Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Stephen Hillary Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja asilimia mia moja. Hii Serikali yetu wote, tunatakiwa tuwaunge mkono kwa kila kona katika matukio yote wanayoyafanya kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. Ila nilete kwako masikitiko yangu makubwa kutokana na kitendo alichonionesha Mheshimiwa Naibu Waziri asubuhi. Sikutarajia kama ningepata majibu ya namna ile, lakini nataka nimwambie kwenye siku ya Wizara yake, shilingi yangu hataiona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona nimeleta maneno hapa Bungeni, maana yake ni kwamba kule Wakurugenzi, watumishi wa Halmashauri wameshindwa kuyafanya yale mambo, ndiyo maana nayaleta hapa ili nipate msaada zaidi. Kuna lugha nzuri za kuweza kutufanya sisi ambao tunatumwa na wananchi tuyalete hapa ili mtuelekeze ni namna gani ya kwenda kuongea na wananchi watusikie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu, Wakurugenzi zaidi ya tano; toka nimeingia Bungeni, Wakurugenzi kwangu wanakaa miezi sita sita, hii taarifa ya ardhi wao wataipata wapi? Muda wa kukusanya habari, wao watazipata wapi? Mkurugenzi akikaa miezi sita kaondolewa; akikaa mwaka mmoja, kaondolewa! Kuna watumishi wengine wanakaa miaka, hawaondolewi! Sasa narudi kwenye hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwenye upande wa TAMISEMI. Naomba kwanza wafanye marekebisho ya Sheria ya Manunuzi. Hapa tutakuwa tunadanganyana, hakuna Mbunge anayeingia hapa kuangalia kwenye ile Kamati ya Sheria ya Manunuzi, Wabunge wote tunakaa nje. Wanayojadili mpaka kununua vitu, wananunua watumishi wa Halmashauri, sasa sisi Wabunge tunakwenda pale, tunaambiwa Jimbo lako halifanyi kazi. Kama leo kujenga nyumba inaandaliwa na watumishi wa Halmshauri, unaambiwa shilingi milioni 35, wewe Mbunge hushirikishwi, halafu tunakuja huku tunaambiwa sisi ni mafisadi, ufisadi wetu unaletwa na nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuangaliane kwamba Sheria ya Manunuzi ikirekebishwa na sisi Wabunge tunaingia pale tunatoa hoja zetu. Tukiona mahali hapaendani na jinsi ilivyo, tunapinga. Sasa sisi Wabunge tunakuja kulalamikia Bungeni, kule hakuna mahali tunaingia. Eti wataalam ndio wanakaa, wanamtafuta mkandarasi, wanamweka pale, ananunua vitu; nyumba ya kujenga shilingi milioni 30 anajenga kwa shilingi milioni 90, wewe Mbunge utalalamikia wapi? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nasikitika, tunaletewa hela sana na Serikali, lakini zinaletwa siku za mwisho mwisho. Ikifika siku ya mwezi wa saba tarehe 1, hela zinatakiwa zirudi huko. Kwa nini hizi hela kama mnatuamini mnatuletea, zisibaki Halmashauri ili wananchi wakaendeleza ile miradi ambayo ilikwama kwasababu hela zilikuwa hazipatikani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaashangaa hela zinakuja; Serikali haiwezi kukusanya hela kwa wakati mmoja na ikagawa kwa sehemu moja. Hela ni lazima igawanywe kwa kila sehemu. Wanasema kakondoo kadogo kanaliwa na kila mtu, sasa lazima kila sehemu zipewe lakini inafika mahali kwamba tunaletewa pesa zile, baada ya siku mbili unaambiwa hela zinatakiwa zirudi Hazina; hazijafanya kazi yoyote, hatujapanga mikakati ya aina yoyote, halafu leo tunakuja kulaumiwa kwamba Wabunge hatusimamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili suala Mheshimiwa waziri utakapokuja tueleze; kama hela mnaamini; mimi naamini Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Pombe Magufuli hakuna mahali mtu atapita kuchukua hata thumni kwa jinsi mlivyojipanga safari hii Mawaziri wetu. Mmnejipanga vizuri, mnafanya kazi vizuri na watendaji wenu ni wazuri. Sasa kama Watendaji ni wazuri, mna wasiwasi gani hela zisibaki Halmashauri? Mimi kwangu zilikuja hela za maji, Benki ya Dunia, mabomba yametengenezwa, hayakwisha, lakini hela zinatakiwa zirudi, zinakwenda kufanya kazi gani? Kama zililetwa kwa ajili ya Watanzania na Serikali ya Tanzania itazilipa fedha zile, kwa nini zisibaki pale ili tukijua kwamba zimebaki pale, ziendeleze miradi mingine ya maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niseme kwasababu sasa hivi kuna hospitali, tuna zahanati nyingi ambazo tuliziahidi kwamba zitaboreshwa, mpaka sasa hivi hatujaboresha. Tulikuwa tunaomba vilevile maabara, wananchi wamechangishwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yangu tukufu tuongeze mtaji ili zile maabara ambazo wananchi walijitolea kwa nguvu ili mwongeze hata ka-percent kidogo wananchi waone Serikali yao inavyofanya kazi, kwasababu Serikali hii ni sikivu na kama Serikali ni sikivu, lazima tuwe kwa kila kona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Kuna suala la Mombo. Mombo toka mwaka juzi ilikuwa iwe Halmashauri, lakini kila siku naomba katika Ufalme wako Mheshimiwa Waziri na hilo naomba uliangalie sana. Niko chini ya miguu yako, Mombo. Katika vitu ambavyo vinaumiza kichwa wananchi wa Korogwe Vijijini, Mombo, iweke iwe Halmashauri ya Mji. Watu tumezunguka kila kitu tumefanya tumefanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye utawala bora. Ukimkuta mtu anawasema watu wa TAKUKURU akili yake kidogo imepungua, wanafanya kazi sana. Ukimkuta mtu anasema watu wa Kamati ya Maadili, wanafanya kazi sana. Naomba tuboreshe ofisi zao, naomba tuwape nguvu, naomba badala ya kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashitaka, wapewe ruhusa, wao wenyewe wapeleke watu mahakamani. Tunaogopa nini? Kama mtu huna tatizo ambalo umelifanya, wao mpaka kesi waichukue, waijadili, waichunguze wakishaichunguza halafu inapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka. Sasa kama hamwaamini, mliwapa kazi za nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maadili wanafanya kazi. Juzi nilikwenda Kibaha, nimeangalia Ofisi ya Maadili ya Kibaha, utafikiria ni nyumba ya Mganga wa Kienyeji, tena ni nyumba ya kukodi na wakati watu wanafanya kazi kuhusu maadili yenu kuwa mazuri! Kwa nini tusiwaboreshee ofisi zao na kila Mkoa kukawa na ofisi? Wanapokuwa wanafanya kazi na ukiwawekea ofisi nzuri, nao wanakuwa nguvu ya kufanya kazi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa usalama. Leo hii Usalama wa Taifa tunatakiwa tuwaongeze posho, kwa sababu wanapofanya kazi ni kwa ajili ya maslahi ya Watanzania. Ninyi hamjakaa Kenya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimekaa Kenya miaka 15. Kuna wakati Mtanzania analala saa 6.00, kwa nini? Kwa sababu usalama wao ni mdogo. Leo hapa Tanzania watu wa usalama wanafanya kazi vizuri, tunawaangalia, hatuwapi matumaini, tena tukiwaona tunawadharau. Tusifanye kazi kwa mazoea. Tufanye kazi kama Mheshimiwa Pombe Magufuli anavyofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona niyaseme haya kwasababu hii ndiyo demokrasia yetu. Mheshimiwa Lukuvi ni rafiki yangu, siondoi shilingi hata siku moja, wala siwezi kuipinga Serikali yangu. Kwa hiyo, kukwambia kwamba nitakuja kuondoa shilingi, siondoi tena naunga mkono moja kwa moja.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana mtuunge mkono sisi Wabunge. Tunakaa katika mazingira magumu sana huko vijijini. Mnapokuwa katika Bunge hili, mjue kwamba ninyi wote ni Wabunge kama sisi. Angalieni kauli za kutujibu. Itafika mahali na sisi tutaonekana kama watu ambao tumetoka nje ya Bunge hili; na hatupendezewi, hatufurahishwi tuonekane kama Wabunge tumekuja hapa kujipendekeza au kupendeza baadhi ya watu, tuonekane tunaiponda Serikali yetu. Serikali yetu ni sikivu, inafanya kazi vizuri, Mawaziri safari hii ni Wazuri, naomba muendelee kutujali na kututhamini katika majibu yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwape nafasi wengine; nakushukuru kwanza wewe binafsi kwa kukuomba ombi langu kwamba naumwa sana mguu niasidie na umenikubalia, Mungu akubariki sana.