekeza maeneo yenye uhitaji mkubwa wa umeme, hivyo naomba kujua kama REA Phase III imeyafanyia kazi na ukizingatia Kata ya Kataer, Nyandoto na Kenyamanyori wanajihusisha sana na kilimo ambacho kitasaidia kwenye dhana nzima ya Tanzania ya Viwanda, tuweze kusindika mazao yetu, kufungua viwanda vidogo vidogo. Kata ya Nkende ndio yenye soko la Kimataifa ambalo linajengwa pale, pia kuna uwanja wa ndege ambao unatumiwa na watalii waendao Nyamongo na hata Viongozi wa Serikali na kisiasa, hivyo taa ni muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Kata ya Nkende ndiyo yenye Mnada wa Magera ambao Serikali imeahidi kuufufua. Pili, ni katika Kata hii ya Nkende ndiyo tuna machinjio ya kisasa, ofisi ya Uhamiaji inajengwa karibu na Mgena Airport na Remague East Africa Market, lakini pia wajasiriamali wadogo wadogo wanategemea nishati hii ya umeme ili kuendesha shughuli zao za kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, ijulikane kuwa mahitaji muhimu ya kijamii, kama shule za sekondari na msingi, hospitali, vituo vya afya, zahanati, vituo vya polisi, viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao; hivyo, naomba sana Wizara hii itoe kipaumbele katika Halmashauri ya Mji wa Tarime ambayo ni Makao Makuu ya Wilaya ya Tarime. Hivyo nishati ya umeme ni ya muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba Wizara hii ichukue hatua ya kuhakikisha hakuna ukatikaji wa umeme mara kwa mara bila kutoa taarifa kwa mteja/wateja kitu ambacho husababisha uharibifu wa vifaa vinavyotumia umeme na kusababisha hasara kwa mlaji. Utolewe Waraka toka ngazi ya Wizara ukiamrisha uboreshaji wa utoaji wa nishati ya umeme bila kuleta madhara kwa mlaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha kwa kutoa ushauri kwa Serikali kuhakikisha fedha za maendeleo zilizotengwa zitumike kwa ajili ya bajeti iliyotengwa ikiwa ni pamoja na kutoa elimu mbadala kwa wachimbaji wadogo wadogo, ili wapate elimu mbadala kwa uchimbaji wenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.