Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hotuba iliyopo mbele yangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa na umahiri wa hali ya juu katika Wizara hii nyeti kwa jinsi wanavayojitoa kulitumikia Taifa hasa katika kusimamia huduma ya umeme kwenye maeneo yote ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, naomba kuchangia katika huduma ya umeme vijijini (REA). Huduma hii ni nyeti na imelenga kusambaza umeme kote nchini, lakini zipo changamoto kwa baadhi ya maeneo nchini. Mfano, katika Jimbo langu la Kilindi lenye ukubwa wa sm2 za mraba 6,125 vijiji 102 na kata 21 ni vijiji 24 tu ambavyo vimepata umeme, tena ni maeneo ya Bura. Je, Waziri na Wizara kwa ujumla, ni lini vijiji vilivyobaki vitapata umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa yapo maeneo yenye huduma za kijamii hatuna umeme, mfano zahanati, shule za sekondari na shule za msingi. Ni imani yangu Serikali italitazama suala hili katika awamu ya tatu ili maeneo nyeti yaliyobaki yapate umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika Wilaya ya Kilindi kuna tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara, hali hii imetokana na umeme mdogo, miundombinu chakavu na ukosefu wa transformer. Umeme uliopo ulilenga kutoa huduma kwa wananchi wachache na wakazi 300,000. Nishauri hatua za haraka za dhati zichukuliwe ili wananchi wapate huduma hii kwa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia juu ya sheria ya utoaji wa leseni kwa wachimbaji wa madini. Sheria hii imesababisha migogoro ya mara kwa mara kwa kuwa Sheria hii ya Madini na Sheria ya Ardhi zinafofautiana. Mwenye leseni anapotaka kuchimba madini ni lazima akubaliane na mwananchi aliye katika eneo husika kwa ajili ya fidia. Sasa, inakuwa vigumu mwananchi kuondoka eneo hilo pale anapojua dhahabu au aina nyingine ya madini yamegundulika eneo hilo, hususani pale inapotokea fidia inayotolewa ni ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna changamoto kwa Ofisi ya Madini ya Handeni inayohudumia Wilaya ya Kilindi kutoa leseni kwa watu waliopo nje ya Kilindi na kuwaacha wazawa wa wilaya husika. Hali hii imechangia migogoro ya mara kwa mara. Naishauri wizara isogeze huduma ya ofisi wilayani Kilindi, naomba jibu kwa Wizara husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia kitabu chote cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijaona sehemu ya hotuba yake inayoonesha dhamira ya Serikali katika kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo katika Jimbo la Kilindi. Naomba majibu ya kuridhisha kutoka kwa Mheshimiwa Waziri. Aidha, kama Serikali ikitoa ruzuku basi fedha hizo hazifiki kwa walengwa. Nashauri kila Mbunge anayetoka kwenye eneo lenye madini ahusishwe katika kusimamia zoezi hili ili walengwa wanufaike na nia nzuri ya Serikali katika kuwasaidia wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuchangia hotuba hii juu ya kutokuwa na ofisi yenye hadhi ya wilaya, kwa maana ofisi ya TANESCO. Watumishi wa TANESCO kiukweli ni wachache, hawana vitendea kazi vya kutosha kuweza kuwafikia wananchi wenye jiografia ngumu. Naomba Waziri ashirikiane na Shirika la Umeme tupate ofisi bora na watumishi wa kutosha wa kuwahudumia wananchi wa wilaya hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa jitihada kubwa alizofanya za kufanikisha upatikanaji wa mkataba wa kujenga bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga litakalosaidia kukuza uchumi wa Mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla; ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa ajira wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.