Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, jamani Wabunge wakati tunachangia hapa kuna vitu vya kuongea. Jana kuna Mbunge mmoja aliongea hapa alikuwa anafananisha mwenendo wa utendaji wa Serikali yetu, sawa sawa na mauaji ya Kimbari. Jamani wanaofahamu yale mauaji jinsi yalivyotokea siyo ya kuyataja, jambo la kusikitisha zaidi yule Mbunge ni Mchungaji. Ninatamani niwaone hao waumini wake anaowasalisha, na kama kweli ni waumini basi yatakuwa yale makanisa ambayo wanasali bila nguo.(Makofi)
Mheshimiwa Nape, wewe ni rafiki yangu, ni kaka yangu, ni mwanachama mwenzangu wa CCM, lakini kwenye hili, ndugu yangu utanikosa na utanisamehe. (Kicheko/Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, hamna kabila ambalo wako strategically kwenye maisha kama Wachaga, lakini Mchaga mtoto, sauti ikishaanza kukomaa, baba anamwambia mtoto hapa nyumbani siyo mahali sahihi pa kukaa. Hata hivyo, Mheshimiwa Nape, hawa watu wanatoa mtaji, mtu anaoa mtaji kwa mtoto wake nenda kaanze maisha.
Leo hii Mheshimiwa Nape unakubali kubeba hiki kimeo, unaiachia TBC bila shilingi! Kwenye hili ndugu yangu, siko na wewe. UKAWA moto, Mlinga moto, CCM moto, kazi unayo kaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha ajabu zaidi, TBC imeachwa bila shilingi. Katika Wilaya 81 TBC haipatikani, hasa Wilaya za mipakani; wanasikiliza redio za Uganda, Rwanda, Malawi na Congo. Cha kusikitisha zaidi kabisa TBC ndiyo inaongea taarifa za ukweli kuhusu Serikali. Sasa nchi zetu za majirani wakiamua kutuhujumu tunatokea wapi? Kwa hiyo, katika huu muda mfupi, hii nusu saa iliyobaki, tafuta mifuko ya mbele ya nyuma, ongezea hela kwenye TBC. Najua shilingi unazo nyingi, lakini mimi nitatoa hata noti nitaondoka nazo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni timu ya Taifa. Waheshimiwa Wabunge wote ni mashahidi, ule mchakato wa kuwapata wachezaji wa timu ya Taifa huwa ni wa ukurupukaji. Utasikia ikitokea mechi ndiyo wanaanza kukusanya wachezaji, tena wachezaji wenyewe mnawatoa mjini. Nimewaambia Waheshimiwa Wabunge mwambieni Waziri wa Barabara aweke lami Ulanga upite uje uchukue wachezaji kule wapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hiyo timu ya Taifa wana maslahi duni, hawana mtu wa kuwafanyia counseling. Mtu anatoka na stress zake za maisha, hajalipa kodi ya nyumba, kesho unamwambia akacheze na Misri, atawafungia wapi? Hii tutakuwa tunacheza makida makida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna timu imeenda India under seventeen sijui, sina uhakika sana, lakini ile timu nenda kaulize wale watoto wamewatoa wapi? Hawajawapa chochote, wamewabeba tu juu juu, wamewapeleka huko India, mnategemea mtapata nini? Wanaenda kuwakilisha au wanaenda kuchukua ushindi? Mimi nadhani hawa wote wanaenda kuwakilisha, lakini hatuna strategy kwa ajili ya kuendeleza michezo yetu.
Mheshimiwa Nape, wakati unahitimisha naomba uniambie ni manufaa gani Taifa limepata kwa ile sports academy iliyoanzishwa? Kama ipo bado. Maana yake inaweza isiwepo kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uwanja wa Taifa umejengwa kwa shilingi bilioni 60. Ukihitimisha ningependa kujua mpaka sasa hivi ule uwanja umeingiza kiasi gani? Isije ikawa pango la watu wapigaji wa pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kocha wa Taifa, Serikali iliyopita nilikuwa nasikia Mheshimiwa Rais anasema anatoa hela, nataka nijue, utaendelea ule utaratibu au ndiyo vile? Ndugu zangu UKAWA leo pumzikeni. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye vyombo vya habari. Waheshimiwa Wabunge, naomba nimpongeze ndugu Reginald Mengi kwa mfumo aliouweka katika vyombo vyake vya habari (IPP Media). Angalia gazeti la Nipashe, linaandika habari ina-balance ndiyo maana linaendelea ku-exist wafanyakazi wanalipwa vizuri, ndiyo maana hawachukui habari za mtaani. Wamiliki wa vyombo vya habari, naomba mumuige Reginald Mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaanzisha vyombo vya habari, mnategemea waandishi waende wakajikodolee hela huko. Kuna gazeti juzi liliandika habari za Mlinga, lile gazeti tangu lianze halijawahi kufika Ulanga. Zilipelekwa copy 1,000! Waheshimiwa Wabunge, niliwaambia mimi ni mdogo kwa umbo, mkifika Ulanga kule mimi ni mkubwa kuliko hili jengo. (Kicheko)
Waheshimiwa Wabunge, kweli zile copy zilipofika Mto Kilombero zikatumbukia, zikapotelea huko. Ni kweli Waheshimiwa Wabunge, naomba TBC wamuige Reginald Mengi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimpongeze ndugu Ruge wa Clouds Media; watangazaji wanatangaza unaona kabisa wanavyo-relax, yaani wanapata vitu vizuri kutoka kwa mwajiri wao. Siyo watangazaji wanatanga wamenuna, wanafanya kazi kama wamelazimishwa. Kwa hiyo, naomba muwaige hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye issue ya live. Live, live mnataka nini? Si mna majimbo ninyi. Mlipoomba kura si mliombea majimboni, mnataka muonekane ili iweje? Wabunge wanatukana, wengine ndiyo wanatoa mifano sijui ya Kimbari, mnataka muonekane live ili iweje?
Waheshimiwa Wabunge, Wabunge wengi wanaotaka live walikuwa hawaendi majimboni, wanapiga simu kwenye ma-bar, niangalieni nitaongea; sasa hivi mtakufa kibudu humu humu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ingekuwa kuonekana live, kupiga makele, leo hii tungekuwepo na Mheshimiwa Kafulila, tungekuwepo na Mheshimiwa Mkosamali, walikuwa waongeaji wazuri, wanavimba kwenye ma-desk haya mpaka basi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije issue ya wanamuziki. Naomba nimpongeze Diamond popote ulipo. Ingekuwa amri yangu, tungechonga sanamu la Diamond tukaliweka pale kwenye ule mnara wa askari. Ule mnara tumeuchoka, tungetoa tungeweka sanamu ya Diamond. Ametufikisha mbali! Ni alama, ameitangaza nchi yetu huko mbele; na Serikali hatuna mpango wowote wa kusaidia wanamuziki, wanapenya wenyewe, tunaenda kukutana nao mbele na sisi tunajifanya tunawasaidia, yuko wapi Mr. Nice? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungewawekea mfumo mzuri hawa watu wasingekuwa wanapata shida leo. Yuko wapi Saida Karoli, Kanichambua Kama Karanga? Eeh, hatujawawekea mfumo mzuri.
tumeweka vyombo vya kuwatapeli; sijui kuna BASATA, sijui kuna COSOTA hawa ni wapigaji wa hela za wasanii tu, hamna lolote wanalolifanya. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayaongea haya, ninamaanisha kwa sababu tunawaacha wanamuziki wanafanya wanayoyataka, matokeo yake ndiyo haya ya akina chura, sijui akina nani, mnakuja mnawafungia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sina mengi, ni haya tu yananitosha.