Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Mariamu Ditopile Mzuzuri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti ni suala muhimu linalowezesha kupata taarifa sahihi na kuwezesha kuweka mipango mbalimbali ya nchi. Ili kupata maendeleo endelevu katika michezo, ni muhimu kuwa na taarifa sahihi zilizofanyiwa utafiti. Serikali imefanya tafiti nyingi kama vile michezo kwa watu wenye ulemavu, michezo na UKIMWI, haiba na michezo na kadhalika. Bado kuna maeneo mengi ya michezo yanahitaji kufanyiwa tafiti ili kuongeza tija katika sekta ya michezo nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo la kukosekana mfumo endelevu wa kuviendeleza vipaji vinavyoibuliwa na kuwa na miundombinu isiyokidhi mahitaji. Vilevile somo la elimu ya michezo limekuwa halifundishwi kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 2002 hadi 2007 kulifanyika utafiti uliofanywa na Idara ya Elimu ya Michezo na Utamaduni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ulioonyesha kwamba vipindi vya masomo ya michezo katika shule za sekondari za Serikali na binafsi vimekuwa vikitumika kufundisha masomo mengine badala ya elimu ya michezo na michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, tafiti hizi zilibainisha ukosefu wa walimu wenye sifa stahiki za kufundisha elimu ya michezo kuwa ni changamoto kwa shule za Serikali na binafsi nchini. Nashauri Mheshimiwa Waziri aanze na shule za binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokuwepo kwa mfumo na utaratibu mzuri wa ufuatiliaji na tathmini katika michezo kumeendelea kuathiri upatikanaji wa taarifa na mapato halisi yanayotokana na ajira za wanamichezo. Hali hii imeathiri wachezaji na wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta hii ikilinganishwa na nchi kama Nigeria, Ivory Coast, Ghana na Afrika ya Kusini ambazo zimefanikiwa kupitia michezo. Mheshimiwa Waziri, hili linaendana sambamba na sanaa, hususan muziki wa kizazi kipya. Kwa mfano, Diamond ndiye msanii anayelipwa zaidi kuliko msanii yeyote Afrika Mashariki na Kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka Disemba, 2015, Tanzania ilikuwa na wachezaji takribani kumi wanaocheza michezo ya kulipwa nje ya nchi. Tisa ni wa soka na mmoja wa mpira wa kikapu. Hata hivyo, mtazamo wa jamii haujajielekeza kutambua kuwa michezo ina michango katika kukuza uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Mheshimiwa Waziri, tuweze kutafuta wabia zaidi tuweze kujenga sports academy kama ile Jakaya Kikwete Sports Academy, ikiwezekana kila mkoa au angalau kila kanda kwa kuanzia.