Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa. Vilevile niwashukuru wananchi wa Wilaya ya Siha kwa kuniamini kwamba naweza nikawawakilisha. (Makofi)
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Jafo anamjua Mwanri vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kwa kusema kwamba kama kweli tunataka kuitoa Tanzania kutoka sehemu moja kwenda nyingine ni lazima tuwe na tafakuri ya juu sana katika kuamua ni namna gani tunatumia rasilimali za nchi yetu. Hata hivyo, nimshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa sababu kwa muda mrefu watu wamekuwa wakisema kwenye jengo hili kwamba kuna ufisadi, kuna ubadhirifu wa rasilimali za nchi, yeye amekuwa shahidi namba moja, twendeni tukapambane na huo ufisadi. Amekuwa shahidi yetu kwamba yaliyokuwa yanasemwa kwa miaka yote ni kweli kabisa. Sasa wote kwa umoja wetu bila kujali vyama vyetu twendeni tujikoki silaha zetu tukapambane kwa ajili ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuzungumzia ardhi kwa Wilaya ya Siha. Wilaya ya Siha ina eneo kubwa la ardhi ambayo haitumiki inaitwa ardhi ya Serikali ni zaidi ya heka 32,000, zipo tu na hakuna matumizi yoyote. Vilevile ardhi ambayo haiendelezwi vizuri inayosemekana Ushirika wameishika ni zaidi ya heka 14,000 na ardhi ambayo inasemekana wawekezaji wamemiliki ni zaidi ya heka 39,000. Ukijumlisha heka zote unakuta kuna heka 120,000 na zaidi. Unakuja kugundua ardhi hiyo kwa heka ni zaidi ya wananchi wa Wilaya ya Siha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Lukuvi, Waziri wa Ardhi na Mawaziri wengine wahusika nimewaeleza na wamenisaidia, wamenisikiliza vizuri. Niseme karibuni Wilaya ya Siha, karibuni Mkoa wa Kilimanjaro kwa sababu ni mkoa mdogo sana na matumizi yake ya ardhi yanatakiwa yaangaliwe kwa jicho tofauti na kwingine ambako kuna mapori makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niombe, tuna shamba ambalo lina ukubwa wa heka 3,429 linaitwa shamba la Gararagua. Ni shamba ambalo linasemekana linamilikiwa na KNCU. Shamba lina miundombinu ya maji ndani yake ambayo ndiyo backup ya maji ndani ya Wilaya ya Siha na kwenye Halmashauri lakini shamba hili anauziwa mwekezaji ambaye anakuja kulima maparachichi na mwingine kufuga kufuga kuku. Tuna uzoefu na huo uwekezaji wa maparachichi, nimeuliza ndani ya Wilaya ya Siha unaiingizia Halmashauri shilingi ngapi hamna chochote zaidi ya maparachichi yaliyoharibika kulipiwa ushuru wa geti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji huyu anataka kuongezewa eneo lingine ukipiga bei kwa kila heka yeye anaenda kuchukua kwa Sh.2,000,000 kwa heka moja. Ni heka moja yenye maji ndani yake thamani yake ni kubwa mno. Tutafute tafakari ya juu ya namna gani tutatumia hiyo ardhi kwa maslahi ya Taifa letu. Kwa sababu tukimjenga mwananchi wa chini ili aweze kuzalisha vizuri, alipe kodi na akapata ardhi nzuri ndivyo ambavyo tutaweza tukasema tunaweza kutekeleza bajeti tuliyonayo kwa sababu hatutegemei hela kutoka Serikali Kuu, tunategemea hela kutoka kodi wanazolipa wananchi wa chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nionye tu kuhusu shamba hili, mwekezaji ambaye alipewa na KNCU kwa muda wote wa miaka mingi toka nikiwa mtoto akichangisha Sh.50,000 kwa kila mwananchi kukodisha kulima mazao. KNCU wanasema wanataka kuuza hili shamba kwa sababu wana deni la Sh.4,000,000,000 wanalodaiwa na CRDB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msimamo wetu kama Wilaya na Mkoa kabla ya kusema unauza shamba hili, tujiulize aliyechukua Sh.4,000,000,000 kutoka Halmashauri kwa nini alishindwa kurejesha? Kama ni jipu litumbuliwe kabla ya kwenda kusema unaenda kurudisha hela za CRDB. KNCU inajulikana kwamba imekuwa kidonda ndugu kwa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuua zao la kahawa na kufanya mambo mengine ambayo wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro hawaridhika nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuonyesha kuna tatizo hapa, nimetembelea mashamba zaidi ya 23 niliyoyazungumzia lakini nilipofika katika hili shamba la Gararagua mwekezaji aliyeko pale aliagiza walinzi wake wanizuie nisiingie kwenye shamba. Nilipoingia alienda Polisi kusema nimemwingilia shambani kwake. Cha kusikitisha amepiga simu toka Dar es Salaam, Polisi na Serikali ya Wilaya ya Siha ikawa inakimbiakimbia inanitafuta mimi, nikajiuliza kazi ya Mbunge ni nini? Sisi tumechukua silaha zetu tunakwenda kutumbua majipu watu wachache ambao wanahisi majipu yao tunaenda kuyatumbua wanaiamsha Serikali yetu inapingana na sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa kwenye Wilaya au Mikoa yetu kuna shida moja mnapokuja ziara. Nashauri muanzishe utaratibu mzuri kama aliouanzisha Mheshimiwa Mwigulu kwamba kabla ya kwenda eneo fulani anaonana na watu wa eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye eneo la la elimu. Nielezee kitu cha tofauti, imesemekana elimu ni kitu ambacho tunaenda kukiangalia kwa jicho lingine. Nimshukuru Mheshimiwa Ndalichako, naamini unaweza ukaenda ukafanya hilo lakini tuangalie pamoja na kwamba tutaboresha shule, tutaboresha kila kitu lakini tuna eneo ambalo tunatakiwa tuliwekeze nalo ni eneo la mtoto na uwezo wa akili wa mtoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, twendeni tuwekeze katika lishe ya watoto wetu ili tunapowapeleka shule basi ukuaji wa ubongo uwe umekua vizuri ili aweze kupata kile kinachotakiwa. Kwa sababu wenzetu wametuzidi kiteknolojia siyo kwa sababu tu wana rasilimali nyingi au wana vitu vingi ni kwa sababu wana watu wenye uwezo wa kufikiri zaidi ya kufikiri katika ubongo (thinking beyond the brain). Tunatakiwa na sisi tuanze kujenga watu wenye uwezo huo ili tuweze kuwekeza kwenye teknolojia. Kama hatujawekeza vizuri kwenye ubongo wa mtoto kwa maana ya ukuaji pamoja na elimu nzuri hata kama tutajenga vyuo vikuu vizuri namna gani hatutakuwa na ubongo wa kuweza kuelewa teknolojia ambayo tunaitaka tuitengeneze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala kilimo. Wilaya ya Siha ni Wilaya mojawapo iliyozunguka Mlima Kilimanjaro lakini utalii huo haufaidishi Wilaya ya Siha na vilevile tunahitaji tuboreshe miundombinu iliyozunguka Wilaya hiyo. Ukiangalia barabara ambayo inapitia ile Kisimiri Corridor kwenda Londrosi Gate imechimbika sana na Rais ameahidi kuishughulikia na nasikia kwamba tayari procurement imeshafanyika kwa ajili ya kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami imebaki kusainiwa mkataba. Naomba hilo suala liharakishwe kwa sababu magari yamekuwa yakianguka katika barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuboreshe eneo la kilimo, wananchi wamekuwa wakizalisha mazao mengi lakini wakati wa mavuno mipaka yetu imekuwa ikufungwa. Nina zao moja katika Jimbo la Siha ambalo wananchi wako tayari kulima hata mashimo wanyeshee nalo ni zao la nyanya. Cha kushangaza wanapovuna mahindi mengi wanakosa pa kuuza. Naomba ikiwezekana wananchi wakivuna waruhusiwe kuuza popote wanapoweza kuuza ili kuhamasisha mazao ya chakula kuzalishwa na hata wananchi wawe tayari kuchimba mashimo watafute maji ili wanyeshee na tutaweza kuzalisha chakula kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya yaSiha wamekuwa wakizalisha zao la kahawa. Naomba Waziri wa Kilimo tusaidiane…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha
kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umemalizika.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)