Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Tangu awali hapa ngoja niseme kabisa kwamba Bajeti iliyopo mbele yetu inastahili na ninaiunga mkono kabisa, ila sasa nachangia kwa mtazamo wa mwananchi wa Muleba Kusini na hasa Halmashauri ya Muleba kwa ujumla wake.
Imeshasemwa hapa kwamba kwa sisi ambao tunatoka kwenye Halmashauri ambazo ni kubwa na Majimbo makubwa, tuko katika hali ngumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri Simbachawene atakaposimama hapa kufafanua, ajaribu kuoanisha mgao wa fedha zilizogawiwa na wingi wa watu na ukubwa wa eneo. Kwa maneno mengine, tunataka weighted average; kwa sababu haitoshi kusema fedha kadhaa zinapelekwa mahali, ni lazima uangalie per capita; wale wananchi walio mle wanapata kiasi gani? Uone kama zinatosha kusukuma maendeleo au hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipofanya hivyo, tunajikuta katika hii pressure inayozidi kuongezeka ya kugawa Mikoa, Majimbo na Wilaya lakini mwisho wa siku tunakuwa na viongozi ambao sasa hawana OC ya kufanyia kazi, hili ni tatizo kubwa sana. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri ajaribu kutusaidia kama siyo sasa huko anapokwenda kuliangalia jambo hili, ni la muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Muleba ndiyo kubwa katika Mkoa wa Kagera, ina Kilomita za mraba 10,500, theluthi mbili zikiwa ni maji, mimi hapa nina Kata 25; nina wananchi 600,000; nina wapigakura 264,000 na kadhalika na kadhalika. Sasa katika hali hiyo bajeti ambayo iko mbele yetu, kitu cha kwanza nakubaliana na Serikali. Serikali haiwezi kugawa fedha ambazo hazipo. Sisi kama Wabunge tunapenda sana kusema kwamba tuongeze bajeti, lakini nimeangalia katika majedwali ambayo Waziri ameleta hapa na yamekaa vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia jedwali namba 11, linaonyesha vitu muhimu. Kitu kinachokosa ni uwiano na wananchi katika lile eneo husika, hilo halipo. Isipokuwa utaona kwamba kwa ruzuku ambazo zimekwenda, kwa mfano kwenye Road Fund. Road Fund nadhani kila Mbunge hapa anaitegemea sana, lakini ni asilimia 5.25 ya fedha ambazo zililipwa zilizopelekwa kule.
Sasa unaona kwamba unapokuwa katika hali ya kupanga bajeti kubwa, watu wakawa na matumaini, Halmashauri zikafikia kwamba fedha zitatoka katika bajeti kuu, fedha hizo zisipokwenda tunarudi nyuma. Kwa hiyo, napendekeza kwa Mheshimiwa Waziri alifikirie hili atakapokuwa anajumuisha (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhuru zaidi na hapa ninapoangalia, Waziri wetu wa Utawala Bora na decentralization, dhana nzima ya kugatua madaraka ni kupeleka wajibu kwa hawa watu. Wajibu huwezi kupeleka wajibu bila kuwapa watu uhuru na kuwaamini. Nimemshukuru sana Waziri Mkuu aliposimama hapa na kusema sasa bajeti chini ya shilingi bilioni moja itaweza kuamuliwa yaani mikataba itaweza kuamuliwa kwenye Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia na Mawaziri wetu mwangalie suala la ajira kwa mfano, process ya kuwaajiri watu kwenye Halmashauri, eti watu wanatoka Dar es Salaam kuwaajiri Watendaji wa Vijiji Muleba. Jamani, mambo mengine Mheshimiwa Mwalimu Nyerere alisema kuna maendeleo ambayo hayahitaji pesa. Mtu atoke Dar es Salaam kusimamia eti kumwajiri Mtendaji wa Kijiji. Sehemu nyingine Kiswahili ni lugha ya Taifa, lakini sehemu nyingine Mtendaji wa Kijiji ni vizuri pia akajua mazingira ya pale ambapo anaajiriwa. Kwa hiyo, unaona mantiki ya kuwa na Serikali za Mitaa ni nini. Kama tutaendelea na control ya namna hii, maana yake hii central control inafuta dhana nzima ya decentrelization. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu limezungumziwa sana, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ameshavuna a low hanging fruit. Kwa kutamka tu elimu bure, watoto walioandikishwa wameongezeka kwa asilimia 32. Nimeona hapa Mheshimiwa Waziri ameleta takwimu ziko very clear. Watoto walioandikishwa Darasa la Kwanza wameongezeka kwa 32%; kutoka bilioni 1.3 mpaka bilioni 1.8; ni maendeleo makubwa. Katika Mkoa wa Kagera wameongezeka kwa 44% na Muleba kwangu wameongezeka kwa 69% kwa tamko tu yaani hii ndiyo Mwalimu Nyerere alisema mendeleo yasiyohitaji pesa. Watoto kuletwa shuleni ni maendeleo, hayo tumeyaona. Sasa mtu anaposimama hapa kusema kwamba elimu bure haijaleta tija, huyo hawezi kuwa anakwenda na takwimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa ufahamu wangu wa mambo nasema kwamba indicators ya mafanikio ndiyo hizo kwamba watoto wameletwa shule. Sasa sisi tuwezeshwe na wahusika Mawaziri, tujitegemee. Kuna dhana ya kujitegemea. Hii notion kwamba Serikali italeta fedha, Serikali haiwezi kuleta fedha ambayo haina, hilo nalo tulijue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi kama Halmashauri nimeona kuna Halmashauri nyingine zimekopa, zimekuwa pro-active zimekazana. Halmashauri nyingine zimesubiri kwa sababu tunakosa mwongozo. Tunaomba Mheshimiwa Waziri utuletee mwongozo kuhusu waraka wa hii dhana ya elimu bure. Elimu bure haitaweza kujenga madarasa yote, haitaweza kujenga maabara zote, lakini wananchi tuko katika hali ngumu au siyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu niko katika hali ngumu. Siwezi kusimama Muleba nikawaambia wananchi wachangie, wakati wanasema kwamba Serikali imesema kila kitu ni bure. Nafikiri ingekuwa ni vizuri tukapata waraka sasa kutoka kwa Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Elimu kufafanua responsibility ya mzazi ni nini na responsibility ya Serikali ni nini. Katika hili niseme waraka ambao ulitolewa na Wizara mwezi Disemba ulisema wazazi wanagharamia chakula, mimi kama mwalimu wa siku nyingi, naomba kama mtu mwenye umri hapa, maana yake na sisi wazee tuna kitu cha kuwaambia hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nikisoma primary enzi za mkoloni, hakuna mtoto alikuwa anaruhusiwa kwenda shuleni bila chakula. Kulikuwa hakuna hotpot, hakuna kitu chochote, lakini mama anachemsha kiazi unakwenda nacho; mama anachemsha muhogo unakwenda nao; mama anakupa kipande cha ndizi, unakwenda nacho. Sasa sisi tumekuwa Taifa, watoto wanashinda na njaa. Eti watoto watasomaje hawajala kitu chochote? It is not serious! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, nafikiri tungepata waraka ukafafanua mambo, sisi tuko tayari kuwajibika; Muleba Kusini tuko tayari kuwajibika lakini sasa ngazi za juu zisituchanganye. Mnatuchanganya kwa kusema kwamba mambo yote yatafanywa bure wakati uwezo wa kufanya bure hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mchango wangu na ninautoa nikiunga mkono hoja kwa asilimia mia moja kabisa kwa sababu najua kwamba ndivyo hali ilivyo. (Makofi)
Mwisho kabisa, watoto wa miaka minne kwenda kwenye chekechea, Mheshimiwa Waziri naomba uliangalie, labda umri ungepanda kidogo, kwa sababu watoto wanakuwa wengi, madarasa hayapo, walimu hawapo, service ratios haziwezi! Sasa unakusanya watoto wadogo 50 au 80 kwa mwalimu mmoja, ataweza kufanya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi nyingine unasema kwamba watoto wawe miaka mitano au sita au saba kwa sababu inapunguza pressure kusudi uweze kujiandaa na kuweka services zinazohitajika.
Baada ya kusema yote hayo, naunga mkono hoja moja kwa moja, Muleba Kusini usitusahau Mheshimiwa Waziri, karibu ututembelee. Na wewe Mheshimiwa Mama Angellah Kairuki, njoo ututembelee, uje uangalie sasa Watendaji wa Vijiji walioajiriwa kutoka Dar es Salaam, kwa kweli ni kizungumkuti! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.