Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Philipo Augustino Mulugo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupewa nafasi hii ya kuchangia Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwanza, napenda niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Songwe, kwa kunirudisha tena kuwa Mbunge wa awamu hii ya pili. Nataka niwahakikishie kwamba, nitawasaidia sana namna ya kufuatilia huduma zao za afya, elimu, umeme, maji na mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari jambo ambalo nilikuwa nimeahidi kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 kwamba, nitahakikisha napigania kupata Mkoa mpya na Wilaya mpya ya Songwe sasa nimepata, sasa ni hapa kazi tu. Nitahakikisha mambo yanakwenda vizuri. Napenda vilevile nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kipindi kifupi takribani kama miezi sita nchi imebadilika, hali ya hewa imebadilika kabisa Tanzania, tunaanza kuiona Tanzania yenye asali japo ndugu zetu hawa Wapinzani wao kama ambavyo wanaitwa Wapinzani hawana zuri, hawana dogo, wao kila kitu ni kupinga. Kwa hiyo, nawashauri Wapinzani mbadilike, hii nchi ambayo tulikuwa tunaitegemea ndiyo hii ya Tanzania nakumbuka kwenye Bunge la Kumi ninyi ndio mlikuwa watu wa kwanza kusema Serikali ni dhaifu, sasa leo Serikali siyo dhaifu, Serikali hii sasa ni imara, naomba mwendelee na ninyi kupongeza jitihada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nirudi katika hoja za wananchi wa Mkoa mpya wa Songwe na Jimbo la Songwe na Wilaya mpya ya Songwe. Tumepata Mkoa mpya, Mheshimiwa Waziri Simbachawene anajua hilo, lakini Mkoa huu mpya Mheshimiwa Simbachawene juzi ama jana wakati naangalia taarifa za habari kwamba, Mheshimiwa Rais ameteua ma-RAS katika kila Mkoa lakini Mkoa wetu wa Songwe tayari Mkuu wa Mkoa amesha-report ameshafika mama yetu Chiku Galawa, lakini sijaona pale kwenye list ya ma-RAS kwamba tumepata RAS naomba hilo Mheshimiwa Waziri ali-note asiweze kusahau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweze kututeulia Katibu Tawala wa Mkoa haraka ili maendeleo vilevile katika Mkoa huu yaweze kwenda haraka sana. Vilevile bado na Wakuu wa Wilaya, Wilaya yetu hiyo mpya bado haina Mkuu wa Wilaya, nadhani hilo liko chini ya vetting na mnaendelea na taratibu hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema daima mikoa mipya na wilaya mpya zina changamoto zake. Naomba Serikali pale mtakapokuwa mnaweka vipaumbele katika bajeti ya maendeleo, basi msisahau kuweka hizi halmashauri na Wilaya mpya pamoja na mikoa mipya kuweka kipaumbele, kwa sababu ukiangalia kama Halmashauri yangu mpya ya Songwe pale Makao Makuu ya Halmashauri maji ni tatizo na miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna nyumba ya Mkuu wa Wilaya, hakuna nyumba ya Katibu Tawala, hakuna nyumba ya Maofisa wa Serikali, hakuna nyumba yoyote ya Kiserikali ambayo sasa wale viongozi wakija watakuja kuhamia pale maana yake Mkuu wa Wilaya atakaa hotelini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliomba special fund milioni kama 403 tuletewe mapema ili tuanze maandalizi, lakini mpaka sasa hatujapata hizo fedha. Hizo fedha zingekuja kukarabati jengo ambalo liko pale Mkwajuni ili Mkurugenzi akija aweze kupata ofisi, Mkuu wa Wilaya aweze kupata nyumba pamoja na Mkuu wa Mkoa pale Vwawa aweze kupata nyumba. Fedha hizo Mheshimiwa Waziri hatujapata mpaka sasa. Kwa hiyo, naomba jambo hilo lichukuliwe katika uzito wa namna yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba vilevile nipongeze Kamati ya Mgao wa Mali pamoja na Watumishi katika Wilaya ya Chunya. Nampongeza sana kwanza Mkurugenzi dada Sophia Kumbuli alishirikiana sana na ile Kamati. Mimi mwenyewe nadhani last week hamkuniona hapa nilienda kuweka kambi pale Chunya kuhakikisha tunagawa mali vizuri, kugawa magari vizuri, kugawa watumishi vizuri wenye career mbalimbali ili kuona kwamba, Mkurugenzi anaweka mambo vizuri. Kwa kweli, yule mama amenisaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu ile tumefunga mjadala, Baraza la Madiwani limepitisha na jana DCC imekaa, imepitisha kwamba, tumegawa vizuri, kwa hiyo hakuna malumbano wala hakuna mambo mengine yoyote. Kwa hiyo naomba niseme kwamba, limeenda vizuri, sasa ni kazi ya RCC ikae ipitishe na Mheshimiwa Waziri atapata hiyo document waweze kutupatia GN namba haraka sana kwenye Halmashauri mpya ya Songwe. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, vilevile ningemwomba afanye ziara kwenye Halmashauri yangu hii mpya, aje pale Mkwajuni aliniambia hata wakati ule kwamba, atakuja Songwe. Naomba basi atembelee mkoa mpya pale Vwawa lakini vilevile afike na pale Mkwajuni jimboni kwangu aone jinsi hali ilivyo kwenye Halmashauri mpya ya Songwe, ataona ukubwa na umbali kutoka Kata moja mpaka Kata nyingine unakuta ni kilometa 30. Tumeomba kwenye Bodi ya Barabara kwamba, Kata zingine kutoka Kapalala mpaka Ngwala tungeomba zile barabara ziingie kwenye barabara ya Mkoa kuliko kuweka kwenye Halmashauri ambazo fedha zikija, zinakuwa ni kidogo, haziwezi kukidhi mahitaji ya matengenezo. Hiyo ndiyo changamoto yangu iliyopo huko kwenye Mkoa mpya na Wilaya mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie jambo lingine kwenye upande wa Watumishi wa Halmashauri hasa ma-VEO na ma-WEO. Mimi wakati nafanya ziara kwenye jimbo langu kushukuru mwezi Februari nimekutana na changamoto, ukifika vijijini unakuta hakuna VEO, kwenye Kata hakuna WEO, lakini wanasema tuna barua ya Mkurugenzi amemteua Mwalimu Mkuu wa Shule ndiye anakaimu WEO ama anakaimu VEO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hotuba yake amesema kwamba, sasa hivi mapato ya Halmashauri ama mapato ya ndani yatakusanywa na hawa viongozi ma-VEO na ma-WEO kwenye Serikali za Mitaa. Sasa je, tuanze kumtoa mwalimu darasani akakusanye mapato? Naomba suala la ajira la ma-VEO na ma-WEO lifanyiwe haraka ili wale Wakurugenzi wapate vibali tuweze kuajiri haraka angalau vijiji vyetu viwe na viongozi hao ili wakusanye mapato kwa upande wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile nichangie upande wa elimu. Mimi ni mwalimu by professional lakini elimu bure dhana hii nimeichukulia vizuri sana na wananchi wameshaanza kuielewa, lakini ningeweza tu kuishauri Serikali kwenye baadhi ya vipengele. Mheshimiwa Waziri, elimu bure inawafanya hata wazazi wasichangie hata madawati, elimu bure inamfanya mzazi asiweze hata kumnunulia mtoto wake sare, elimu bure inawafanya hata wazazi wasichangie hata michango ya UMISETA, elimu bure inawafanya wazazi waache hata kuchangia mitihani mock.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoka Mbeya juzi tu hapa nilikuwa namuuliza Mwalimu mmoja wa shule ya private kwamba, hivi mock Mkoa wa Mbeya ama mock Wilaya ya Mbeya Mjini ama Vijijini ama Chunya, mnafanya lini? Wakasema mpaka leo hatujapata mwongozo wa mitihani hii ya mashindano ya mock kwenye Wilaya na Mkoa kwa sababu Serikali haina fedha. Zamani walikuwa wanachangia wao wenyewe wanafunzi kutoka kwenye mifuko ya wazazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali kama kweli tumeshaanza kuibeba dhana ya elimu bure, basi fedha zile zijumuishwe pamoja na michango ya mock itafikia mahali shule za Serikali wataacha kufanya real practical kwa sababu hakuna hela. Sasa kama na shule zikianza kutokufanya real practical maana yake ndiyo tunaua sayansi kwenye shule za Serikali. Naomba Mheshimiwa Waziri hili walichukulie kiumakini sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mwalimu najaribu kushauri kwamba, tukikosa mock kwenye shule za Serikali ila tukawa na mock kwenye shule za private huwezi kufundisha bila ya kuwa na zile academic competitions ili angalau wanafunzi waweze kufanya vizuri. Kunakuwa na mashindano ya kitaaluma kwenye shule, sasa tumeyaua hayo halafu baadaye tunasema elimu bure, matokeo ya mitihani yakitoka unakuta shule zinakuwa labda hazijashika namba vizuri, halafu tunaanza kuongea tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana kwenye suala la elimu, mock iweze kufanyika. Mheshimiwa Waziri wa Elimu yuko pale, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Naibu wake hebu jaribuni ili mliangalie, mimi nawashauri; pigeni simu kwa ma-REO wa nchi nzima mseme mock ipo mwaka huu, maana inaonekana mock haipo kwa sababu fedha hakuna. Fedha zile ambazo tunapeleka kwenye Shule za Msingi kama capitation grants hazitoshi kwa ajili ya matumizi ya shule, kununulia chaki, Mwalimu kufanya mikutano na mambo mengine. Kwa hiyo, hawana fedha za mock, hawana fedha za kufanya real practical, naomba hili mliangalie, mimi nawashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nisingependa dakika ziniishie, naomba ushauri wangu uzingatiwe. Ahsante sana.