Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu. Kwanza kabisa, naomba nielekeze mchango wangu kushukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuanza kutimiza ahadi zake ambazo aliahidi kipindi cha kampeni. Aliahidi shilingi milioni 50 kila kijiji, tumeona zimeanza kwenda, tunashukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Shilingi milioni 50 hizi za kila kijiji tumeona wanawapa Baraza la Wawekezaji, ni mpango mzuri sana. Hata hivyo, tunaomba Baraza la Wawekezaji wahakikishe wamepita kata hadi kata ili fedha hizi zifike kwa walengwa.
T A A R I F A....
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yake kwanza naikataa.
Fuatilia vizuri, naona Magufuli anawapa moto na hiyo ni bado. Arusha tumeshachukua kata, tumeshaanza kuchukua mitaa…
Tulieni, tulieni. Mheshimiwa Naibu Spika, ulinde muda wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana jembe Rais Magufuli, Rais wa wanyonge, Rais wa maskini, sasa hivi maskini wote wanaimba Chama cha Mapinduzi kwa sababu ya Rais Magufuli. Hongera sana Rais wetu na Arusha tutarudisha Majimbo kwa hii kasi ya Magufuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kutoa mchango wangu, tunaomba sana hizi shilingi milioni 50 za kila kijiji, Wabunge wa maeneo husika hasa wa Chama cha Mapinduzi tushirikishwe ili tujue zinapoenda na vilevile sisi ndiyo ambao tunajua watu ambao wanahitaji fedha hizi. Tunaomba zile asilimia tano ambazo zilikuwa kwenye Halmashauri kwa ajili ya akinamama na vijana ziendelee kuwepo, siyo shilingi milioni 50 itoke zile zisiwepo, ziendelee kuwepo kama sheria inavyosema.
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze katika suala zima la elimu. Tumeona Serikali ya Chama cha Mapinduzi imesema elimu bure. Mpango huu umesaidia sana watoto wa maskini sasa hivi wanapata elimu. Watoto wengi wa maskini walikuwa wanachukuliwa wakiwa wadogo kwenda kufanya kazi za ndani, lakini sasa hivi tunaona Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeleta usawa kwa watoto wetu na imeleta usawa kwa maskini na matajiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili ni zuri sana ingawa lina changamoto chache. Tumeona baadhi ya shule za kutwa wazazi wanaendelea kutoa fedha kwa ajili ya chakula. Tunaomba sana Serikali yetu sikivu chini ya Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli irekebishe suala hili ili watoto waweze kupata mlo shuleni wazazi wasiendelee kutoa michango.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nije katika suala zima la madawati. Naipongeza sana TAMISEMI kwa jinsi inavyoshughulikia suala la madawati. Katika Mkoa wangu wa Arusha kulikuwa na tatizo la madawati 24,304 lakini uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya za Mkoa wa Arusha wamejitahidi mpaka sasa hivi wameshakusanya madawati zaidi ya 18,000. Tatizo la madawati lililobaki kwa sasa hivi kwa shule za msingi ni kama madawati 6,000. Naomba sana tuendelee kusaidiana katika suala hili hata kwa mikoa mingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende katika suala zima la afya. Naomba Serikali ilitoe suala la afya TAMISEMI ili Wizara hii ijitegemee waweze kughulikia matatizo ya wananchi kiundani zaidi. Naomba niendelee kwa kumpongeza Mkuu wangu wa Mkoa wa Arusha kwa jitihada ambazo amekuwa akizionesha katika suala zima la afya. Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza kukarabati Kituo cha Afya cha Ngarenaro, Hospitali yetu kubwa ya Mount Meru wamefungua duka la dawa pale la MSD na limeshaanza kufanya kazi, Hospitali ya Kaloleni wameikarabati na sasa hivi ninavyoongea wanaendelea na Hospitali ya Levorosi, nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba Serikali iuangalie sana Mkoa wangu wa Arusha, Wilaya ya Ngorongoro hasa Hospitali ya Loliondo inayoitwa Waso. Hospitali ile imekuwa ikipokea wagonjwa wengi sana na akinamama wajawazito, lakini kwa sababu eneo lile ni la wafugaji akinamama wamekuwa wakiacha wagonjwa wao kwenda kuwatafutia chakula nyumbani wakati mwingine wanakwenda umbali wa kilometa mpaka tatu. Naiomba Serikali katika bajeti yake ya Hospitali ya Loliondo ya Waso watuwekee chakula ili wagonjwa wawe wanapata chakula pale pale na wawe na matumaini makubwa na Serikali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala la ugonjwa wa endometriosis ambapo tumemwona mwanamitindo maarufu kama Millen Magese amejitokeza hadharani na kukubali kuwa anaumwa endometriosis. Ugonjwa huu ni mbaya sana kwa watoto wetu wa kike na wanawake kwa ujumla kwani unapelekea utasa. Mwanamitindo huyo amejitokeza na anapita mpaka kwenye shule kuelezea kuhusu ugonjwa huu, ni ugonjwa ambao unaweza ukamkuta ndugu yako, dada yako au watoto wetu. Tunaomba sana Serikali ielezee kiundani kuhusiana na ugonjwa huu, athari zake na vilevile watoto wetu wa kike wapate matibabu ya ugonjwa huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Ummy na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla na Makamu wetu wa Rais, mwanamama Mheshimiwa Samia, tumeona wamemuunga mkono mwanamitindo huyu kwa ajili ya kuelimisha jamii nzima ya Watanzania hususani watoto wa kike ili waelewe tatizo hili na jinsi ya kujikinga maana wakijikubali kama mwanamitindo huyo nadhani watakuwa free kueleza tatizo lao na kutibu ugonjwa huu ambao unapelekea utasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ilani yetu ya Uchaguzi tuliahidi bima ya afya kwa kila mwananchi. Tunaomba sana Serikali ilete Muswada huu Bungeni mapema ili tuweze kuupitisha, wananchi wetu waweze kupata huduma ya afya kupitia Serikali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana Serikali iangalie upya suala zima la ugonjwa wa kisukari. Ugonjwa wa kisukari hasa huu wa kurithi, tumeona watoto wadogo wanapata sukari na zimekuwa zikiwatesa sana. Wananchi waelimishwe watajikinga vipi na kisukari, tumeona hata watu wazima, wanaume wanaachwa mpaka na wake zao kwa sababu ya ugonjwa huu wa sukari.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali i-take serious ugonjwa huu, kwa kweli wananchi wanapata shida, akinamama wanapata shida kwa sababu wanaume zao wanakuwa na ugonjwa wa sukari. Tunaomba sana Serikali iangalie kwa makini ugonjwa huu na kuelimisha watu jinsi ya kujikinga na itawasaidia vipi kaka zetu na baba zetu katika suala zima la ugonjwa huu wa kisukari.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba safari hii fedha za miradi ya maendeleo ziende kama ilivyokusudiwa. Tumeona katika sekta ya afya hususani kwenye vituo vya afya na maeneo mengi fedha za maendeleo hazifiki kama zilivyokusudiwa na hivyo kuzorotesha shughuli za maendeleo. Tunaomba sana Serikali ifikishe fedha za maendeleo kama ilivyopangwa kwa sababu tumekuwa tunapata matatizo mengi lakini fedha haziendi kama ambavyo zimekusudiwa. Tunaomba Serikali ihakikishe inafikisha fedha hizi kama ilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kumshukuru Rais wetu John Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kutumbua majipu, tunamuunga mkono aendelee na kazi hiyo ya kutumbua majipu. Tunaona wananchi wanamkubali, tumeanza kuirudisha Arusha kidogo kidogo, mitaa Arusha tumepata, yote hii ni kutokana na kwamba wananchi wanakubali utendaji wa Rais wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwenye macho haambiwi tazama, lakini ndiyo hivyo Serikali ya CCM iko juu na tukiendelea hivyo tutarudisha majimbo yetu yote na watu wa Arusha siku hizi hata nguo za kijani tunavaa na tunashangiliwa tunaambiwa Hapa Kazi Tu. Tunaomba waendelee kuboresha hospitali zetu ili Chama chetu cha Mapinduzi ambacho ni cha ukweli, kinatekeleza ahadi, kinawajali maskini na ambacho mafisadi walikikimbia wenyewe walivyoona moto wake kiendelee kukubaliwa na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.