Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Mussa Azzan Zungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ilala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na pia namshukuru Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono bajeti hii ya Wizara ya TAMISEMI kwa asilimia mia moja. Nina hakika kwa Mawaziri hawa na usimamizi mzuri utakaofanywa wataweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua nafasi hii kupongeza Serikali kwa kuweza kuingia mkataba na Serikali ya China kujenga reli ya kati nchini mwetu. Hili jambo sio la mchezo. Kwanza tumeweka pesa zetu, wadau wa nje wakashawishika na wao kuleta pesa zao kwa asilimia zaidi ya mia moja. Napongeza sana jitihada zilizofanywa na Mheshimiwa Magufuli pamoja na Serikali yote na Waziri Mkuu kwa namna reli hii itakavyojengwa. Reli hii ita-capture biashara katika nchi nyingi sana ambazo zinatuzunguka. Uwezo wa reli hii kubeba mizigo ni zaidi ya tani milioni kumi kwa mwaka. Reli hii katika kipindi cha miaka saba mpaka kumi gharama zote za deni zitalipwa. Kwa hiyo, naomba tuendeleze amani, amani za majirani zetu ndiyo amani yetu sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto za elimu bure ambapo ni kazi yetu kuzifanyia kazi ili tuzimalize. Suala la madawati si suala la Serikali peke yake, ni suala letu sisi wote, wa vyama vyote vilivyoko nchini mwetu. Tushirikiane na Serikali yetu tutafute njia mbadala. Watoto hawa ni wetu, mtoto wa mwenzio ni wako. Kwa hiyo, suala la elimu bure na hii changamoto ya madawati tuisaidie Serikali, tuje na hoja positive za kuisaidia Serikali iweze kutatua tatizo hili na changamoto hii iishe ili watoto hawa waweze kusoma na nchi yetu iweze kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina mchango mkubwa kama kawaida yangu, nazungumzia Benki ya Wananchi ya Dar es Salaam (Dar es Salaam Community Bank). Benki hii imeanzishwa kwa mtaji wa Halmashauri nne, Halmashauri za Manispaa ya Ilala, Kinondoni, Temeke na Jiji la Dar es Salaam. Tume-sacrifice miradi yetu kuweka mtaji kuanzisha benki hii. Hawa watendaji wa sasa hivi walikuwa wanakuja pale Jiji mikono nyuma wanaomba kazi. Baada ya Halmashauri hizi nne kujinyima kwenye vyanzo vyake, tumewanyima wananchi wetu mikopo kwa kutegemea benki hii sasa iwe chombo cha kusaidia wakazi wetu kuwakopesha ili na wao wanyanyue maisha yao. Asilimia kubwa ya mtaji wa benki hii imefanywa na wananchi wa Dar es Salaam wenyewe kupitia kwenye Halmashauri zao. Ni wanyonge ndiyo waliochangia benki hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini habari ya benki hii baada ya wataalam hawa kuingia, baada ya ya benki kusimama kwa hela za wananchi wa Dar es Salaam wenyewe ikiwa kama ndiyo mchango wa kwanza, wameanza kutuingiza katika masuala ya financial regulations, kuna masuala ya mitaji na kipindi kile walisaidiwa wakaanza kutu-dilute. Mtaji wetu sasa hivi wa Halmashauri hizi nne umeshuka mpaka sasa ni asilimia tisa. Wametutoa kwenye umiliki wa benki hii mpaka kutufanya sasa ni watu wa chini kabisa wa benki hii. Benki hii ilifanya mambo haya kwa kutumia vigezo vya mitaji ambayo Halmashauri na uwezo mdogo wa watu kuelewa masuala ya financial services na banking zilivyo hawakuelewa na kila mwezi kila kwenye mikutano mikuu tukanza kushushwa mpaka sasa hivi hatuna mali, hatuna chochote kwenye benki hii. (Makofi)
Naiomba Serikali Mheshimiwa Waziri na wewe ni mtaalamu wa majipu, tunataka benki hii ifanyiwe uchunguzi, tunataka benki hii iende kwa CAG ili sasa hatma na heshima ya wananchi na Halmashauri hizi nne za Dar es Salaam zirudi kumiliki benki hii kama tulivyoianzisha. Haiwezekani wenye mtaji, watu maskini wanyang’anywe benki hii, ni dhambi kubwa sana ambayo imefanywa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri ulichukue hili, kwa vile benki hii imechangiwa na Halmashauri zako, naomba sasa lifanyie kazi ili tuweze kuimiliki benki hii na kuichukua tena iwe mali ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya machache, naunga mkono hoja. Kama kawaida yangu mimi huwa nasema kidogo lakini nasema makubwa. Nakushukuru na nina-save muda ili wengine nao waweze kuchangia.