Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia. Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Sumbawanga Mjini kwa kunipa nafasi tena kwa mara ya pili kuwa Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini.
Jambo la pili naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya, ninaamini Watanzania wote tuko nyuma yake kumwombea Mungu ili aendelee na kazi hii nzuri aliyokuwa ameianza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la tatu, nawapongeza Mawaziri wote walioteuliwa. Naomba niwakumbushe tu wengi wenu tulikuwa huku nyuma, tunakaa pamoja, lakini mmetuacha, mmetangulia, naomba mtumtendee haki kwa sababu na sisi ipo siku tutakuja kukaa huko mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie masuala matatu, lakini katika masuala hayo yapo ambayo inawezekana kwa njia moja au nyingine isiwaguse Mawaziri waliopo mbele yetu hapo; Mheshimiwa Simbachawene, Mheshimiwa Jafo na Mheshimiwa Angellah Kairuki, ni kutokana na majukumu niliyonayo. Inawezekana wakati huo wa kuchangia muda mwingine nisiwepo, Mawaziri waliokuwepo waya-note, wayachukue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la kwanza ni kuhusiana na uwanja wa ndege. Sumbawanga tumejaliwa kuwa na mambo mengi, lakini yapo mengi ambayo tumeyatekeleza kwa mwaka 2010/2015, lakini yapo machache ambayo tulikuwa hatujayakamilisha, ni pamoja na uwanja wa ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeiona bajeti hii ambayo ninaamini tumepata fedha za kujenga uwanja wa ndege, lakini kuna shida moja naomba ichukuliwe kwa sababu wakati tunafanya tathmini ya yale majengo ambayo wananchi wanatakiwa walipwe fidia, tathmini ile imechukua miaka saba sasa. Kwa hiyo, ninaamini kabisa kwenye bajeti hii tumetenga fedha za uwanja ndege, lakini tumetenga fedha kwa tathmini ya miaka sita iliyopoita. Kwa hiyo, naomba sasa tathmini ile ifanywe upya ili wananchi wapate haki yao na waweze kujenga kutokana na gharama zilizopo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili ambalo ni kero kwa wananchi; na kwa hili naomba nichukue nafasi kumpongeza Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa Lukuvi, kwa kazi kubwa aliyoifanya mpaka hapa tulipo leo. Isipokuwa shamba lile la Malonje limekuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi na Mheshimiwa Waziri alisema atakuwa ni mtu wa mwisho kuongelea shamba lile. Sasa nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, alifanyie kazi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nimpe nguvu tu Mheshimiwa Waziri, kwa sababu shamba hili linahusiana na watu wa TAMISEMI na Mheshimiwa Waziri unanisikia, basi naomba tulifanyie kazi ili wananchi waweze kupata shamba lile lililokuwa ni kero kubwa na sisi tunazingatia kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo, lakini naamini kabisa kilimo ni ajira. Tukiwapa ardhi wale wananchi, wanaweza wakalima na wakapata mafanikio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Rais, mgombea wetu alipokuja Sumbawanga kwenye kampeni aliniahidi, akasema endapo mtamchagua Aeshi, chochote atakachoniomba nitampa. Mimi naomba nimwambie Mheshimiwa Rais, sihitaji Uwaziri, wala Unaibu Waziri, naomba anisaidie shamba lile liweze kurudi kwa wananchi. Ninaamini uwezo huo anao na anaweza akatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la tatu, ni maji. Mheshimiwa Waziri tuna mradi mkubwa sana wa maji wa shilingi bilioni 32, mradi ambao tumeweza kujenga miundombinu yote, lakini shida imekuja kila tukichimba kisima hakina maji. Sasa nataka niseme maji ya kutoka Lake Tanganyika tungeweza kuyapata kwa sababu kutoka Lake Tanganyika – Kasanga kuja Sumbawanga ni kilometa 90. Ninaamini kabisa endapo tukipata fedha, tukajenga mradi ule wa maji wa kutoka Lake Tanganyika - Kasanga ukapita Matai na Sumbawanga vijiji vyote vitaweza kufanikiwa kupata maji. Kwa hiyo, nataka niseme tu, jambo hili tuliangalie kwa umakini, endapo tutapata fedha, basi tujaribu kutafuta njia moja ama nyingine ya kuweza kutoa maji Lake Tanganyika ambayo yataweza kuwanufaisha watu wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ni kuhusiana na umeme. Tumepeleka vijiji vingi sana lakini bado vijiji vichache ili tuweze kufanikisha Jimbo lote la Sumbawanga mjini kuwa na umeme. Kwa hiyo, Waziri anayehusika na dhamana ya umeme, naomba naye alichukue kwa sababu kwa upande wa CCM kwa sababu tupo wengi, inakuwa ni vigumu sana kupata nafasi ya kuchangia mara ya pili.
Mwisho kabisa ni kuhusiana na meli MV. Liemba. Tumeona kwenye bajeti kwamba MV. Liemba itafanyiwa marekebisho, nasikitika sana! Meli ile mara ya mwisho nilipanda nikaona kuna jenereta imewekwa juu kabisa kule, ipo nje na ni hatari kubwa. Vilevile meli ile imekuwa ni ya muda mrefu sana, ina umri zaidi ya miaka 120, wananchi bado wanaendelea kuitumia meli ile, ni hatari kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama tumeweza kununua meli Ziwa Victoria, basi ni vizuri sasa na Lake Tanganyika tukakumbukwa angalau kwa meli moja ya kuanzia. Baada ya kusema hayo machache, naomba haya machache niliyoongea, naamini ni ya muhimu ndani ya Jimbo langu la Sumbawanga Mjini, mengi nimeyafanya kama Mbunge, mengi nimeyakamilisha, haya machache ukiyakamilisha mwaka 2020 napita bila kupingwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni sana, naunga mkono hoja.