Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia asubuhi ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwashukuru wananchi wa Jimbo la Kilolo ambao kwa kweli wamenirudisha baada ya miaka 10 kukaa bench, nawashukuru sana. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Mawaziri, kwa mwanzo mzuri wa kazi nzuri ambazo tumeshuhudia Mawaziri wetu wakifanya na kufuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia kuhusu TASAF, kwanza naishukuru Serikali kwa mradi mzima huu wa TASAF, tulianza na TASAF I na II ambazo zenyewe zilijikita kwenye ujenzi wa barabara, ujenzi wa shule, ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na kadhalika. Kazi ilifanyika vizuri na ilikuwa inafanyika kwa ushirikishi kati ya wananchi wa maeneo pamoja na mchango wa TASAF.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachosikitisha ni kwamba. baadhi ya maeneo na baadhi ya miradi ambayo ya awamu ya kwanza na ya pili mpaka leo haijamalizwa. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI naomba nikushauri, jaribu kufuatilia ile miradi ya TASAF ambayo haikumalizwa kwenye awamu ya kwanza na ya pili ili iweze kumaliziwa, kwa sababu inavunja moyo sana kuona miradi ile bado ipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, TASAF III, napongeza uongozi mzima wa TASAF kutoka Makao Makuu mpaka Waziri husika. TASAF III ni TASAF ambayo imelenga kuondoa au kupunguza umaskini kwa wananchi, wamefanya kazi kubwa sana. Tumetembea baadhi ya maeneo tumeona jinsi ambavyo wananchi wameanza kubadilika. Kuna matatizo madogo madogo ambayo kama Serikali inabidi iangalie.
Moja ni kwamba wale wanaosimamia TASAF wakiwemo Wenyeviti wa Vijiji, wao wanasimamia kuwapa fedha wale watu maskini lakini wao hawalipwi, hawana posho Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji anasimamiaje mtu kugawa nyama, wakati yeye mwenyewe hali, haiwezekani! Matokeo yake watu ambao wanaingizwa kwenye TASAF III wengine siyo wahusika, wanaingia baadhi ya ndugu wa viongozi, baadhi ya watu ambao wana nguvu zao, baadhi ya watoto wadogo, maana ya TASAF inaharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa Mheshimiwa umesikia, muangalie na mfikirie jinsi gani ambavyo Wenyeviti wa Vijiji, iwepo sheria kabisa ya kutamka kwamba walipwe shilingi fulani, badala ya kusema Halmashauri zichangie asilimia hii itakuwa haiwezekani, kwa sababu kama Serikali wenyewe tumeshindwa kupeleka fedha kwa wakati, Halmashauri ambazo nazo zinategemea mapato ya ndani zitumie katika zile fedha ambazo Serikali ilikuwa ilete, kweli Mwenyekiti atapata hiyo fedha? Kwa hiyo tuiangalie, tuitungie sheria ili Wenyeviti walipwe, inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna jambo lingine naomba Waziri wa TAMISEMI uje utoe ufafanuzi, kwa sababu TASAF wanapeleka fedha kwa watu maskini ili kupunguza umaskini na yule mtu maskini ile fedha anaitumia kwa ajili ya kupika vitumbua, maandazi, anauza nyanya au mama lishe ili apunguze umaskini, lakini cha ajabu Halmashauri zetu zinakwenda kuwalazimisha kulipa ushuru wale watu maskini. Zinamwaga bidhaa zao, wanawekwa ndani kitu ambacho sasa hatujui tunawafanya nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, TASAF inapeleka fedha kupunguza umaskini, Halmashauri inaongeza umaskini kwa kuwatoza kodi na kuwanyanyasa. Naomba Mheshimiwa Waziri utoe tamko kwamba hizi kodi ndogondogo za hawa watu, ambao ni watu wa chini, maskini, ambao kwa kweli anatafuta fedha kwa ajili ya kununua unga ili aweze kupika ugali ale na familia yake, siyo biashara. Halmashauri zijikite kutafuta biashara zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha nyingi za Mfuko wa TASAF tunategemea kutoka nje, Serikali nafikiri imekuwa ikipanga fedha mara nyingi, lakini zile fedha hazijaenda kule. Nafikiri safari hii kwa kuwa tumeamua sasa kubadilika, kufanya kazi na kudhibiti mapato, basi Serikali ihakikishe inatenga fedha za kutosha na kuunga mkono kwenye Mfuko wa TASAF.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie kuhusu ukubwa wa Wilaya ya Kilolo. Wilaya ya Kilolo lilishaletwa ombi awamu iliyopita, ikakubalika kwamba igawanywe, eneo ni kubwa lina takribani ukubwa ambao ni sawa na Mkoa wa Kilimanjaro , lakini mpaka sasa hivi siyo rahisi kwa mwananchi wa Kilolo kuona ile impact ya fedha ambayo inapelekwa kwenye ile Wilaya na kugawanya kwenye Kata zote. Kwa kuwa tayari mmegawa Halmashauri, tumepata Halmashauri ndogo ya Ilula, Serikali iamue ile iwe Halmashauri ndogo, hii iwe Halmashauri kamili ili baadaye muangalie uwezekano wa kugawa Jimbo hilo na kupata Jimbo lingine kwenye Wilaya zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite katika sehemu ya miundombinu. Wilaya ya Kilolo ni Wilaya ambayo ndiyo inayotegemewa kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali, tatizo lake kubwa ni miundombinu. Miundombinu ambayo ipo ni ile ile ya miaka 10 iliyopita. Hivyo, nafikiri kwamba, barabara zetu ambazo tumeziomba zipandishwe hadhi, ikiwepo barabara ya kutoka Idete kwenda Itonya, Muhanga kwenda kutokea Morogoro, ipandishwe hadhi iwe barabara ya mkoa, ili iwe rahisi zaidi kufungua maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Kilolo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni suala la Wazee. Wazee pamoja na kuwa tumetamka kwamba wanatakiwa wapewe huduma bure pamoja na matibabu, lakini bado hatujawawekea utaratibu mzuri. Nashauri kwamba katika zahanati, dispensary na hospitali zetu litengwe eneo maalum kwa ajili ya huduma za Wazee, ili Mzee akifika pale hana sababu ya kukaa foleni kwa sababu sisi sote ni wazee watarajiwa, yale ambayo tunayafanya leo yatakuja kuturudia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nina muda bado kidogo, zingumzie habari ya Wakuu wa Wilaya. Na-declare interest nilikuwa Mkuu wa Wilaya. Kazi ya Mkuu wa Wilaya ni kubwa, kwa sababu kinapotokea kipindupindu anayeulizwa ni Mkuu wa Wilaya, wanapotokea wafanyakazi hewa anayebanwa ni Mkuu wa Wilaya, unapotokea ujenzi wa maabara anayebanwa ni Mkuu wa Wilaya, yanapotakiwa madawati anayeulizwa ni Mkuu wa Wilaya, zinapoongezeka mimba mashuleni anayeulizwa ni Mkuu wa Wilaya, lakini uwezeshwaji wa Mkuu wa Wilaya bado haujakaa sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, OC ambazo wanapelekewa Wakuu wa Wilaya zinapita mikono mingi, nashauri kwamba isipunguzwe ile hela ya maendeleo ambayo imepangwa kwa ajili ya Mkuu wa Wilaya zipelekwe moja kwa moja kwake, kwa sababu haifurahishi kuona kwamba, Wakuu wa Wilaya wanakuwa ombaomba. Mtu ambaye anasimamia maendeleo na haki anatakiwa aombe hata mafuta, haipendezi!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo basi, kama kifungu kipo kiende moja kwa moja bila kuguswa na RAS (Regional Administrative Secretary) au Mkuu wa Mkoa, kiende kwa Wakuu wa Wilaya moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.