Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Prof. Norman Adamson Sigalla King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DKT. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuchangia, naomba nichukue nafasi hii kipekee kabisa kumshukuru Mungu kwa sababu ya kutuwezesha sisi sote kushinda uchaguzi mwaka jana na kuingia kwenye Bunge hili. Kipekee kabisa nipongeze Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya na Vyombo vyao kwa kusimamia uchaguzi huo vizuri. Kwa kufanya hivyo, wameniwezesha mimi na mdogo wangu Mchungaji Msigwa, kuingia kwenye Bunge hili. Ahsante sana Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kidogo katika Mpango uliowasilishwa. Kwanza, natambua kabisa kwamba yako maeneo mengi ambayo Mpango umejielekeza na hasa upande wa barabara na reli. Mimi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, naomba nisisitize tu kwamba sisi Watanzania tunaamini kwamba uboreshaji wa Reli ya Kati ile tunayoijua yaani ya kwenda Kigoma – Mwanza baada ya pacha ya Tabora ndiyo tunayoisema na matawi yake ya kwenda Mpanda. Mikoa kumi na tano itanufaika na suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze kwa ufupi, Tanzania ilivyo na hasa Wilaya ya Makete na Mkoa wa Njombe, ni Mkoa ambao ni tegemeo kubwa sana kwa sababu ya uchumi wa Tanzania na hasa uzalishaji wa mazao ya chakula. Naomba sana barabara inayotoka Njombe - Mbeya kupitia Makete ipewe kipaumbele kwa sababu hata Ilani ya CCM imeiweka barabara hii ni barabara ya kwanza. Umuhimu wa barabara hii si tu kwa sababu Norman Sigalla King anatoka Makete ni barabara muhimu kwa maana ya uchumi wa Tanzania kwa sababu Hifadhi ya Kitulo ndiyo hifadhi pekee ya maua Afrika. Hifadhi hii ili iboreshwe ni lazima miundombinu ya barabara za lami iwe bayana na hii itasaidia kukuza utalii ndani ya hifadhi hii na si tu kukuza utalii lakini pia kuboresha uchumi wa Wilaya ya Makete. Kwa sababu Wilaya ya Makete pamoja na uchumi wa mazao ya chakula pia ndiyo Wilaya ambayo inaongoza baada ya Mafinga kwa mazao ya mbao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni jambo la muhimu sana, niishukuru Serikali ya CCM kwa kazi nzuri inayoifanya ya kuboresha elimu. Wilaya ya Makete pale tuna Chuo cha VETA, bahati mbaya sana yako madarasa lakini hakuna mabweni. Wilaya ya Makete kwa jiografia yake haiwezekani wanafunzi wa kutoka Tarafa za Matamba, Ikuo, Lupalilo, Ukwama, Bulongwa kwenda kusoma kwenye chuo kilichoko Iwawa-Makete. Ni muhimu sana Serikali ijenge mabweni ili kunufaisha wananchi wa Tarafa zote ikiwemo Taarifa ya Magoma. Hili nimeliwasilisha kwa Waziri mhusika, naomba sana kwenye Mpango wetu wa Maendeleo tufasili kwa vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa elimu pia naomba nisisitize jambo moja. Mtihani tulionao sasa ukisikiliza hotuba ni kana kwamba muhimu kwa Watanzania ni kupata shahada ya kwanza, ya pili ama ya tatu. Mtihani tulionao sasa ni aina ya elimu tunayowapa watoto na watu wetu. Sote tunajua nguvu ya uchumi wa Tanzania ni kilimo, asilimia 77 ya watu wetu wanategemea kilimo. Hata hivyo elimu yetu kuanzia darasa la kwanza mpaka chuo kikuu hakuna mahali ambapo mwanafunzi anakutana na kilimo. Ni hatari sana!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wamarekani na nchi zilizoendelea nguvu yao ni kwenye teknolojia ndiyo maana mtoto wa Kimarekani wa miaka nane au kumi anacheza na komputa, ana-feed data na analipwa. Kwao Wazungu wanasema hiyo siyo child labour lakini Mwafrika, Mtanzania akibeba jembe akiwa na miaka kumi na mbili, kumi na tatu tunamfundisha kilimo ambacho ndiyo nguvu yetu tunasema child labour. Tunaingia kwenye ugonjwa huu, matokeo yake tutakuwa na wanafunzi wanao-graduate kwenye level ya digrii ya kwanza, ya pili na ya tatu lakini hawana mahali pa kutumia elimu hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali, baada miaka ile mitatu ya kujua kusoma na kuandika kwa watoto wetu ni muhimu sana watoto hawa wajifundishe ABC ya kilimo, siongelei kilimo nadharia, kilimo vitendo. Mtu anatoka Kanda ya Ziwa basi ajue akifika darasa la saba ni jinsi gani ya kutumia mbolea kulima pamba, kama anatoka Nyanda za Juu Kusini kwa mfano ajue kwa nini tunatumia DAP na kwa nini tunatumia urea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dozi hiyo ya course inaongezewa uzito anapomaliza kidato cha Nne ili tuwe na Watanzania ambao wakihitimu kidato cha nne hawana haja ya kutafuta shahada maana elimu waliyonayo inatosha kujitegemea. Nafikiri hili Wizara ya Elimu iliangalie kwa namna ya kipekee sana maana vinginevyo tutajuta kwa sababu tutakuwa na watu wengi walio-graduate, lakini hawana mahali pa kutumia elimu hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kusisitiza umuhimu wa Bwawa la Lumakali. Kaka yangu Mheshimiwa Profesa Muhongo yuko hapa. Mto wa Lumakali ambao uko Bulongwa, Wilaya ya Makete, ni kati ya mito michache katika Tanzania ambayo haipungui maji kwa miaka 40 sasa ya utafiti. Document ambayo ni official ya TANESCO inaonyesha kwamba umeme unaotakiwa kuzalishwa kwa kutumia mto ule ni megawatts 640 hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali itekeleze mradi wa Lumakali kwa sababu utasaidia sana kutoa ajira kwa wananchi wa Makete, Mbeya na Njombe kwa sababu ni bwawa kubwa lakini pili utasaidia sana kuongeza umeme wetu. Mheshimiwa kaka yangu Profesa Muhongo chondechonde, naomba sana Mto Lumakali upewe nafasi yake ya kipekee kabisa ili Wilaya ya Makete ipate kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe hotuba yangu kwa kuongelea umuhimu wa kuunganisha barabara ya kutoka Ludewa - Mlangali. Niipongeze Serikali kwa sababu ya kufungua barabara hiyo lakini ni vizuri ifunguliwe kwa kiwango cha lami kutoka Mlangali - Lupila kutokea Ikonda - Makete, kutoka Chimala - Matamba - Kitulo - Mbeya, kutoka Mbeya - Ishonje - Makete - Njombe na kutoka Makete – Bulongwa – Iniho - Ipelele - Isonje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mungu akubariki na naunga mkono hoja. (Makofi)