Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hotuba ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni; naunga mkono pia hotuba mbili za Utumishi na mambo ya TAMISEMI kwa Wasemaji wa Upinzani Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kadhaa hapa ya kuzungumza. Kuna hoja hapa ya ndugu yangu, Mheshimiwa Angellah Kairuki aliyowasilisha, ya Utawala Bora; ndiyo nataka nianze nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora ambao unazungumziwa ni muhimu tungeanzia hata humu ndani kwenye Bunge hili kama kweli kuna utawala bora. Bunge limengolewa meno, limekuwa butu kweli kweli!
Bunge limekuwa kibogoyo! Bunge limekuwa na watu waoga kweli kweli! Wabunge hawana uhuru wa kuzungumza na kutoa maoni yao! Hili Bunge ni aina ya Mabunge ambayo hayajawahi kutokea, labda hii ndio kazi tu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya. Nimesikiliza Wabunge wa CCM wengi waliopangwa kwenye Kamati ile. Inaonekana walipangwa na Mheshimiwa Spika kwa maelekezo na naambiwa kwamba kikao kilikaa, wale wengi ambao walikuwa wanamuunga mkono Mheshimiwa Lowassa walitupwa kwenye Kamati yangu na mimi naipenda sana, kama sehemu ya kuwaadhibisha. Maana yake hiyo kazi Spika aliifanya kwa maelekezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Spika mwenyewe ningependa awe hapa. Jana alimwita Mheshimiwa Mbunge mwenzetu hapa bwege. Akamwambia aache ubwege! Yaani bwege asionyeshe ubwege!
Kwenye kikao cha Bunge jana! Ilizungumzwa, wala siongei uongo. Hapa nitaongea mambo ya ukweli tupu. Alisema Mheshimiwa Bwege, naomba uache ubwege. Sasa wataalam wa Kiswalihi wanaweza wakasaidia.
KUHUSU UTARATIBU......
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuelewa na nitazingatia ushauri wako. Kwa hiyo, maneno yote yale yameondolewa eeh! Mnapenda sana hiyo eeh!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muda wangu ulindwe.
Hoja yangu tu ni kwamba, Bunge hili Waheshimiwa Wabunge hawana uhuru, wanapigiwa pigiwa simu, haijalishi nani amepiga lakini wanapigiwa na watu wa ngazi ya juu kwa kuwatishatisha ili wasiwe na uhuru wa kutoa maoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taarifa mbalimbali za ukaguzi inaonyesha kwamba hata Ikulu yenyewe kunakuwa na rushwa. Taarifa mbalimbali zipo, wala hili huwezi kupinga. Sasa kama Mheshimiwa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba Ikulu ni mahali patakatifu, kama kuna chembe chembe za rushwa kwa nyakati mbalimbali, sasa huo utawala bora utawaelezaje watu wa kawaida kama kule jikoni kwenyewe chakula kinaibiwa, watu wananyofoa minofu jikoni...
Tutafanyaje katika mazingira hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ulizikataa, nakushukuru sana.
MHE. MWITA M.WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kaka yangu, sisi watu wa kule kwetu huwa hatuogopi kusema ukweli. Namshauri Mwanasheri Mkuu wa Serikali, asiwe anatoa tafsiri za sheria za ki-CCM atoe tafsiri za kisheria za sheria in profession. Namshauri sana maana yake nimevumilia imebidi niseme tu hadharani kwamba ni muhimu Mwanasheria aseme sheria za kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, hapa kuna mambo yanaelezwa, sisi tulichosema ni kushauri kwamba katika mambo kadhaa yaliyofanyika, Mheshimiwa Rais hajafuata utaratibu kwa maana ya kutumia mamlaka yake vibaya, kwa maana ya kufanya reallocation ya fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ushauri na sheria hizi zipo, utakuja na tafsiri nyingi sana kwa maana ya kuficha mambo, lakini ukweli unabaki pale pale. Naomba nitaje kwa mfano, Katiba ya Nchi Ibara 18(a), (b) na (c) kinaeleza uhuru wa kupata habari; tena unasema hata nje ya mipaka ya nchi. Hili jambo huhitaji kupata mkalimani, inaeleweka tu, kwamba Watanzania wamenyimwa fursa ya kupata taarifa ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapanga wananchi hawa walipe kodi, tunawashawishi namna gani? Hawa jamaa wa CCM wameenda wamekaa kwenye mkutano wao, wanaaminisha watu kwamba ooh, watu wa Upinzani tutaonekana. Hii siyo hoja! Ni hoja ya kitoto kabisa! Hoja hapa ni kwamba ni kwa nini kama kweli mnafanya kazi vizuri, wananchi wasiwe na uwezo wa kujadili na kuona tunachokiona? Nawa…
MWENYEKITI: Ahsante, muda wako… Aalah! (Kicheko)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kengele ya kwanza. Nakushukuru! Naona sasa unaanza kunitania! Aisee! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Hoja nyingine, ukisoma Ibara ya Katiba ya 135, mambo yale ya Hazina inaeleza, Katiba ya Ibara ya 146(1) inaeleza, vitu vingi vimezungumzwa.
Niende kwenye hoja ya TAMISEMI; kuna jambo la bodaboda hapa; hawa vijana na hasa Dar es Salaam. Sasa hivi kuna uhalifu mkubwa, vijana wetu walishawishika, wengine wamechukua mikopo, wanajikopeshea fedha zao kwa watu binafsi na wengine VICOBAvile wanapata fedha ya kujiendeshea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na mitindo wa kusumbuliwa sana Dar es Salaam pale! Kuna watu wameitwa Askari wa Jiji, nadhani wale tutawashughulikia kwa sababu Jiji la Dar es Salaam tunaongoza sisi, nami ndio Mwenyekiti wa Mkoa, naelekeza sasa, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, hili jambo alifanyie haraka mapema sana. Hawa vijana wanapata shida kule Dar es Salaam, wanakamatwa hovyo, wanasumbuliwa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameenda kuteua hawa Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Ma-RAS waliostaafu Majenerali. Sasa hawa vijana ambao wanahitaji hapa ajira, si angewapa kazi hao vijana! Humu ndani kuna Wabunge wana vyeo viwili viwili; yaani mtu ni Mbunge halafu ni DC, halafu ajira ni shida! Hivi huyu mwenye vyeo viwili ana nini? Ana pembe kichwani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wanyang’anywe vyeo, tugawane kilichopo. Mtu amefanya kazi, amestaafu, anapewa kazi nyingine tena, halafu mnataka ufanisi! Watu wameshachoka, wanasinzia ofisini mnawapa kazi nyingine. Hii kitu kwa kweli vijana hawa msiwanyanyase na utaratibu uwekwe sawa sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti ya Manispaa ya Ilala tumekadiria kukusanya shilingi bilioni 85 ikiwepo kodi ya majengo na mabango lakini shilingi bilioni 28; Shilingi bilioni 18 majengo na Shilingi bilioni kumi ni mabango. Maana yake huu mpango, kwenye hotuba ya Waziri wa TAMISEMI inaeleza kwamba Halmashauri itasimamia, kwenye Mpango wa Waziri wa Fedha inaonyesha vinginevyo. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind-up hapa aeleze kipi ni kipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa ya Ilala ilifanyiwa ukaguzi mwaka 2011/2012 - 2012/2013 lakini na hii ya leo nimeisoma, Manispaa ile inaonekana ni miongoni mwa hati isiyoridhisha. Sasa haya mambo, walikaguliwa watu 2011, Mkaguzi Mkuu alikagua, akaleta taarifa; lakini ninavyozungumza hapa, tuna vitengo na idara zaidi ya 18 lakini viongozi wale watano tu ndio wamethibitishwa, wengine wote wanakaimu. Nimejaribu kuhesabu hapa, karibu 13! Sasa katika mazingira hayo, tunafanyaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.