Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kidogo katika hoja iliyo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze na Mfuko wa Barabara. Halmashauri zetu zinapokea fedha kidogo kwa ajili ya matengenezo ya barabara, kwa sababu fedha hizo ni kidogo, hawawezi kutengeneza barabara ambazo zina viwango kama zile zinazotengenezwa na TANROAD. Uwiano wa utoaji wa pesa za Mfuko wa Barabara kwa kila shilingi laki moja inayotoka kwa ajili ya Mfuko wa Barabara, Halmashauri inapewa sh. 30,000 which is 30 percent, kwa hiyo unaweza kuona Halmashauri wakipewa fedha, ni zile fedha ambazo zinaweza kufanya grading peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawawezi kutengeneza mitaro, hawawezi kuweka karavati, kwa hiyo mwaka hadi mwaka tutabaki kulaumu hizo Halmashauri. Serikali imekuwa ngumu kubadili sheria hii ili kusudi Halmashauri ziweze kupata fedha angalau hata asilimia 40 waweze kutengeneza barabara ambazo zinawiana, kwa kuangalia jinsi walivyotueleza ukisoma katika hotuba ya Waziri, anasema kuna zaidi ya barabara mtandao wa kilomita laki moja na kitu na nafikiri inawezekana ni zaidi ya hizo, maana yake sina uhakika wamefanya lini research.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya kuongeza maeneo mapya ya utawala, hizi barabara za Halmashauri zina mitandao mikubwa ambayo kwa kweli Serikali inapaswa ifikirie namna ya kuwapa Halmashauri fedha za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napitia hili jedwali ambalo tumepewa na Waziri, nitoe mfano tu wa Mkoa wa Kagera peke yake. Mwaka 2014/2015, Mkoa wa Kagera ulikuwa umetengewa bilioni 9.1, lakini ulipewa bilioni 3.9, mwaka 2015/2016, Mkoa wetu tulitengewa bilioni 6.9 lakini tulipewa milioni 366, kwa hiyo ukichukua pesa zote hizo tulizopewa katika miaka hii miwili, tumepewa 4.2 bilioni. Unaweza ukaona ni jinsi gani, pesa zinavyokwenda katika Halmashauri na katika Mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ifikirie namna ya kupeleka pesa ili tuweze kusaidia hizi Halmashauri, ziweze kutengeneza barabara kwa kuzingatia kwamba watu wote wako kule katika Halmashauri na huduma zinahitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili naomba niongelee, ni kuhusu elimu. Ukurasa wa 24 wa kitabu cha Waziri, ameongelea kuhusu mambo ya elimu, mipango ni mizuri, lakini naomba nijielekeze katika hizi shule maalum ambazo zinafundisha watoto wenye matatizo, walemavu wa ngozi, walemavu wa viungo, pamoja na wale wasioona. Naomba nitoe mfano wa shule ambayo iko katika Mkoa wa Kagera inaitwa Ngeza Mseto.
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 8 Machi ilikuwa ni Siku ya Wanawake Duniani, Chama chetu cha CHADEMA kilisherehekea sherehe hiyo kwa kwenda kutoa huduma katika sehemu mbalimbali ikiwemo shule hiyo. Tulichokikuta pale kuna watoto walemavu wa ngozi, kuna wale walemavu wa viungo, lakini pia kuna watoto wasioona. Tulichokikuta pale, wale wamama walioenda pale, walikuta vitanda vimejaa vinyesi, watoto hawaoni wale, wanalalia vinyesi, yaani mizinga ya vinyesi imejaa kwenye vitanda vyao, Walimu wapo, Matroni yupo.
Mheshimiwa Naibu Spika, worse still, nakumbuka mwaka 2000 nilikuwa Diwani, wakati ule Mheshimiwa Mizengo Pinda alikuwa Waziri mwenye dhamana na TAMISEMI, alifika kwenye shule hii na kwa kweli aliomba Hazina, Hazina wakawa wanatoa fedha extra money milioni 60 kila mwaka, yaani milioni 15 kila baada ya kota moja. Je, naomba niulize TAMISEMI na nimuulize Waziri wa Elimu, pesa hizo bado zinakwenda na kama zinakwenda zinafanya nini?(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uchungu mkubwa kabisa wale watoto wanavaa mpaka lisani zinatazama huko hawana mtu wa kuwaambia au kuwavisha, mabweni yao yote yamezungukwa na vinyesi, uchafu, wale watoto wanaishi kama wanyama. Ninyi mmetamka katika kitabu hiki kwamba mtahakikisha kwamba watoto wenye mahitaji maalum watapewa elimu na wataangaliwa afya zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli shule ya Ngeza Mseto iko Manispaa ya Bukoba, tunaomba Waziri wa TAMISEMI na Naibu Waziri nendeni mkaiangalie hiyo shule, mhakikishe kwamba inapewa pesa. Siyo hiyo tu, hata vile vituo vingine ambavyo vina watoto ambao wana matatizo ya namna hiyo Serikali iweke mkono wake. Halmashauri peke yake ya Manispaa ya Bukoba haiwezi kabisa ku-manage shule hii, kwa sababu shule inabeba watoto wa Mkoa mzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu taarifa ya Mdhibiti, mimi niko kwenye Kamati ya LAAC na hapa wameongelea kuhusu asilimia 20 ya fedha za Serikali ambazo zinazotoka kama ruzuku ambazo zinapaswa kwenda katika Vijiji, zingeweza kulipa mishahara ya Wenyeviti wa Vijiji au posho zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tulichogundua Kamati yetu imepitia Halmashauri 30, Halmashauri zote 30 zimeshindwa kupeleka hiyo asilimia 10, hizo Halmashauri zina jeuri! Zile pesa siyo mapato ya ndani ya Halmashauri, zile fedha zinatokana na ruzuku ya Serikali ambayo ni fidia ya vile vyanzo vya mapato, lakini Halmashauri hazipeleki hizo fedha na zikipeleka zinapeleka kwa asilimia kidogo. Mheshimiwa Simbachawene anajua na nafikiri Mheshimiwa Jafo anaelewa, waliona maoni yetu ni kwamba hizi fedha haziendi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ihakikishe na kusimamia pesa hizi ziwe zinakwenda na ninachotaka kuwaambia hata Vijiji vyenyewe havijui, havina taarifa kuhusu fedha hizo, inawezekana hata zikipelekwa zinaweza kulambwa na Wenyeviti wa Vijiji pale au na Watendaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kwa kusema juu ya utawala bora. Nisimalize bila kuongelea kuhusu haya mambo mnayosema hapa kuhusu TBC na nashangaa sana, wenzangu CCM msije mkafikiri kurudi ndani ya Bunge hili, mjitazame ninyi huko nyote kuna watu hawakurudi almost 60 percent kwani matangazo hayakuwepo? Kurudi au kutorudi haina maana kwamba wasiangalie matangazo yao (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii inaendeshwa kwa demokrasia ya uwakilishi, ndiyo maana kuna vyombo kama Bunge, Bunge siyo mali ya Serikali, Bunge ni mali ya watu, ni chombo cha watu na ukitazama dunia nzima huwa kunakuwa na mvutano mkubwa kati ya Serikali na Bunge. Serikali hailipendi Bunge, kwa sababu Wabunge mnaisema Serikali, mnaisahihisha, mnafichua, kwa hiyo itafanya kila mbinu kuhakikisha kwamba hili Bunge linadhoofika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi hii, viongozi wote nawaambia, Naibu Spika upo hapo na Spika, hebu igeni hayo Mabunge ya nyuma yalikuwa yanafanya kazi gani, igeni hata nyuma, mnakumbuka Wabunge mliokuwepo, ilikuwa ni kazi kubwa sana kuanzisha Kamati ya Bajeti ndani ya Bunge hili, tunamshukuru Madam Spika pamoja na kwamba tulikuwa tunamkoa makwenzi humu, lakini yule Mama alisimama imara kuhakikisha Kamati ya Bajeti inaanzishwa. Serikali ilikuwa haitaki Kamati ya Bajeti lakini Bunge lilisimama imara,na Spika alisimama imara na Naibu wake. Kwa hiyo na ninyi msikubali Serikali kutuyumbisha, tutashindwa kusimamia watu.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, mtashindwa kuwa na legacy kwa sababu mkimaliza miaka yenu mitano au kumi watu watawakumbuka kwa sababu ipi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana haya mambo ya watu kusikia taarifa ni namna ya kuwaelimisha Watanzania. Katika kitabu hiki, wametuambia kwamba kuna watoto zaidi ya laki mbili na sitini na kitu, hawakuweza kufanya mtihani wa darasa la saba, tunawa-damp huko ndani na inawezekana hawawezi kujiendeleza tena. Watu wanapaswa kupata elimu kupitia majarida, ndivyo wanavyoweza kujua namna Serikali yao inavyoendeshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mnawaambia watoe kodi, watajuaje maana ya kodi, watajuaje zinasimamiwaje hizo kodi, mnawarudisha Watanzania katika ujima. Hatuwezi nchi hii kwenda hivyo, mngefanya miaka ya 60, sasa hivi Watanzania ni waelewa, wanataka kusikiliza Bunge lao, wanataka kujifunza na tuwasaidie kujifunza, tusiwadumaze Watanzania kwa kuwarudisha katika kuvaa ngozi, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yangu ni hayo, lakini nakuomba tena ninyi ni wasomi…