Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuweza kunipatia fursa hii kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba Wizara hii ndiyo imeshikilia uchumi wa Tanzania, tukisema Tanzania ya viwanda ina maana Wizara hii ndiyo inatakiwa ifanye vema. Tukienda hata kwenye sekta ya afya, tumeshuhudia mikoani hasa katika Wilaya ya Tarime kwenye vituo vya afya ambavyo vipo kando kando ya mji wanawake wakienda kujifungua vituo hivi vinatumia tochi kuwazalisha wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea kwamba Wizara hii iweze kweli kuonesha kama ilivyosema kwenye hotuba yake kwamba asilimia zaidi 98 zimekwenda kwenye fedha za maendeleo na nje ya hizo 98 ambazo ni trilioni 1.54; trilioni 1.32 zinaenda kwenye nishati. Kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba itaenda kuwatendea haki Watanzania kwa kuwapatia nishati mbadala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa kwenye madini; Halmashauri ya Mji wa Tarime au Wilaya ya Tarime imebarikiwa kuwa na madini pamoja na kwamba Profesa alisema dhahabu siyo kitu siku hizi, lakini bado tunaithamini dhahabu na tukiitumia vizuri inaweza ikatusaidia sana kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime ina migodi midogo midogo ya Nyabori, Kebaga na Buguti. Hii migodi ya Kebaga, Nyabori na Buguti; mgodi wa Buguti bado ulikuwa na leseni ya Acacia ambao walisema inakwisha Disemba. Kwa hiyo, natumaini kwamba kama itakuwa imekwisha basi watapewa wachimbaji wadogo wadogo ambao tayari wapo field.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata mwanzoni mwa mwaka huu nilimwambia Profesa wakati ameweka ziara ya Tarime atembelee ule mgodi nafikiri nafasi haikumtosha. Hao wachimbaji wadogo wadogo wanapata changamoto nyingi sana na tukirejea Sera ya Wachimbaji Wadogo ya 2009 ambayo ilielekeza kwamba waweze kupatiwa mitaji kwa maana ya ruzuku ambayo wameonesha kwamba wanaitoa lakini ruzuku hizi ambazo wanazitoa hazifuati utaratibu au utaratibu wake ni mbovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, walengwa siyo wale wachimbaji wadogo wadogo, wale ambao tunawa-target bali ni wajanja baadhi wanakuja wanajivisha umbrella ya wachimbaji wadogo wadogo, wana-benefit kwa hizi fedha na wale ambao ni targeted group hawapati. Kwa hiyo, ningependa sana utaratibu huu uweze kufuatiliwa vizuri, waweze kupata wale Watanzania ambao kweli ni wachimbaji wadogo wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine tuna GST kwa maana ya Geological Survey of Tanzania (Mawakala wa Jiolojia) hawaendi kuhakikisha wanasaidiana na hawa wachimbaji wadogo wadogo kujua kwamba sehemu fulani kuna madini. Kwa mfano, sasa hivi wachimbaji wa Buguti na Nyabori ambao nimewaainisha hapa wanachimba kwa kubahatisha; kwanza wanatumia vifaa duni, wanatumia nguvu zaidi kuliko teknolojia ya kisasa; lakini wakifika chini wanakuta hakuna madini wanahama tena wanakwenda kwenye shimo lingine hivyo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa hii GST ijielekeze kule iwasaidie hawa wachimbaji wadogo wadogo waweze kujua bayana kwamba nikichimba hapa nitakwenda kukutana na madini. Ukizingatia kwa mfano Buguti water table ipo juu sana, wanatumia vifaa duni, kutafuta jenereta na kuanza kutoa maji na kuchimba na hakuna umeme maeneo hayo yote ambayo nimeyaainisha, zile Kata hazina umeme kabisa. Hao wachimbaji kwanza hawajaweza ku-benefit na hiyo ruzuku wanajikongoja kwa kuchangishana vikundi vile, lakini wakichimba bado hawawezi kupata kinachostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba huwa kuna Wakaguzi wa Madini ambao wanakagua teknolojia ya uchimbaji. Hawa watu hawawafikii hawa wachimbaji wadogo wadogo kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, unakuta hawa wachimbaji hawapati ushauri mbadala kutoka kwa hawa wataalam wetu. Ningependa kuelekeza Wizara hii kama tumeamua kuwasaidia hawa wachimbaji wadogo wadogo tuhakikishe kwamba tunawafikia, tunashauriana nao, ikiwezekana tunawapatia elimu mbadala na tunawapatia na vifaa ili waweze kuchimba kwa teknolojia ya kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachosikitisha zaidi kupitia uchimbaji mdogo mdogo ule uchenjuaji wa madini mineral processing mnaita, unakuta wanachukua yale madini, wanatia mercury ili kuweza ku-process na kupata ile dhahabu yenyewe; hii inawaua Watanzania kidogo kidogo, leo hata ukienda kwenye haya maeneo ya dhahabu au madini , utakuta kuna watu vipofu, maana yake haya madini yakiingia kwenye damu yana affect zile chromosome macho yataharibika. Unakuta watoto wanazaliwa wana vichwa vidogo, unakuta wengine ngozi zao ukiziona hazitamalaki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika huu uchimbaji mdogo mdogo tusipowekeza vizuri, tukawapa kinu cha kufanya direct smelting mwisho wa siku tunawaua hawa Watanzania, baada ya muda mchache Watanzania wengi wanakufa kwa sababu wanatumia zile mercury. Leo ukienda Buguti, ukienda Kebaga, ukienda Nyabori unawakuta akinamama wengine hata ni wajawazito wanashika shika ile mercury, inawapa direct effect kwa kiumbe aliyepo tumboni ,lakini na yeye mwenyewe after five, ten years wanafariki dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fanya research kwa wote nenda Geita, nenda Nyamongo, njoo kwenye hii migodi midogo midogo pale na Profesa unajua mercury effect yake, lakini wanatumia. Hivyo basi tuwawezeshe, tuwape modern instruments za kufanya hiyo process ya madini wasitumie mikono yao moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Nyamongo kabla sijakwenda kwenye nishati. Nyamongo kwa kweli na naongea hii kama natokea Tarime, tumekuwa tukiongea huku kwa muda mrefu sana ule mgodi siyo neema kwa watu wa Tarime bali ni majonzi kwa watu wa Tarime na hata Watanzania wengine ambao wanafanya shughuli zao pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba ukienda nchi za wengine kama kuna migodi ni neema, hivi leo kweli ukija Tarime huwezi ukaona reflection kwamba kuna mgodi ambao unatoa dhahabu ya kutosha kilometa kadhaa kutoka Tarime Mjini, hatuna barabara za lami, wamejitahidi ndani ya ile Kata ya Matongo pale ndiyo kuna shule wamejenga na kile kituo cha sungusungu, lakini hata ukienda hospitali ile ya mji ambayo mnaisema ambayo ndiyo inatoa huduma hata kwa asilimia kubwa kwa Wilaya nzima ya Tarime haioneshi uhalisia kwamba kuna mgodi upo kwenye hii Wilaya ya Tarime.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukiangalia huduma za jamii maji walikuwa wanatoa kwa kupeleka ile buldoza lidumu la maji lile, ina maana hawajawachimbia kuhakikishia kwamba wanawapa maji ambayo yapo salama. Kwa hiyo naomba sana kikubwa mwaka 2011 baada ya watu zaidi ya sita kuuawa Nyamongo aliyekuwa Waziri wa Nishati Mheshimiwa Ngeleja, Mama Nagu Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji na Mheshimiwa Wasira walikuja Nyamongo wakawaahidi wale Watanzania kwamba watawapa maeneo mbadala ya kuchimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wakaongea na mgodi na wakawaahidi kwamba watachukua yale mawe wawe wanakuja kuwamwagia kwenye maeneo yao, maana wakienda kuokota mawe mnawapiga risasi. Wameshindwa kutimiza yale ambayo waliahidi, kwa sababu naamini Wizara hiyo ni institution hata kama ametoka yule Waziri amekuja mwingine, mnabukua ma-file mnaona mliahidi nini kwa wale Watanzania mkawatimizie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la nishati; Jimbo la Tarime Mjini au Wilaya ya Tarime kwa asilimia zaidi ya 70 wananchi wake hawana umeme. Leo tunavyoongea Mheshimiwa Profesa Muhongo, tumeshaleta mapendekezo yetu kupitia REA l pia na hizo njia nyingine za kuweka umeme kwa hawa Watanzania. Kama tunataka kukuza uchumi wetu tuhakikishe tunasaidia, mathalani Tarime Mjini Kata ya Nkende, Nyandoto, Kitale na Kenyamanyoli asilimia zaidi ya 98 hawana umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Nkende kuna soko tunalijenga la Afrika Mashariki hamna umeme, kuna uwanja wa ndege pale, kuna mnada wa Magena, lakini kuna machinjio ya kisasa Nkende na huduma zingine za jamii. Zaidi kwa upande wa pili wa Tarime ni Kenya; wenzetu Kenya ukija usiku ni taa zinawaka tu, ukija usiku upande wa Tanzania ni giza kama vile ni pori. Kwa hiyo, ningependa kuwaomba sana hizi trilioni 1.32 Tarime mtukumbuke, mtuletee hii nishati ya umeme, sisi ni wakulima, sisi ni wafugaji tuweze kusindika mazao yetu, tuweze kukuza uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna Watanzania wengine ni wajasiriamali wadogo wadogo wamewekeza, leo mtu mwenye saloon kama hana umeme hawezi kumudu kununua jenereta, leo wale wafanyabiashara wadogo wadogo hawawezi kumudu bila umeme. Tukiwaza Tanzania ya viwanda, pia tuwaze Tanzania ya wajasiriamali wadogo wadogo ambao nishati ya umeme ndiyo mbadala wa kuweza kuwakomboa Watanzania. Tuwaze huduma za jamii kama shule, tuwaze huduma za jamii kama hospitali, tuwaze huduma za jamii zinginezo, magereza na vituo vya polisi bila umeme huko vijijini, hata hao wahalifu mnakwenda kuwaweka pamoja na Polisi mnategemea nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba sana Serikali hii ya CCM kupitia kwa Profesa Muhongo wawekeze na nina imani labda alikaa hawajampunja bajeti yake na akajiridhisha kabisa hii trilioni 1.32 inatosha kuhakikisha wanaleta umeme zaidi ya asilimia 70 kwa Watanzania ili tuweze kuondokana na umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa lolote lile lenye nishati mbadala ya umeme utaona uchumi wake utaji-reflect kwa sababu umeme ndiyo kila kitu. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atuangalie Tarime, Kata nilizozitaja za Kenyamanyoli na mgodi ukiwapelekea umeme hiyo migodi itaenda kufanya kazi bila kutumia jenereta. Apeleke umeme Kitale, Turo, Nyamisangula, Nyandoto na kwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.